Tatizo la UTI sugu, aina zake, chanzo, dalili na tiba

UTI ni maambukizi ya kawaida ambayo hutokea endapo vimelea wa magonjwa hasa bakteria aina ya E. coli waishio kwenye ngozi na mfumo wa chakula huingia kwenye urethra, na kusababisha maambukiza katika njia ya mkojo.

Maambukizi yanaweza kuathiri sehemu kadhaa za njia ya mkojo, lakini kibofu, figo ni baadhi ya maeneo ambayo huathiriwa zaidi.

Aina ya maradhi ya mfumo wa mkojo na jinsi ya kutibu.

Tatizo la maradhi ya mfumo wa mkojo (UTI) limegawanywa katika namna kuu mbili ambazo ni;
  1. Mgawanyo unaozingatia eneo lililoathiriwa.
  2. Mgawanyo unaozingatia ni kwa jinsi gani tatizo ni kubwa.

Mgawanyo unaozingatia eneo lililoathiriwa

Katika mgawanyo huu UTI imegawanywa katika aina kuu mbili ambazo ni;
  • Maradhi ya sehemu ya chini ya mfumo wa mkojo: Ambapo milija ya urethra na kibofu ndio huwa vimeathiriwa Zaidi.
  • Maradhi ya sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo: Ambapo milija ya uleta, mlango wa figo na figo lenyewe ndio huwa vimeathiriwa zaidi.

Mgawanyo unaozingatia ukubwa wa tatizo

Mgawanyo wa pili ni kuzingatia kiwango na athari ya maambukizi katika mfumo wa mkojo. Katika mgawanyo huu kuna aina kuu mbili za maradhi ya mfumo wa mkojo ambazo ni;
  • Maradhi ya kawaida ya mfumo wa mkojo: Ambapo maeneo mbalimbali ya mfumo wa mkojo huwa yameathiriwa bila kuathiri eneo linalounganisha mfumo wa fahamu na mfumo wa mkojo, eneo hili linalounganisha mifumo hii hupatikana katika mfumo wa mkojo.
  • Maradhi tata/sugu ya mfumo wa mkojo (UTI sugu): Ambapo sehemu kubwa ya mfumo wa mkojo huwa imeathiriwa huku sababu kubwa ikiwa ni tatizo la kimaumbile au matatizo katika mfumo wa fahamu wa eneo la mfumo wa mkojo. Aina hii ya pili ni ngumu kuitibuklingana kutokana na utata wake.

Maradhi ya UTI katika makundi mbalimbali ya waathirika.

Watoto wadogo.

Maradhi ya mfumo wa mkojo (UTI) kwa Watoto husababishwa zaidi na sababu za kibaolojia ambapo mtoto huzaliwa na tatizo katika moja au zaidi ya ogani moja ya mfumo wa uzazi haifanyi kazi vizuri.

Mfano mtoto anazaliwa milija yake ya ureta imejikunja. Katika hali hii mtoto hushindwa kutoa mkojo, wakati mwingine mkojo hurudi katika figo badala ya kuingia katika kibofu. Hii hupelekea Watoto wa aina hii kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya UTI.

Kurudi kwa mkojo katika figo kunaweza sababisha maradhi ya figo, maradhi yanayoweza kupelekea figo na sehemu nyingine za mfumo wa mkojo kuachwa na makovu. Makovu katika figo ni chanzo kikubwa cha figo kushindwa kufanya kazi.

Watoto ni kundi kubwa ambalo huwa katika hatari ya kushambuliwa na UTI sugu. Mzazi au mlezi hakikisha unafika kituo cha afya kwa matibabu zaidi ikiwa mtoto wako ataonyesha dalili zozote za UTI.

Wajawazito.

UTI kwa wajawazito inaweza kupelekea maradhi ya ghafla ya figo (hasa milija ya kuchuja mkojo), maradhi haya husababisha kudumaa kwa mfuko wa uzazi, kuzaa mtoto njiti, na matatizo mengine mengi ya mimba.

Kwa wajawazito wanatakiwa kupima UTI hata kama haoneshi dalili zozote.

UTI kwa watu wenye umri mkubwa.

UTI ni tatizo la kawaida kuwapata wazee hasa kuanzia umri wa miaka zaidi ya 50. Sababu kubwa ni kwamba wazee hawa kuwa na uwezo mdogo wa kujijali.

Kwa wanaume uwezekano wa kupata UTI huongezeka mara dufu baada ya miaka 50 kwa sababu ya tatizo la tezi dume.

Wenye magonjwa sugu.

Watu wenye matatizo ya kisukari na matatizo ya figo kama vile mawe katika figo wapo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya UTI sugu.

Wagonjwa wanaotumia mipira au mirija.

Wagonjwa wote ambao hutumia tiba ya mirija au mipira kwa ajili ya haja ndogo wako katika hatari zaidi ya kupata UTI, na uwezekano huwa mkubwa zaidi pale ambapo mirija au mipira hiyo hukaa mwilini kwa muda mrefu.

Watu hawa hupata UTI sugu ambayo huwa ni ngumu zaidi kuitibu na inahitaji kuondolewa kwa mirija au mipira hiyo.

Dalili za UTI

Zipo dalili nyingi na tofauti ambazo huashiria uwepo wa UTI. Baadhi ya dalili izo ni pamoja na;
  • Kuhisi kubanwa mkojo na kuwa na hamu ya kukojoa lakini kiwango cha mkojo kinachotoka ni kidogo.
  • Kupata maumivu wakati wa kukojoa.
  • Maumivu maeneo ya chini ya kitovu.
  • Mkojo uliochanganyikana na damu, ikiwa sehemu za ndani zimepata majeraha.
  • Huambatana na homa kali na mwili kuchoka.
  • Kichefuchefu na kutapika.
  • Kushindwa kula hasa Watoto.
  • Kupoteza kumbukumbu hasa kwa wazee.

Jinsi ya kutibu maradhi ya mfumo wa mkojo (UTI).

Ili kutibu tatizo la UTI, mambo kadhaa yanapaswa kuzingatiwa. Mambo hayo ni kama yafuatayo;
  • hali ya mgonjwa kiafya,
  • aina ya UTI, umri,
  • jinsia na historia ya matibabu iwapo mgonjwa amewahi tibiwa UTI.

Tiba za kisasa.

Mgonjwa atapewa dawa aina ya antibiotiki ambazo huua na kuangamiza bakteria wanaosababisha tatizo la UTI.

Aina ya antibiotiki, kiwango na muda wa matumizi hutofautiana kati ya mgonjwa, mfano mtoto, mjamzito na mzee, matibabu yao hutofautiana kulingana na hali zao.

Baadhi ya dawa ambazo hutumiwa zaidi Tanzania kutibu UTI ni pamoja na Ciprofloxacin, Amoxycillin + Clavulanic acid(co-amoxiclav), ceftriaxone na doxycycline.

Tiba za mitishamba.

Kutokana na usugu wa dawa za kisasa kwa bacteria hawa wa E. coli, matumizi ya mitishamba yanaweza kuwa ni chaguo bora zaidi katika kutibu tatizo la UTI.

Utafiti wa kitaalamu unaonyesha matunda aina ya Beriberi ni moja ya tiba za uhakika za UTI bila kujali aina ya UTI.

Matumizi ya beriberi katika mfumo wa unga huonyesha ufanisi zaidi ambapo inapendekezwa kutumia beriberi kati ya milligram 400 – 600 kila siku kwa muda usiopungua miezi 2.

Mitishamba mingineyo ni pamoja na kitunguu saumu.

Njia za kujikinga na UTI.

Yapo mambo mengi ambayo unaweza kuyafanya ili kuepukana na matatizo ya maradhi ya mfumo wa mkojo (UTI). Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na;
  • Kunywa maji mengi na ya kutosha.
  • Kuwa na kiasi au epuka matumizi ya vinywaji kama pombe na kahawa kwasababu zina haribu kibofu.
  • Hakikisha unakojoa mara tu umalizapo kujamiana.
  • Zingatia usafi hasa wakati wa kujiosha nyeti zako, hakikisha unaosha kutoka mbele kwenda nyuma na si vinginevyo, hii ni ya kuzingatia zaidi kwa wanawake.
  • Zingatia usafi uke au uume na nguo unazovaa.
  • Epuka matumizi ya manukato sehemu za ukeni au uume.

Hitimisho

Unashauriwa kuonana na mtaalamu wa afya mara tu uonapo dalili zozote zinazoashiria uwepo wa UTI. Kwa kufanya hivyo unaonyesha kujali na kuuthamini afya yako
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url