Jinsi ya kutambua kama una tatizo la uzito mkubwa ( Kitambi).

Moja ya changamoto kubwa kubwa inayowakabili watanzania kwa sasa na dunia kote ni tatizo la ongezeko la uzito kupita kwaida. Asilimia zaidi ya 90 ya watu wanaokumbwa na tatizo la uzito mkunwa huishia kupatawa na tatizo la kitambi.

Tatizo hili linashika kasi kila kukicha na huathiri watu wa rika na jinsia zote kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania huku watu waishio mijini wakiathiriwa zaidi na tatizo.

Ukubwa wa tatizo hili maeneo ya mijini unatokana na mitindo ya ulaji na upatikanaji wa vyakula katika maeneo haya.

Maeneo haya kwa kiasi kikubwa hutegemea vyakula vilivyochakatwa kutoka viwandani, vyakula ambavyo hubeba kiasi kikubwa cha wanga na mafuta.

Vyakula kutoka viwandani vinaweza visiwe tatizo lakini elimu juu ya kiasi sahihi ambacho mtu anatakiwa kula ndio changamoto kubwa.

Katika makala hii tutaangazia tatizo la kitambi kwa ujumla wake na ni kwa namna gani unaweza kufahamu kuwa tayari umeathirika na tatizo hili la kitambi.

Chanzo cha tatizo la kitambi.

Kitambi ni tatizo linalotokana na mlundikano wa chakula cha ziada katika mwili ambacho huifadhiwa katika mfumo wa mafuta.

Chakula hiki hutokana na ziada ya chakula aina ya wanga na sukari mwilini. Kitaalamu mahitaji ya chakula yanategemea na mahitaji ya nishati mwilini.

Kwa kawaida mahitaji ya nishati ya mwili ni kati ya calori 1500 hadi 1900 kwa wanawake na 2000 hadi 2500 kwa wanaume.

Ikiwa mahitaji yako ya mwili ya nishati ni madogo kuliko kiasi cha nishati unachopata kutoka katika vyakula mbalimbali.

Basi chakula hiki hubadilishwa katika muundo wa mafuta na kuhifadhiwa sehemu mbalimbali za mwili katika muundo wa mafuta.

Chakula ambacho hubadilishwa katika muundo wa mafuta na kuhifadhiwa mwilini ni chakula aina ya wanga.

Baadhi ya maeneo ambayo chakula hiki huweza kuhifadhiwa ni;
  • Tumboni kwa sehemu kubwa.
  • Makalioni (matako).
  • Mapajani.
  • Misuli.
  • Ini.
  • Moyo.
  • Mashavuni na
  • Kiunoni.
Mlundikano wa mafuta katika sehemu hii unapelekea ongezeko la uzito wa ziada wa mwili.

Kutokana na hali hii, ongezeko la uzito ni moja ya viashiria muhimu vya uwepo wa tatizo la kitambi.

Kisayansi uzito wa mtu unapaswa kuwa na uwiano na mambo kadhaa kama vile umri, kimo na jinsia.

Kuna njia nyingi za uwianishaji wa uzito wako na mambo ya kibaolojia yanayoathiri uzito katika mwili.

Ikiwa uwianishaji hauko katika uwiano unaopendekezwa kitaalamu basi yawezekana kuna tatizo na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa.

Jinsi ya kutambua uzito wako wa mwili na kupima BMI.

Zipo njia nyingi za kutambua uwiano na uhalali wa wa uzito wako kwa kuzingatia mambo mengine ya kibaolojia ya mwili.

Kwa sasa njia nzuri inayopendekezwa na kutumiwa katika kutambua kiwango cha mafuta katika wa mwili wako ni uzito wako na kimo chako.

Uwiano huu kitaalamu huitwa Body Mass Index, ambao unapatikana kwa kuangalia uwiano wa uzito wako katika kipimo cha kilogramu na kipeo cha pili cha kimo au urefu wako katika kizio cha mita.

Uwiano huu unaweza kukokotolewa kwa kutumia kanuni ya kimahesabu ifuatayo;

BMI = Uzito wako katika kilogramu gawanya kipeo cha pili cha urefu wako katika mita.

BMI = (Uzito)kg / (Urefu katika mita)2

Tafsiri ya majibu utakayoyapata ni kama ifuatavyo. 

Ikiwa;
  • BMI yako ni chini ya 18.5. Hii hutafsiriwa kama una uzito mdogo (kiwango cha mafuta ni kigodo).
  • BMI yako ni kati ya 18.5 – 24.9. Hii hutafsiriwa kama uzito sahihi kiafya(kiwango cha mafuta kiko sawa).
  • BMI yako ni kati 25 – 29.9. Hii hutafsiriwa kama una uzito mkubwa kuliko kawaida (kiwango cha mafuta ni kikubwa).
  • Na ikiwa BMI yako ni zaidi ya 30 hutafsiriwa kama uzito uriokithiri yaani kiwango cha mafuta kikubwa mno na huwekwa katika kundi la watu wenye kitambi.
Licha ya kutumiwa kama kipimo kikuu cha kiwango cha mafuta mwilini, njia hii pia si sahihi kwa asilimia 100%.

Kwa sababu kwa baadhi ya makundi ya watu haipaswi kutumiwa kama njia tegemezi ya kupima kiwango cha mafuta mwilini.

Makundi ambayo hayapaswi kuridhishwa moja kwa moja na aina hii ya kipimo cha mafuta mwilini ni;
  • Wajawazito.
Kwa sababu ni kawaida kwa mjamzito kuongezeka uzito hadi kilogramu 11 ili kukidhi mahitaji ya mtoto tumboni.
  • Watu wenye tatizo la ujazo mdogo wa mifupa.
Kitaalamu tatizo hili huitwa sarcopenia, ambapo mtu huweza kuwa na kiasi kikubwa cha mafuta lakini BMI yake ikawa katika thamani inayokubalika kiafya.
  • Vilevile watu wanofanya mazoezi ya kutunisha misuli.
Watu hawa huwa na uzito mkubwa na BMI yao mara nyingi huonyesha kama wana tatizo la uzito.

Kwa watu hawa uzito wao kwa sehemu kubwa hutokana na kutuna kwa misuli, yaani ni uzito wa misuli na si mafuta.

Hitimisho

Ni muhimu kufahamu BMI yako kwa sababu BMI ni moja ya kipimo muhimu katika kutoa taarifa za uwiano wa lishe na matumizi ya lishe mwilini.madhara ya kiafya ya tatizo la kitambi

Kwa kutumia kipimo hiki tunaweza kufahamu ikiwa una tatizo lolote la utapiamlo ambalo linaweza kuleta madhara ya kiafya.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url