Jinsi ya kuhesabu mzunguko wa hedhi wa siku 28 na 32.

Mzunguko wa hedhi ni moja ya tukio muhimu zaidi la kibaolojia kwa mwanamke. Mwanamke yoyote ambaye amefikia balehe na hana matatizo yeyote katika mfumo wake wa uzazi ni lazima apate hedhi.

Tukio hili ni muhimu sana kwa mwanamke kwa kuwa hutoa ishara kwamba via vya uzazi vya mwanamke vimekomaa na tayari kwa kushika mimba.

Kwa kawaida tukio hili la mzunguko wa hedhi huchukua wastani wa siku 28 kukamilika.

Siku 28 ni wastani tu, kwa maana ya kwamba kundi kubwa la wanawake mzunguko wa hedhi ni siku 28.

Lakini pia wapo wanawake wengi ambao mzunguko wao ni kati ya siku 21 hadi 35.

Bila kujali urefu wa mzunguko wako, jambo la msingi kwa mwanamke ni kuwa na uhakika wa urefu wa siku za mzunguko wake wa hedhi.

Faida za kujua mzunguko wako wa hedhi.

Kutokana na umuhimu wa tukio hili ni vyema mwanamke kufahamu kwa kina kuhusu mzunguko wake wa hedhi kwa manufaa na faida zifuatazo;
  • Hedhi inatoa ishara ya kwamba mwanamke anaweza kushika ujauzito.
  • Kupevuka kwa mayai ya uzazi ya mwanamke ni sehemu ya tukio hili la kibaolojia, hivyo husaidia mwanamke kushika mimba.
  • Kukusaidia kufahamu ni wakati gani mwanamke anakuwa katika nafasi nzuri ya kupata ujauzito.
  • Unaweza kutumia mzunguko wako wa hedhi kama njia mojawapo ya uzazi wa mpango.
  • Mabadiliko katika mzunguko wa hedhi yanaweza kutumika kugundua kasoro mbalimbali za kiafya katika mfumo wa uzazi wa mwanamke.

Jinsi ya kuhesabu mzunguko wa hedhi.

Ni rahisi sana kwa mwanamke kutambua mzunguko wake wa hedhi.

Tangu enzi za kale njia ya kalenda ndio njia kuu iliyotumika kufuatilia na kutambua mzunguko wa hedhi kwa mwanamke.

Njia hii ndio ambayo hutumiwa zaidi mpaka sasa ambapo mwanamke analazimika kufuatilia, kutambua na kuweka kumbukumbu ya matukio muhimu wakati wa kipindi chote cha mzunguko wa hedhi.

Mzunguko wa hedhi ili ukamilike umegawanywa katika hatua kuu tatu.

Hatua hizo ni
  1. kipindi cha kutoka damu (hedhi),
  2. Pili ni kipindi cha yai kupevuka na
  3. Tatu ni kipindi cha yai na ukuta wa tunbo la uzazi kuharibika.
Katika hatua zote hizi kuna mabadiliko muhimu ambayo mwanamke anapaswa kuyang’amua na kuyarekodi kama sehemu ya ufuatiliaji wa mzunguko wake wa hedhi.

Baadhi ya mabadiliko muhimu yanayopaswa kunukuliwa katika mzunguko wa hedhi ni pamoja na;
  • Kutokwa damu.
  • Mabadiliko ya joto.
  • Hamu ya kujamiana.
  • Maumivu na tumbo.
  • Hali ya msawazo wa kimwili.
  • Ute wa aina tofauti katika hatua tofauti za mzunguko.

Jinsi ya kuhesabu mzunguko wa hedhi siku 26, 28, 30 na 35.

Mzunguko wa hedhi huanza kuhesabiwa siku ya kwanza ya hedhi (kutokwa damu).

Iwapo utaona damu basi hesabu siku hii kama siku ya kwanza ya mzunguko.

Kwa wanawake wengi siku hii huambatana na homa na maumivu makali masaa machache kabla ya damu kuanza kutoka ama wakati damu ikiendelea kutoka.

Maumivu na homa huweza kuendelea kwa kipindi chote cha damu kutoka ama yakaisha siku ya kwanza a damu kutoka.

Ikiwa homa na maumivu yatakuwa makali sana mwanamke anaweza kutumia dawa za kutuliza maumivu na homa kwa msaada.

Kwa wanawake wengi hatua hii ya kutoka damu huweza kudumu kwa kati ya muda wa siku 2 hadi 7 kutegemea na urefu wa mzunguko.

Ambapo kwa kawaida hatua hii;

  • Huchukua siku 2-3 kwa wale ambao mzunguko wao ni kati ya siku 21-24.
  • Siku 3-4 kwa wale ambao mzunguko wao ni kati ya siku 26-28.
  • Na siku 5-7 kwa wale ambao mzunguko wao ni kati ya siku 30-35.
Baada ya hatua ya kutoka damu kuisha. Yaani ya damu kukata mzunguko wa hedhi huingia hatua nyingine.

Katika hatua hii ukuta wa mfuko wa uzazi huanza kutengenezwa na mchakato wa yai kupevushwa huanza.

Hatua hii inachukua kati ya siku 5 hadi 10 kulingana na urefu wa mzunguko.

Hivyo basi baada ya damu kukata endelea kuhesabu siku zako kama ilinavyoainishwa hapa chini.

Mzunguko hedhi wa siku 28.

Mara nyingi wanawake katika kundi hili hutokwa damu ya hedhi kwa siku 3 mfululizo na kumalizika siku ya 4.

Kwa kundi hili la wanawake baada ya kumalizika hedhi siku 3 au 4.

Mwili hutumia siku 6 hadi 7 kuandaa mji mpya wa uzazi ambao utasaidia ukuaji wa mtoto ikiwa yai lake litarutubishwa.

Hivyo basi endelea kuhesabu kutoka siku ya kumaliza hedhi kwa kuchukua siku tatu au nne za hedhi jumlisha siku 7 au 6 za ukuta wa mfuko wa uzazi kutengenezwa ili upate jumla ya siku 10.

Hesabu kutoka siku ya kwanza ya kutoka damu hadi siku ya 10. Siku hizi 10 za mwanzo hutajwa kama siku salama za mzunguko.

Katika kipindi hiki uwezekano wa kupata ujauzito ni mdogo hasa siku nane za mwanzo yaani siku 5 baada ya damu kukata.

Lakini uwezekano wa kushika ujauzito huongezeka kadri unavyokaribia siku ya kumi.

Kuanzia siku ya 11 hadi 16;

Kwa mwanamke ambaye mzunguko wake ni siku 28, siku ya 11 hadi 16 hutajwa kama siku za neema kwa vile ni katika kipindi hiki uwezekano wa kupata ujauzito ni zaidi ya 80%.

Uwezekano wa kushika mimba huongezeka na kufikia 100% siku ya 13 na 14.

Kuanzia siku ya 11 yai huanza kupevushwa na siku ya 13-14 yai linakuwa tayari limeshatoka katika ovari kuelekea mfuko wa uzazi.

Likiwa nje ya ovari yai linaweza kuishi kwa takribani masaa 72 yaani siku 3.

Baada ya siku 3 yai linakufa na linapoteza uwezo wa kurutubishwa.

Kwa hivyo siku ya 11 hadi siku ya 16 ya mzunguko kwa wanawake ambao mzunguko ni wa siku 28 ni siku ambazo anapaswa kuwa mwangalifu kutokana na uwezekano mkubwa wa kushika ujauzito.

Kipindi hiki ni rahisi kukitambua kwa vile huambatana na dalili zifuatazo;
  • Hamu ya kujamiana inaongezeka kupita kawaida.
  • Kutokwa na ute ukeni.
  • Maumivu chini ya tumbo.
  • Matiti kujaa na chuchu kuuma.
  • Uwezo wa kutambua harufu unaongezeka.
Siku ya 17 hadi 28;

Baada ya kipindi cha yai kupevuka kupita, kipindi kinachofuatia ni mchakato mzima wa kuharibika kwa ukuta ukuta wa mfuko wa uzazi uliotengenezwa.

Kipindi hiki huchukua takribani siku 14 kwa wanawake wote bila kujali urefu wa mzunguko wa mwanamke.

Baada ya siku 14 ukuta ulioharibiwa unatolewa kama damu kupisha maandalizi mapya ya mazingira bora ya ukuaji wa mtoto ikiwa yai litarutubishwa.

Kwa hivyo kutoka siku ya 14 jumlisha siku 14 ndio kunakamilisha siku 28 za mzunguko wa hedhi.

Mzunguko wa siku 30

Mara nyingi wanawake hawa hedhi yao huchukua siku 5 hadi 7.

Kama kawaida baada ya hedhi kuisha zinajumlishwa siku 7 ambazo ni muendelezo wa maandalizi ya ukuta na wa uzazi na kupevuka kwa yai.

Kwa ambaye anapata hedhi siku 5 ukijumlisha siku 7 utapata jumla ya siku 12.

Kwa hivyo wanawake katika kundi hili siku salama katika mzunguko wao ni kuanzia siku ya kwanza ya hedhi mpaka siku ya 12.
Siku ya 12 hadi 17 ya mzunguko.

Hizi ni siku za yai kupevuka na kutolewa kutoka katika ovari tayari kwa kurutubishwa.

Kwa hivyo katika kipindi hiki neema ya kupata ujauzito huongezeka kwa 80% na hufikia 100% siku ya 14, 15 na 16.

Baada ya siku ya 17, ukuta uliotengenezwa huanza kuharibiwa na baada ya siku 14 hutolewa nje kama uchafu kwa njia ya damu (hedhi).

Kwa hivyo kutoka siku ya 16 ya mzunguko jumlisha 14 za hatua ya ukuta kuharibika inakamilisha jumla ya siku 30 za mzunguko wa hedhi.

Mzunguko wa siku 32.

Na kwa wale ambao hupata hedhi kwa siku 7 ukijumlisha siku 7 unapata jumla ya siku 14.

Kwa wanawake hawa siku salama katika mzunguko wao ni kuanzia siku ya kwanza ya hedhi mpaka siku ya 14.
 
Siku ya 15 hadi 20 ya mzunguko;

Kwa wanawake ambao hedhi yao ni siku 32 wao siku za neema ya kupata ujauzito ni kati ya siku ya 15 hadi 20 ya mzunguko kutokea siku ya kwanza ya kutoka damu.

Huku uwezekano mkubwa ukiwa ni siku ya 16, 17 na 18.

Kutoka siku ya 18, ongeza siku 14 za hatua ya mwisho ya mzunguko wa hedhi unapata jumla ya siku 32 kukamilisha mzunguko.

Hitimisho.

Kuhesabu mzunguko wa hedhi si jambo rahisi kwa kuwa kuna mambo mengi yanayoweza kuathiri mzunguko wa hedhi.

Ili kujiridhisha na urefu wa mzunguko wako ni vyema kunukuu na kufuatilia mizunguko isiopungua 6 ili kujiridhisha na wastani wa urefu wa mzunguko wako.

Kwa mwanamke ambaye ameanza hedhi yaani amepeta hedhi yake ya kwanza baada ya kubalehe.

Kutengamaa kwa mzunguko wake huchukua takribani miezi 8 mzunguko wake kuwa imara na unaoeleweka.

Kwa wanawake hawa hesabu za kawaida zilizoainishwa hapa juu zinaweza zisiwasaidia kwa kuwa mara nyingi mzunguko wao hukaa sawa baada ya miezi isiyopungua 8.

Zifuatazo ni changamoto ambazo zinaweza kuathiri na kuvuruga hesabu za mzunguko wako wa hedhi;
  • Kupata hedhi yenye damu nyingi.
  • Kukosa hedhi wa miezi kadhaa bila sababu ya msingi ambayo ni ujauzito.
  • Magonjwa.
  • Lishe.
  • Na mitindo ya maisha na mazingira yako kwa ujumla.
Ikiwa unakabiliwa na changamoto yeyote tajwa hapo juu ni vyema kufika kituo cha afya na kupata elimu na ushauri ikiwa changamoto yako inaweza kuwa sababu ya matatizo mbalimbali ya hedhi na mfumo wa uzazi kwa ujumla.

Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url