Aina kuu 5 za ngozi, sifa zake na njia ya kuzitunza

Kufahamu aina ya ngozi ndio siraha kuu itakayokuongoza ni kwa namna gani unatakiwa kutunza ngozi yako. 

Ngozi yoyote bila kujali aina, inaweza kuwa na muonekano bora na wa kuvutia iwapo kanuni muhimu za utunzaji zitazingatiwa.

Hata kama ngozi yako imeharibika kiasi gani, ikiwa utafahamu aina ya ngozi yako basi unaweza kurudisha muonekano imara na wa kuvutia wa ngozi yako.

Katika Makala hii tutaangazia aina kuu za ngozi, tabia na kanuni muhimu za utunzaji kwa kila aina ya ngozi.

Aina kuu za ngozi

Ngozi imegawanyika katika makundi tofauti kwa kuzingatia vigezo mbalimbali. 

Baadhi ya vigezo ambavyo hutumika kutambua aina ya ngozi ni pamoja na;
  • Tofauti ya kiwango cha melanini katika ngozi
  • Hali ya wekundu katika ngozi
  • Uangavu wa ngozi
  • Kiwango cha mafuta katika ngozi
  • Kiwango cha unyevu katika ngozi
  • Unyororo wa ngozi
  • Uwepo wa makunyanzi na mikunjo katika ngozi
  • Aina na ukubwa wa mashina ya vinyweleo
  • Kiwango cha maji katika ngozi
  • Uimara wa ngozi (kulegea au kukaza kwa ngozi)
  • Unene wa ngozi
  • Uwezo wa ngozi kunyumbulika
Kutokana na vigezo hivi kuna aina kuu 5 za ngozi ambazo ni;
  • Aina ya kwanza ni ngozi ya kawaida
  • Pili ni ngozi yenye mafuta
  • Tatu ni ngozi kavu
  • Nnne ni ngozi nyeti
  • Na tano ni ngozi yenye mafuta na ukavu kwa wakati mmoja

01: Ngozi ya kawaida.

Ikiwa uko kwenye kundi la watu wenye ngozi hii basi jiite mwenye bahati. Bila shaka utakuwa ni mtu ambaye kila mtu anaisifia na kuihusudu ngozi yako kwa muonekano wake.

Aina hii ya ngozi ya kawaida huwa na tabia zifuatazo:
  • Kiwango cha melanini huwa na mlinganyo kiasi cha kuifanya ngozi kuonekana yenye rangi moja
  • Ngozi katika kundi hili haina madoa wala mapunye
  • Ngozi huwa nyororo na yenye kung’ara
  • Haina mafuta mengi wala sio kavu
  • Mashina ya vinyweleo huwa ni madogo na ya kawaida
Aina hii ya ngozi haihitaji matunzo makubwa ili kuwa na muonekano mzuri. Ni ngozi ambayo haipati matatizo ya mzio mara kwa mara na inaweza kuvumilia aina tofauti za mafuta na vipodozi bila kuleta madhara.

02: Ngozi ya mafuta mengi

Hii ni aina ya ngozi ambayo huzalisha kiwango kikubwa cha ute wa sebamu. Ute huu una mchanganyiko wa vitu mbalimbali kama vile maji, mafuta na jasho.

Mafuta katika ute huu huifanya ngozi yako kuwa na muonekano wa kung’ara na wenye mafuta muda wote.

Ngozi ya mafuta huwa na tabia zifuatazo;
  • Huwa na muonekano wa mng’ao wa mafuta.
  • Mashina ya vinyweleo huwa ni makubwa
  • Inaweza kuonesha mabaka mithili ya tone la mafuta hasa baada ya kujisafisha
  • Mabaka au mapunye maeneo ya kidevu na komwe
  • Ngozi hii huwa ni nene na si rahisi kupata makunyanzi
Changamoto kubwa ya aina hii ya ngozi ni kudhibiti kiwango cha mafuta katika ngozi. Unatakiwa kuwa makini katika kuchagua aina ya vipodozi ambayo ni rafiki wa ngozi yako.

Njia bora ya kutunza ngozi ya mafuta ni kuchagua vipodozi na mafuta ambayo husaidia kufyonza mafuta katika ngozi.

03: Ngozi nyeti

Hii ni aina ya ngozi ambayo ina changamoto nyingi za utunzaji kulingana na udhaifu wa aina hii ya ngozi katika mazingira kwa ujumla.

Ni ngozi ambayo huaribiwa kirahisi na vipodozi, jua na baadhi ya vyakula. Watu wenye aina hii ya ngozi wanapaswa kuwa na tahadhari zaidi juu ya kile wanachokula na kuwaka katika ngozi.

Ngozi nyeti huwa na tabia zifuatazo:
  • Ni ngozi nyembamba na kavu
  • Ni rahisi kupata matatizo ya mzio
  • Ngozi hii huwa nyepesi kiasi ambacho mishipa ya damu inaweza kuonekana hasa maeneo ya mikono
  • Ngozi hii huwa na makunyanzi muda wote
  • Maeneo ya mashavu na kidevu huwa na rangi ya wekundu inayotokana na mishipa ya damu kuwa karibu zaidi
  • Ngozi huwa na wekundu hasa wakati wa baridi kali
  • Ngozi hii huwa na muonekano wa wekundu baada ya kutumia aina fulani ya vyakula kama vile pilipili
  • Muonekano wa sura huwa ni wa kupooza wenye makunyanzi ambayo huwa na muonekano wa kuvimba
Changamoto kubwa ya aina hii ya ngozi katika utunzaji ni ugumu wa kupata vipodozi ambavyo ni rafiki wa ngozi hii. Kwa kawaida vyakula ndio nguzo kuu katika utunzaji wa aina hii ya ngozi

04: Ngozi yenye mafuta na ukavu

Hii ni ngozi yenye changamoto zaidi katika utunzaji kutokana na tabia za ngozi hii. Ni ngozi ambayo Baadhi ya maeneo huwa na tabia ya mafuta, huku Baadhi ya maeneo huwa na tabia ya ukavu.

Tofauti na aina nyingine za ngozi, aina hii ya ngozi mara nyingi husababishwa na sababu za kibaolojia za kurithi.

Ngozi hii huwa na tabia zifuatazo:
  • Huwa na mabaka mithili ya vibarango katika baadhi ya maeneo
  • Ngozi huwa nyepesi
  • Huwa na muonekano hafifu usio na mg’ao
  • Huwa na mgawanyo wa melanini usio na mlinganyo hivyo kufanya ngozi yako kuwa na muonekana wa rangi tofauti katika maeneo mbalimbali ya ngozi
  • Ngozi haitoi mafuta mengi
Changamoto kubwa ya aina hii ya ngozi ni kuifanya ngozi hii kuwa na muonekano wa rangi moja usio na mabaka.

Vipodozi maalumu kwa ajili ya kurekebisha uzalishwaji wa melenini au matumizi ya foundation kwa ajili ya kuziba mabaka ni miongoni mwa njia bora za kuimarisha muonekano wa ngozi yako.

Vilevile vyakula sahihi kama vile vitamini ni mambo ambayo yanaweza kukusaidia kuboresha afya ya ngozi yako.

05: Ngozi ya chunusi

Jina lisikuchanganye, ngozi ya chunusi haimaanishi ngozi ambayo tayari ina chunusi bali inamaanisha ngozi ambayo ni rahisi kupatwa na chunusi kuliko aina nyingine yeyote ya ngozi.

Ngozi hii ni rahisi kupatwa chunusi ikiwa utatumia vipodozi au kula vyakula ambavyo sio sahihi.

Vilevile athari mbalimbali za mazingira kama vile uchafu, wadudu, poleni na kemikali katika bidhaa mbalimbali, vyote hivi vinaweza kusababisha ngozi hii kupatwa na chunusi

Ngozi ya chunusi huwa na tabia zifuatazo:
  • Huwa na mafuta mengi
  • Ni rahisi kuathiriwa na mzio
  • Ni rahisi kupatwa na chunusi
  • Inaweza kutengenezwa chunusi zisizo na usaha zenye kichwa cheupe au cheusi
  • Wakati mwingine inaweza kutengenezwa chunusi zenye usaha
  • Chunusi kubwa mithili ya jipu huweza kujitokeza na kuacha kovu
Kwa mtu mwenye ngozi ya aina ya chunusi, changamoto ni kuhakikisha kwamba ngozi yako huathiriwa na chunusi.

Unaweza kufanikisha hili kwa kuzingatia aina sahihi ya vipodozi, Kubadili mtindo wako wa maisha na lishe bora.

Hitimisho

Vinasaba ndio huamua aina ya ngozi yako. Kisayansi, kila mtu ngozi imeangukia katika moja ya makundi haya 5 ya ngozi.

Bila kujali aina ya ngozi, unaweza kuwa na muonekano bora wa ngozi yako kwa kuzingatia kanuni muhimu za utunzaji sahihi wa ngozi yako.

Vipodozi vinaweza kuwa muhimu kwako lakini vinaweza visiwe suluhisho sahihi kwa matatizo yako ya ngozi.

Vipodozi, chakula, lishe na mitindo ya maisha kwa pamoja ndio vinaweza kukupa matokeo bora katika utunzaji wa ngozi yako.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url