Sababu 10 za kukosa hedhi kwa mwanamke na tiba zake

Tatizo la kukosa hedhi ni hali ya mwanamke kutoona siku zake za kutoka damu katika mzunguko wake wa hedhi wa kawaida. 

Tatizo hili ni miongoni mwa matatizo makuu yanayoathiri mzunguko wa hedhi kwa wanawake na ni chanzo kikuu cha ugumba kwa wanawake.

Kukosa hedhi husababishwa na sababu mbalimbali za kiafya na za kijamii kama vile msongo wa mawazo, lishe na matatizo ya mlinganyo wa homoni.

Baadhi ya sababu hizi ni za kawaida na huweza kutibiwa na tatizo likaisha na mwanamke akaendelea kupata hedhi kama kawaida.

Vilevile tatizo hili huweza kusababishwa na matatizo au magonjwa ya kuzaliwa kama vile tatizo la ukuaji wa tezi za adrenali bila udhibiti.

Tatizo la kukosa hedhi na aina zake  

Kwa kuzingatia umri, sababu na muda wa tatizo, tatizo la kukosa hedhi limegawanywa katika aina kuu mbili ambazo ni; 
  1. Tatizo la kutopata hedhi la awali na 
  2. Tatizo la kutopata hedhi la upili.

01: Tatizo la kukosa hedhi la awali.

Aina hii ya tatizo la kukosa hedhi linahusisha kundi la wanawake ambao hawajawahi kabisa kupata hedhi licha ya kufikisha umri wa balehe.

Wanawake hawa huwa na sifa na vigezo vyote vya mwanamke kupata hedhi lakini hawapati.

Kutokana na utata wake aina hii ya kukosa hedhi inaweza kusababishwa na sababu za kuzaliwa au zisizo za kuzaliwa. 

Ufuatao ni mgawanyo wa aina hii ya kukosa hedhi;

Kukosa hedhi kwa mwanamke asiye na matiti lakini ana mfuko wa uzazi.

Katika kundi hili la wanawake, kukosa hedhi kunaweza sababishwa na mambo yafuatayo;
  • Tezi ya hypothalamus haizalishi homoni ya GnRH.
  • Tezi ya pituitary haizalishi homoni za LH na FSH.
  • Uvimbe na michubuko katika tezi ya hypothalamus.
  • Tatizo la ovari kushindwa kuitikia homoni ya FSH ambayo hupevusha yai.
Kwa sehemu kubwa tatizo hili ni la kuzaliwa nalo ambalo pia huweza kusababishwa na tatizo la Turner’s syndrome (tatizo katika mpangilio wa vinasaba).

Kukosa hedhi kwa mwanamke aliye na matiti lakini hana mfuko wa uzazi.

Mwanamke anaweza kuzaliwa bila mfuko wa uzazi lakini akawa na ovari vilevile tabia za kike zikakua bila shida.

Mfano wa tatizo linaloweza kusababisha hali hii ni androgen-insensitivity syndrome ambapo mwanamke anakosa mfuko wa uzazi lakini anakuwa na ovari ambazo hazina uwezo wa kupokea wala kuhisi homoni za uzazi.

Kukosa hedhi kwa mwanamke aliye na matiti na ana mfuko wa uzazi.

Katika kundi hili la wanawake tatizo husababishwa na sababu sawa na zile zinazosababisha tatizo la kukosa hedhi aina ya upili.

02: Tatizo la kukosa hedhi la upili.

Aina hii ya pili ya tatizo la kukosa hedhi hutafsiriwa katika namna kuu mbili:

Tafsiri ya kwanza:
Hali ya mwanamke kukosa hedhi kwa muda wa miezi sita mfululizo au zaidi kwa wanawake ambao tayari wameshawahi kupata hedhi na mzunguko wao ulikuwa wa kawaida.

Tafsiri ya pili:
Hali ya kukosa hedhi kwa muda wa miezi 3 mfululizo au zaidi kwa wanawake ambao mzunguko wao wa hedhi haujawahi kuwa wa kawaida na unaoeleweka. 

Sababu za kukosa hedhi aina ya upili.

Zipo sababu mbalimbali zinazoweza kupelekea mwanamke mwenye sifa na vigezo vya kupata hedhi, kukosa hedhi. 

Baadhi ni za kurithi na nyingine si za kurithi ambazo hujitokeza katika maisha ya kawaida ya kila siku.

Baadhi ya sababu kuu za mwanamke kukosa hedhi ni kama zifuatzo;

#1: Matatizo katika shingo au mfuko wa uzazi.

Baadhi ya matatizo yanaweza kusabisha kuziba kwa njia ya shingo ya uzazi au kuharibiwa kwa mfuko wa uzazi na kusababisha damu kuvujia ndani badala ya kutoka nje.

Maradhi yanayoweza kushambulia shingo na mfuko wa uzazi ni pamoja na;

Asherman’s syndrome

Hili ni kundi la maradhi ambalo husababishwa na michubuko au kutoboka kwa kuta za ukuta wa tumbo la uzazi.
Tatizo hili husababishwa na matumizi ya vifaa vigumu kama vile vifaa vinavyotumika kufanyia uchunguzi wa ndani ya mfumo wa uzazi na pia husababishwa na maradhi sugu kama maradhi ya uvimbe na PID.

Tatizo hili hupelekea damu kuvujia ndani na kushindwa kutoka nje, hivyo mwanamke anashindwa kuiona damu. Atizo hili ni hatari na linahitaji dharula ya kitabibu.

Kuziba kwa shingo ya uzazi:

Kuziba au kupungua kwa kipenyo cha shingo ya uzazi ni moja ya chanzo kikubwa cha mwanamke kukosa hedhi.

Katika hali hii damu inashindwa kupenya katika kiwango ambacho mwanamke anaweza kutambua kama yuko katika siku zake za kutokwa damu.

Hali hii pia husababisha damu kutuama katika kiwambo cha kuta za shingo ya uzazi na kupelekea maumivu makali ya chini ya kitovu.

Wakati mwingine mwanamke hupata maumivu ya hedhi lakini haoni damu hii ni moja ya sababu.

#2: Hitilafu katika tezi ya Hypothalamasi.

Hii ni tezi mama ambayo huthibiti utengenezwaji wa homoni zote mwilini. Tezi hii huzalisha homoni maalumu ya GnRH ambayo huthibiti utengenezwaji wa homoni za uzazi za oestrojen, FSH na LH.

Uzalishwaji wa homoni ya GnRH kutoka katika Hypothalamasi huweza kuathiriwa na mambo mabalimbali kama vile;
  • Msongo wa mawazo.
  • Kupungua uzito.
  • Lishe duni.
  • Magonjwa sugu na ya muda mrefu.
  • Mazoezi makali.
  • Kuacha matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango.
Asilimia zaidi ya 80 ya wanawake huanza kupata hedhi miezi 3 hadi 6 baada ya kuachana na matumizi ya vidonge vya kupanga uzazi. Hii inatokana na mabadiliko ya homoni ambayo mwili unaya.

#3: Mimba ya uongo.

Mimba ya uongo huongeza kiwango cha homoni ya prolactin na LH ambazo huzuia upevushwaji wa yai. Kama hakuna upevushwaji wa yai basi hakuna hedhi.

#4: Uvimbe na michubuko ya tezi ya Hypothalamasi.

Hii inapelekea kudhoofu kwa utengenezwaji wa homoni ya GnRH ambayo husababishwa kutengenezwa kwa homoni za LH na FSH. Homoni hizi ndio husaidia yai kupevuka.

#5: Matatizo katika tezi ya pituitary.

Tezi hii hutengeneza homoni zaidi ya 7, athari katika tezi hii inaweza kusababisha matatizo mbalimbali ya mwili mbali na yale ya uzazi pekee. 

Tezi hii hueweza kushambuliwa au kuathiriwa na matatizo yafuatayo.
  • Uvimbe ambao unaweza kuwa wa kawaida au saratani.
  • Tezi iliyoundwa na seli dhaifu.
  • Tatizo hili linajulikana kama Sheehan’s syndrome.
  • Tatizo lijulikanalo kama Empty sella syndrome.
Matatizo haya yote katika tezi ya pituitary yanapelekea uzalishwaji mdogo wa homoni za LH na FSH ambazo husaidia kupevusha yai. 

Ikiwa yai halijapevuka basi mwanamke hawezi kuona wala kupata hedhi.

#6: Kushindwa kupevuka kwa yai.

Kushindwa kupevuka kwa yai kunaashiria matatizo katika namna mbili, kwanza ni kutokuwapo kwa homoni za upevushaji LH na FSH,  pili ni kuwepo kwa matatizo katika ovari (mfuko wa mayai).

Matatizo haya ya yai kutopevuka huweza kusababishwa na mambo yafuatayo;
  • Kuharibiwa au uvimbe katika seli za ovari na tezi za adrenali, hii ni sababu kuu.
  • Matumizi ya dawa.
  • Matumizi ya dawa kama vile kundi la dawa la phenothiazides ambazo huongeza uzalishwaji wa prolactin. Dawa za shinikizo la damu kama spironolactone na dawa za uzazi wa mpango na matibabu ya mionzi.
  • Kunyonyesha kwa sababu mwili huzalisha prolactin kwa wingi kwa ajili ya maziwa.
  • Matatizo katika tezi ya thyroid ambayo hupelekea utengenezwaji wa oestrojeni kupita kiasi.
  • Kuwahi kushindwa kufanya kazi kwa ovari kabla ya kufikia hatua ya menopause.
Menopause ni hatua ya kibaolojia ambapo ovari za mwanamke hupoteza uwezo wa kutoa mayai, kwa kaida hatua hii hujitokeza kati ya miaka 45 hadi 50. Lakini kwa baadhi ya wanawake huweza kuwahi zaidi hadi miaka 30 au 40.

#7: Tatizo la Cushing’s syndrome.

Katika tatizo hili kunakuwa na uzalishwaji mkubwa wa homoni za corticosteroids au matumizi makubwa ya kundi hili la dawa.

#8: Tatizo la ukuaji wa tezi ya adrenal kupita kawaida.

Ukuaji huu unapelekea uzalishwaji wa homoni za uzazi za mwanamke kuwa mkubwa na kuathiri upevushwaji wa yai.

Jinsi ya kutambua sababu za kukosa hedhi kwa wanawake.

Historia ya mgonjwa.

Kuna mambo ya kuzingatia ili kutambua ikiwa kuna tatizo la kibaolijia ambalo linasababisha kutopata hedhi. 

Vitu vya kuzingatia ni pamoja na;
  • muda ambao mwanamke amebalehe, 
  • muda ambao matiti yaliota, 
  • umri ambao nywele za sehemu za siri zilianza kuota 
  • vilevile ni kwa muda gani tatizo lipo.
  • historia ya lishe kwa mgonjwa, 
  • mabadiliko ya uzito wa mwili, 
  • matumizi ya njia za uzazi wa mpango, 
  • matatizo ya msongo wa mawazo na 
  • historia ya mwanamke kujihusisha na mazoezi au michezo ya kukimbia au mieleka.
  • uwepo wa chunusi na mapunye katika ngozi na 
  • mabadiliko ya sauti
Mambo yote haya ni vyema kuyafahamu ikiwa yamewahi kutokea au huwa yanatokea kwa mwanamke ambaye hukosa hedhi; kwa sababu ni ishara ya uwepo wa uvimbe katika tezi za androgen na ovari.

Ni lazima tathmini juu ya uwepo wa mimba kufanyika kwa kina kwa kuangalia dalili mbalimbali kama vile  
  • kutapika, 
  • matiti kuvimba, 
  • uchovu, 
  • kichefuchefu na 
  • maumivu chini ya kitovu. 
Pia ni muhimu kufanya vipimo vya mimba ili kubaini ikiwa tatizo limesababishwa na ujauzito.

Uchunguzi wa nje wa mwili.

Uchunguzi wa kina wa mwili unapaswa kuzingatiwa. Baadhi ya vitu muhimu kama uzito wa mwanamke, urefu lazima vijulikane ili kutathmini ikiwa kiwango cha mafuta mwilini ni chanzo cha tatizo.

Vilevile vile dalili za uwepo wa magonjwa ya moyo na kiwango cha mapigo ya moyo inapaswa kuchunguzwa. 

 Shinikizo la damu kuwa chini na mapigo ya moyo kuwa chini ya mara 50 kwa dakika ni ishara ya uwepo wa tatizo la kushindwa kufanya kazi kwa tezi za thyroid na adrenali.

Pia shinikizo la damu la juu na mapigo ya moyo ya zaidi ya mara 75 kwa dakika ni ishara ya uwepo wa tatizo la cushing syndrome na uzito mkubwa ambavyo huathiri hedhi.

Uchunguzi wa ndani wa mwili.

Matumizi ya vifaa maalumu kama ultrasound na kamera zinaweza kutumika kugundua matatizo ya uvimbe katika mfumo wa uzazi.

Vilevile vipimo vya damu kuchungua kiwango cha homoni na afya ya tezi mbalimbali Pamoja na uwepo wa magonjwa hatarishi kama PID.

Jinsi ya kutibu tatizo la kukosa hedhi kwa wanawake.

1: Kubadili namna ya kuishi.

Ikiwa tatizo limegundulika kusababishwa na lishe duni, uzito mdogo, msongo wa mawazo na mazoezi makali basi kurekebisha mienendo katika mambo haya ndio tiba pekee.

Mgonjwa napaswa kuzingatia lishe bora, kupumzika, kupunguza mazoezi makali na kuhakikisha anrudisha uzito kwa kuzingatia mpango sahihi wa lishe.

2: Matumizi ya dawa mbalimbali.

Hasa ikiwa tatizo linatokana na kupungua kwa homoni kama vile oestrogen. 

Kwa wanawake hawa matumizi ya dawa kama estradiol na norethindrone yanaweza kuwa na msaada kwa vile huongeza ujazo wa mifupa na kupelekea mwili kuzalisha homoni za oestrogen.

Lakini pia matumizi ya moja kwa moja ya dawa za homoni ya oestrogen ni msaada mkubwa kwa wanake hawa.

Baadhi ya virutubisho kama vile vitamin D na Calcium hushauriwa kutumika zaidi kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa mifupa na kuimarisha uzito wa wanawake hawa.

3: Tiba asili ya kukosa hedhi.

Baadhi ya mitishamba ina uwezo mkubwa wa kusaidia kuleta mlinganyo wa homoni na kutibu baadhi ya maradhi ikiwemo uvimbe na saratani ni pamoja na;
  • Vitex agnus-castus (chaste tree au chesterberry)
  • Paeonia lactiflora(peony), 
  • Trigonella ffoenum-graecum(fenugreek), 
  • Cinnamommum verum (mdalasini), 
  • Foeniculum vulgare(Feneli ya kawaida)
  • Cesamum indicum (ufuta), 
  • Mentha longifolia(wild mint), 
  • Allium cepa(kitunguu maji), 
  • Urtica dioica(Common Neettle), 
  • Pimpinella anisum(anise) na 
  • Nigella sativa(black cumin).
Hizi ni baadhi ya mitishamba ambayo imethibitishwa kutibu tatizo la kukosa hedhi kwa wanawake.

Hitimisho

Tatizo hili la kukosa hedhi husababishwa na mambo mengi hakuna njia moja ya kutibu. Jambo la msingi ni kufahamu tatizo lako limesababishwa na nini na kuchagua njia sahihi ya kutibu tatizo lako.

Usipuuzie tatizo hili la kukosa hedhi kwa sababu, ikiwa mwanamke hapati hedhi basi hawezi kushika ujauzito.  
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url