Fahamu sababu kuu za tatizo la UTI

Mfumo wa mkojo ni moja ya mifumo inayoshambuliwa sana na vimelea vya magonjwa. Bakteria, virusi na fangasi vyote hivi huweza kuushambulia mfumo huu pamoja na ogani zake.

Vimelea hawa husababisha kundi la matatizo mbalimbali katika mfumo wa mkojo yajulikanayo kama Maradhi katika mfumo wa mkojo au maarufu kama UTI.

Tatizo la UTI linaweza kuathiri eneo lolote la mfumo wa mkojo kama vile;
  • kusababisha uvimbe katika milija ya urethra
  • maradhi ya figo
  • uvimbe na maradhi ya kibofu
  • mara chache matatizo katika milija ya mkojo(ureta).

UTI husababishwa na nini?

Moja ya bakteria ambaye hushambulia zaidi mfumo wa mkojo ni Escherichia Coli (E. coli).

Kwa kawaida bakteria huyu wa E. coli huishi ndani ya mwili wa binadamu na makazi yake rasmi ni katika mfumo wa chakula.

Akiwa katika mfumo wa chakula, bakteria huyu ni salama na rafiki wa mwili kwa sababu husaidia kuimarisha afya na utendaji kazi wa mfumo wa chakula.

Lakini bakteria huyu anapokua katika mifumo mingine hususa ni mfumo wa mkojo hugeuka na kuwa moja ya adui hatari zaidi kwa afya yako.

Tatizo la UTI huambukizwa kwa njia gani?

Kuna njia tofauti ambazo bakteria huyu anaweza fika katika mfumo wa mkojo, njia hizo ni pamoja na ;
  • kinyesi kugusa maeneo ya mfumo wa mkojo au mfumo wa uzazi (mfano ukeni na uumeni),
  • kwa njia ya damu ingawa njia hii ni nadra sana,
  • vilevile kwa njia ya kujamiana.
Kutokana na namna bakteria huyu anaweza kusafiri, wanawake ndio kundi la waathirika wakuu wa ugonjwa huu kutokana na biolojia ya maumbile.

Kulingana na maumbile ya mfumo wa uzazi wa wanawake ni rahisi zaidi kwa uchafu kutoka haja kubwa kufika ukeni hasa wakati wa kujisafisha ukilinganisha na wanume.

Mbali na E. coli, Vimelea wengine ambao husababisha maradhi katika mfumo wa mkojo ni pamoja na
  • E. coli huchangia 75% ya maambukizi,
  • Proteus mirabilis huchangia 5% ya maambukizi,
  • Enterobacteriaceae huchangia 5% ya maambukizi,
  • Enterococcus spp. huchangia 5% ya maambukizi,
Staphylococcus saprophyticus huchangia 5% ya maambukizi, lakini 30% ya maambukizi kwa mabinti wadogo

Wengineo ni Staphylococcus aureus, Candida albicans, Mycobacterium tuberculosis.

Njia ambazo tatizo la UTI husambaa?

#1: Maumbile ya kibaolojia.

Hii ni moja ya sababu inayofanyaa wanawake kuwa katika hatari kubwa ya kupata maradhi ya UTI kuliko wanaume kwa sababu wanawake wana milija ya urethra ambayo ni mifupi.

Kwa hivyo ni rahisi zaidi kwa uchafu kutoka haja kubwa kufika ukeni kisha kuingia ndani ya mfumo wa uzazi kupitia milija ya urethra hasa wakati wa kujisafisha.

Lakini pia muingiliano wa majimaji ya ukeni na uchafu wa haja kubwa unaweza kusababishwa wakati wa kujamiana hasa wa wale wapenzi ambao huingiliana kinyume na maumbile.

Kwa wanaume hali ni tofauti kwa vile wana milija ya urethra mirefu na iko mbali zaidi na puru hii inafanya kuwa vigumu kwa uchafu wa haja kubwa kugusana na ncha ya uume.

#2: Uwepo wa uvimbe, makovu au tiba za milija.

Uvimbe au makovu katika mfumo wa mkojo unapelekea urahisi wa bakteria kujishikiza, kwa kawaida mfumo wa mkojo umeundwa kwa sele ambazo huzalisha ute na seli za ulinzi.

Ute husaidia kuviteka vimelea na seli za ulinzi husaidia kuvishambulia. Uvimbe au kovu katika mfumo wa mkojo hupunguza uzalishaji wa ute na seli hizi za ulinzi.

Jambo hili linapelekea ulinzi wa mfumo mzima kudhoofika kiasi kinachopelekea kiwango kidogo tu cha bakteria kinatosha kukusababishia maradhi.

Vilevile watu ambao wako katika tiba za milija au mipira, ambayo huwasaidia kupunguza maji mwilini au kutoa haja ndogo wako katika hatari zaidi kwa kuwa bakteria hutumia milija au mipira hiyo kupita na kuingia katika mfumo wa mkojo.

Kwa watu hawa usafi na kufuata maelekezo ya kitaalamu kunaweza kupunguza athari za kupata maambukizi.

#3: Kutokuwapo kwa ulinganifu wa chaji katika mfumo wa mkojo.

Kiwango cha chaji hupimwa katika kipimo kijulikanacho kama PH ambapo kwa kawaida kipimo hiki kinapaswa kusoma kati ya PH ya 4 hadi 8 katika mfumo wa mkojo, yaani mfumo wa mkojo unapaswa kuwa katika hali ya tindikali kwa ufanisi zaidi.

Ikitokea mabadiliko ya PH katika mfumo huu basi hudhoofisha kinga na kupelekea kutawaliwa kiurahisi na backteria.

PH ya mfumo wa mkojo huathiriwa zaidi na magonjwa, vyakula na mabadiliko mengine ya kibaolojia kama vile hedhi.

Mabadiliko ya PH huwa makubwa zaidi kwa mama mjamzito na hii hufanya kundi hili kuwa ni kundi hatari zaidi kushambuliwa na maradhi ya mfumo wa mkojo(UTI).

#4: Uwepo wa sukari katika mkojo.

Kwa mgonjwa wa kisukari kinga yake ya mwili huwa chini sana kiasi kwamba bakteria yeyote anaweza kumletea matatizo makubwa ya kiafya.

#5: Kubana mkojo.

Ikiwa umebanwa na mkojo, kojoa. Kojoa mpaka ujiridhishe kwamba mkojo umekwisha katika kibofu, kwa kuwa kutofanya hivyo kunaongeza nafasi ya kupata maradhi katika mfumo wa mkojo (UTI).

Kuacha mkojo kutuwama kwa muda mrefu kunawapa bakteria muda wa kuweka makazi katika mfumo huu, kitendo kinachoweza kusababisha wakazaliana kwa wingi kiwango cha kuleta madhara.

Kumbuka bakteria huzaliana mamilioni ndani ya sekunde. Hakikisha unakojoa mara mkojo unapokubana hii inasaidia kuzuia bakteria kutuwama lakini pia husaidia kuuosha mfumo wa mkojo.

Sababu na njia nyingine ambazo ugonjwa wa UTI husambaa ni;
  • Wajawazito
  • watu wenye matatizo ya milija kujikunja
  • matatizo ya mfumo wa fahamu
  • watu wenye uvimbe katika maeneo ya mfumo wa mkojo
  • tezi dume

#6: Matumizi ya dawa na ngono zembe.

Matumizi ya dawa mbalimbali kama vile dawa za fangasi, dawa za kutibu maradhi ya bakteria na dawa za uzazi wa mpango huathiri hali ya mlinganyo wa kiutendaji katika mfumo wa mkojo.

Dawa za fangasi na bakteria huua wadudu wa faida ambao hufanya kazi nyingi ikiwemo kuleta mlinganyo wa chaji au PH katika mfumo wa mkojo. Tumia dawa hizi kwa tahadhari.

Pia matumizi ya taulo za kike(pedi) au viuaji vya manii huweza kusababisha bakteria kuzaliana hasa ikiwa usafi hautazingatiwa.

Kujamiana hovyo si salama kwa afya yako pia kwa vile unaweza kupata maambukizi ya magonjwa ambayo yanachagiza maambukizi katika mfumo wa mkojo au maambukizi ya mfumo wa mkojo ikiwa utakutana na mtu ambaye tayari ameathirika.

Jambo linguine la kufahamu ni kwamba majimaji ya uke au uume yanatofautiana michanganyiko yake hasa chaji au PH kwa hivyo migusano ya maji haya huweza kubadili hali ya chaji au kuua vimelea vya faida katika mfumo wa mkojo.

Kumbuka chochote kinachoweza kuathiri mfumo wa uzazi ni rahisi sana kuathiri mfumo wa mkojo kwa vile mifumo hii iko karibu sana na kuna baadhi ya ogani au viungo vinachangia.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url