Dalili za shambulizi la moyo na nini cha kufanya tatizo likitokea.

Shambulizi la moyo ni tatizo linalotokea kwenye moyo ambapo mishipa ya damu katika moyo kushindwa kupitisha damu.

Tatizo hili linapelekea sehemu ya misuli ya moyo kukosa damu ya kutosha na moyo kukosa hewa ya oksijeni.

Kushindwa kufikiwa kwa damu na oksijeni katika misuli ya moyo kunapelekea shughuli nyingi zinazofanywa na misuli hii kusimama.

Moja ya madhara ya damu na hewa ya oksijeni kushindwa kufika katika moyo kwa kiwango kinachotakiwa ni kusimama kwa shughuli za moyo hivyo na kusababisha matatizo mengi ya kiafya na hata kifo.

Sayansi ya moyo wa binadamu na mzunguko wa damu.

Ukuta wa moyo wa binadamu umeundwa kwa tishu za misuli zenye uwezo wa kusinyaa na kutanuka. Vilevile moyo una mishipa ya damu ambayo husambaza damu katika moyo wenyewe.

Mishipa hii huunda mfumo wa mzunguko wa damu wa ndani ya moyo.

Moyo una vyumba vya wazi vinne, 2 upande wa kushoto na 2 upande wa kulia.

Moyo pia umeunganishwa na mishipa mbalimbali ya damu ambayo hutoa na kuingiza damu katika moyo.

Mishipa hii ni pamoja na aorta, vena cava na mishipa inayotoa na kuingiza damu katika mapafu.

Aorta ndio mshipa mkubwa unaotoa damu safi kutoka katika moyo kuelekea sehemu nyingine za mwili.

Moja ya matawi ya mshipa huu wa aorta husambaza damu katika moyo. Damu inayopita katika mshipa wa aorta imebeba hewa safi ya oksijeni ambayo ina kazi nyingi na muhimu katika seli.

Moja ya kazi za oksijeni katika seli ni kuunguza chakula ili kujipatia nishati ambayo inazifanya seli hizi ziendelee kufanya shughuli mbalimbali za mwili.

Bila hewa hii ya oksijeni hakuna seli itakayoweza kuhimili utengenezwaji wa nishati ya kutosha kwa muda mrefu na kuufanya moyo kuendelea kufanya katika ufanisi wake.

Shambulizi la moyo linatokeaje?

Kama ilivyoainishwa hapo awali kuwa shambulio la moyo ni pale sehemu fulani ya moyo inakosa kufikiwa na damu, damu ambayo imebeba dutu muhimu ikiwemo oksijeni na chakula.

Kushindwa kufikiwa na damu katika baadhi ya sehemu za moyo kunafanya seli za maeneo hayo kufa na kutengeneza kovu.

Sehemu ya moyo ambayo imetengeneza kovu inapoteza uwezo wa kufanya kazi ingawa sehemu nyingine ambazo hazijaathiriwa zitaendelea na utendaji kazi kama kawida.

Kwa kuwa tayari kiwango cha seli zinazoshughulika katika moyo zimepungua hivyo basi hata utendaji kazi wa moyo utadhoofu.

Ikiwa sehemu zitakazoathiriwa ni zile pande za chini za moyo, pande ambazo ndio hufanya kazi kubwa ya kusukuma damu jambo hili hupelekea moyo kusimama na hatimaye kifo.

Kumbuka kufa kwa seli za sehemu fulani ya moyo kunaweza kuambukiza sehemu jirani na hatimaye tatito kuwa kubwa kiasi cha kuhatarisha muhai.

Sababu za shambulizi la moyo

Sababu #1: Moyo kufikiwa na kiwango kidogo cha damu. 

Tatizo hili kitaalamu linaitwa Angina na hutafsiriwa kama hali ya mishipa ya damu katika moyo kushindwa kubeba damu iliyo na oksijeni inayokidhi mahitaji ya seli za moyo.

Ikiwa tatizo hili hujirudia mara kwa mara linaweza kupelekea seli za moyo kufa na hatimaye shambulizi la moyo kutokea.

Sababu #2: Kuwa na kiwango kikubwa cha rehemu au mafuta mwilini.

Rehemu inapozidi mwilini huweza kusababisha madhara mengi ya kiafya.

Moja ya madhara ya rehemu ni kutengeneza bonge la mafuta ambalo linaweza kuziba mishipa ya damu na kuzuia damu kufika upande wa pili wa mshipa wa damu.

Mishipa inyosambaza damu katika moyo hushambuliwa zaidi na rehemu kwa sababu ni mishipa miembamba mno.

Sababu #3: Matatizo ya kisukari.

Watu wenye matatizo ya kisukari ni moja ya kundi la watu ambao hushambuliwa zaidi na shambulizi la moyo.

Moja ya sababu ni kwamba watu miili yao huwa na uwezo mdogo wa kuchakata wanga.

Hali hii hupelekea kiasi kikubwa cha wanga ambacho huhifadhiwa kama mafuta mwilini.

Vilevile kundi hili huwa na kiwango kikubwa cha sukari ambayo huongeza shinikizo la damu ambalo huweza sababisha mishipa ya damu kupasuka.

Sababu #4: Matumizi ya vyakula vyenye mafuta.

Mafuta ya wanyama yana kiwango kikubwa cha rehemu. Rehemu husababisha kutengenezwa kwa mabonge ya mafuta ambayo yanaweza kuziba mishipa ya damu. 

Sababu #5: Matatizo ya shinikizo la damu.

Watu wenye shinikizo la damu la kupanda wako katika hatari zaidi ya kupata shambulizi la moyo kwa kuwa shinikizo la damu huaribu mishipa mbalimbali ya damu ikiwemo ya moyo.Uzito mkubwa na 

Sababu #6: Tatizo la kitambi (Fetma).

Watu hawa huwa katika hatari zaidi kwa sababu kitambi ni chakula cha ziada ambacho mwili umeshindwa kukitumia kwa vile hakikuhitajika.

Mwili hukihifadhi chakula hiki katika namna ya mafuta katika sehemu mbalimbali ikiwemo katika moyo. Mafuta haya huweza kuziba mishipa ya damu mwilini. 

Sababu #7: Uzembe na uvivu.

Watu ambao hawafanyi mazoezi au kujihusisha na shughuli mbalimbali za kimwili wako katika hatari pia kwa kuwa kwa kutokufanya hivyo wanakaribisha mlundikano wa mafuta mwilini.

Sababu #8: Mitindo ya maisha isiyo rafiki.

Baadhi ya tabia kama vile kama ulevi, uvutaji, msongo wa mawazo huweza sababisha shambulizi la moyo. 

Sababu #9: Watu wenye ugonjwa wa UKIMWI.

Watu wenye magojwa ya UKIMWI, kifua kikuu na watu walio na historia ya kuugua magojwa ya moyo pamoja na watu wenye umri mkubwa wa kuanzia miaka 55 hawa wako katika hatari zaidi.

Dalili za shambulizi la moyo.

  • Msukumo wa damu huongezeka ikiambatana na mwili kukaza.
  • Maumivu katika maeneo ya kifua yanayoweza kutambaa mpaka shingoni, katika taya za midomo na mgongoni.
  • Kupata kizunguzungu cha ghafla.Kifua kukaza na kuhisi kizito kupita kawaida.
  • Kupumua kwa shida.
  • Kupata kichefuchefu cha ghafla na kuhisi kiungulia au maumivu upande wa chini wat umbo.
  • Kupata kizunguzungu cha ghafla.
Dalili hizi huweza kudumu kwa muda tofauti, dakika, masaa hadi siku kutegemea na hali ya ukubwa wa tatizo.

Tiba ya shambulizi la moyo.

Shambulizi la moyo ni hatari kwa Maisha, takwimu zinaonyesha watu wengi ambao hupata shambulizi la moyo hupoteza maisha.

Sababu kuu ya kwanini tatizo husababisha vifo ni kwamba tatizo hili hutokea ghafla, na ni vigumu kwa mtu kufahamu kwamba yuko kwenye hatari ya kupata shambulizi la moyo.

Ili kujiweka katika mazingira salama ni vyema kufahamu mambo hatarisha yanayoweza kukusababishia tatizo hili.

Vilevile kuwa tayari kutoa taarifa katika vituo vya msaada mara tu uonapo dalili hizi.

Kulingana na ugumu na ukubwa wa tatizo hili si rahisi kumpa huduma ya kwanza mtu aliyepatwa na shambulizi la moyo.

Kwa kuwa namna ya kutibu tatizo hili ni za kitaalamu zaidi na zinahitaji mitambo maalumu ya kumsaidia mgonjwa.

Huduma ya kwanza pekee ambayo inaweza kutolewa nje ya kituo cha afya cha dharula ni kusaidia damu kusafiri kwa urahisi na kumpatia mgonjwa hewa ya kutosha ya Oksijeni.

Kwa mana hiyo ikiwa umekutana na mgonjwa aliyepata tatizo hili fanya yafuatayo wakati tayari umeshaomba msaada kutoka kituo cha afya, fanya yafuatayo:
  • Toa nguo zote za mgonjwa hasa zile za kubana ili kusaidia damu kusafiri kwa urahisi.
  • Hakikisha mgonjwa anapata hewa ya kutosha ya oksijeni, kwa kumuweka eneo la wazi lenye hewa ya kutosha.
Ikiwa mapigo ya moyo ya mgonjwa yamesimama fanya yafuatayo;
  • Mlaze chali mgonjwa sehemu ya wazi huku ukimvua nguo zote.
  • Funga mikono yako vizuri, kisha kandamiza kifua cha mgonjwa kwa kutumia viganja vya mikono yako kwa nguvu na kasi ya mikandamizo 100-120 kwa dakika.
  • Rudia zoezi hili mpaka pale mgonjwa atakaporudisha pumzi yake au timu ya msaada itakapofika.
Katika kituo cha dharula tatizo linaweza kushughulikiwa kwa namna kadhaa kama ifuatavyo;
  • Mgonjwa atapewa dawa za kusaidia kuyeyusha damu iliyokuwa imeganda na kuzuia damu kupita au dawa ya kusaidia mishipa ya damu kuruhusu damu kupita kwa urahisi.
  • Watatumia njia za kitaalamu za kuruhusu damu kufika sehemu ya seli za moyo zilizoathiriwa. Njia hii huitaji mitambo maalumu na pengine upasuaji.
Baada ya mgonjwa kutengamaa. Njia salama ya kupambana na tatizo hili la shambulizi la moyo ni kuomba muongozo sahihi wa namna gani ya kuzuia tatizo hili lisijurudie.

Hitimisho

Shambulizi la moyo ni hatari kwa uhai. Takwimu zinaonyesha kuwa kupatiwa matibabu ndio njia pekee ya kurudisha uhai kwa muathirika.

Kuwa makini na afya yako na tambua kama ni kwa kiasi gani uko katika hatari ya kupata tatizo hili.

Hii itakusaidia pindi uonapo dalili za mapema za tatizo hili na kuweza kuwasiliana na wataalamu wa afya kwa msaada zaidi.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url