Tatizo la kuharisha, chanzo, dalili na tiba.

Tatizo la kuharisha ni moja ya matatizo ya kawaida sana katika jamii, na huwaathiri zaidi watu kutoka nchi zenye uchumi mdogo.

Tatizo hili ni miongoni mwa magonjwa hatari zaidi duniani na linatajwa kuwa tatizo linaloongoza kwa vifo vya watoto duniani kote.

Licha ya kuwa ni tishio la uhai, uhatari wa tatizo hili la kuharisha unategemea zaidi umri wa muathirka, kiwango cha muda litakaochukua na chanzo cha tatizo.

Matibabu ya tatizo la kuharisha yanaweza kuwa ya kawaida ama yakahitaji dharula ya kitabibu, inategemea zaidi na uhatari wake.

Tatizo la kuharisha

Tatizo la Kuharisha ni hali ya kupata haja kubwa au kutoa kinyesi laini kilichoambatana na kiasi kikubwa cha maji kupita kiasi kwa zaidi ya mara 3 kwa siku.

Katika hali ya kawaida tatizo la kuharisha huweza kupelekea kiasi cha hadi lita moja ya maji kupotea mwilini kwa siku.

Ikiwa upotevu wa maji utazidi kiasi cha lita 2 kwa siku basi mgonjwa anatakiwa kupata msaada wa dharula wa kitabibu.

Tatizo la kuharisha huweza kusababishwa na mambo mengi lakini sababu kuu huwa ni maambukizi ya vimelea mbalimbali vya magonjwa vya babteria, minyoo na virusi.

Mtu anaweza kupata vimelea hawa kwa njia mbalimbali, baadhi ni:
  • Matumizi ya maji machafu hasa yaliyotuama yenye vimelea vya magonjwa hasa vimelea vya salmonella.
  • Kugusana na majimaji kutoka kwa mtu aliyeathirika na vimelea husika.
  • Matumizi ya vyakula visivyoiva au kuoshwa vizuri ambavyo vimeathiriwa na vimelea hawa.

Sababu za kuharisha.

Kwa kawaida ufanisi wa mfumo wa chakula katika ufyonzaji maji ni zaidi ya 93%. Ufanisi huu hufikiwa ikiwa hakuna hitilafu yoyote kati ya zilizotajwa hapo juu.

Tatizo la kupoteza maji mengi mwiini kupitia kuharisha hutokea ikiwa kuna hitilafu zifuatazo:
  • Hitilafu ya ufyonzwaji wa maji kutoka tumboni na utumbo kuelekea seli za mwili, ama,
  • Kuvuja kwa maji kutoka katika seli za mwili kuingia katika tumbo na utumbo.
Hitilafu hizi hutokea ikiwa kuna mambo yafuatayo:

01: Matatizo ya ufyonzwaji wa Lactose.

Lactose ni aina ya wanga ambayo hupatikana zaidi kwenye maziwa. Aina hii ya wanga hutengenezwa kwa uwepo wa kichagizi cha enzyme za Lactase na hufyonzwa katika utumbo mwembamba.

Kushindwa kufyonzwa kwa chakula hiki ambako husababishwa na hitilafu katika seli za utumbo au kutokuwepo kwa kichagizi cha enzyme za Lactase.

Kunasababisha chakula hiki kutuama katika utumbo na kupelekea maji kutoka katika seli kukifuata chakula hiki kutokana na tofauti za kiosmotiki.

02: Uvimbe na maradhi ya kongosho.

Kongosho huzalisha vichagizi kadhaa vya enzyme ikiwemo vichagizi vinavyomeng’enya mafuta.

Kushindwa kumengenywa kwa mafuta kunaahiri ufyonzwaji wake hivyo kusababisha tofauti za kiosmotiki kati ya utumbo na seli za utumbo.

Tofauti hii ya kiosmotiki hupelekea maji kufuata mafuta kwa kutoka katika seli za mwili na kuingia katika utumbo kisha kutolewa kama kinyesi.

Vilevile maji ndani ya utumbo kushindwa kufyonzwa katika seli mbalimbali za mwili kupitia seli za utumbo.

03: Ajali katika seli za utumbo.

Ikiwa kutatokea majeraha katika seli za utumbo, utendaji kazi wa ufyonzaji wa maji wa seli hizi huathirika pia.

Kwa hivyo maji hushindwa kuingia katika seli hizi, vilevile husababisha maji kuvuja kutoka katika seli kuingia katika utumbo.

Mara nyingi maambukizi ya vimelea ndio chanzo kikubwa cha majeraha katika seli hizi.

Aina za tatizo la kuharisha

Tatizo la kuharisha limegawanywa katika aina kuu mbili kuzingatia na muda wa tatizo na dalili atakazoonyesha mgonjwa.

Aina hizo ni:

01: Tatizo la kuharisha la kawaida.

Kuharisha hugawanywa katika aina hii ikiwa litatokea na kuchukua wastani wa chini ya siku 14 huku sehemu kubwa ya kinyesi ikiwa ni maji.

Mara nyingi aina hii ya kuharisha husababishwa na maambukizi ya vimelea vya bakteria na virusi.

02: Tatizo sugu la kuharisha.

Tatizo hili huwekwa katika aina hii ikiwa litachukua zaidi ya siku 14 na mgonjwa hupoteza wastani wa zaidi ya lita 2 za maji kila siku na huweza kuambatana na damu.

Mara nyingi aina hii ya kuharisha husababishwa na hitilafu za kiutendaji mwilini na katika mfumo wa chakula.

Baadhi ya hitilafu hizo ni:
  • Matatizo ya kongosho.
  • Mwili kushindwa kumeng’enya mafuta na wanga.
  • Mwili kushindwa kuzalisha vichagizi mbalimbali vya enzyme.
  • Maradhi katika mfumo wa chakula.
  • Ajali katika seli za utumbo mwembamba.
  • Maambukizi ya vimelea vya magonjwa.

Maambukizi ya vimelea vya magonjwa.

Kuna idadi kubwa ya vimelea wa magonjwa, bakteria, minyoo na virusi ambao husababisha tatizo la kuharisha.

Bakteria wanaosababisha tatizo hili:
  • Aeromonas veronii.
  • C. jejuni na C. coli.
  • Escherichia coli.
  • Salmonella enterica.
  • Shigella dysenteriae, Shigella flexneri, Shigella boydii na Shigella sonnei.
  • Tropheryma whipplei.
  • Vibrio cholerae.
  • Yersinia enterocolitica na Yersinia pseudotuberculosis.
Virusi wanaosababisha tatizo hili ni:
  • Rotavirus
  • Norovirus.
  • Sapovirus.
  • Astrovirus.

Dalili za kuharisha.

Mgonjwa wa kuharisha anaweza kuonyesha dalili zifuatazo:
  • Maumivu ya tumbo.
  • Kichefuchefu.
  • Kutapika.
  • Homa.
  • Kinyesi chenye maji mengi, usaha au damu.
  • Kinyesi chenye rangi ya maziwa.
  • Maumivu ya puru.
  • Tumbo kuunguruma.
  • Kujamba.
  • Ngozi kusinyaa.
  • Kutoa mkojo kidogo.
  • Upungua uzito na kukonda.

Dawa ya kuharisha kuharisha.

Katika jitihada za kutibu tatizo la kuharisha, kujua chanzo ni nguzo muhimu ya kufanikisha tiba.

Ni vyema kufahamu ikiwa tatizo linasababishwa na maambukizi au hitilafu za kiutendaji.

Ikiwa chanzo ni maambukizi, aina ya kimelea ni muhimu kufahamika kwa kuwa vimelea wa magonjwa huthibitiwa kwa namna tofauti.

Dawa ya kuharisha ni kufanya mambo yafuatayo;
  • Kunywa juisi za matunda kwa wingi.
  • Kunywa chumvi/sukari tiba maalumu, maarufu kama ORS.
  • Kunywa maji mengi.
  • Sitisha matumizi ya vyakula vya ufumwele.
  • Tumia vyakula kama vile ndizi, ngano na mchele.
Vilevile ikiwa tatizo limesababishwa na bakteria matumizi ya dawa za antibiotiki hushauriwa.

Matumizi ya antibiotiki pia lazima yazingatie chanzo cha tatizo, ni aina gani ya bakteria.

Kwa sababu baadhi ya bakteria wameonyesha kuwa na usugu wa dawa kwa kiasi kikubwa mfano bakteria wa S. typhi wanaosababisha Homa ya matumbo (Typhoid).

Kwa bakteria wengineo, kundi la antibiotiki la fluoroquinolones ndio pendekezo namba moja, na inashauriwa kupewa mara moja tu kwa bakteria wote isipokuwa bakteria jamii ya Campylobacter na Shigella.

Kwa tatizo la kuharisha linalosababishwa na bakteria hawa wa Campylobacter na Shigella tiba hii ya antibiotiki huweza kutumika hadi siku tatu.

Ikiwa tatizo linasababishwa na bakteria wa E.Coli, matibabu yake yanapaswa kuwa maalumu kutokana na ugumu wa kumuangamiza bakteria huyu.

Kwa tatizo sugu la kuharisha ambalo huambatana na damu, usaha ama ute katika kinyesi. Matibabu yake yanapaswa kuwa maalumu.

Ni vizuri mtaalamu wa afya kutambua chanzo kisha kuandaa mpango mkakati muhimu wa matibabu ambao utaonekana unafaa zaidi.

Mbali na antibiotiki vilevile mgonjwa anaweza kupatiwa dawa maalumu za kuzuia ama kupunguza mjongeo wa mfumo mzima wa chakula kwa lengo la kuchelewesha na kuleta nafuu ya hali hii.

Njia za kuzuia na kujikinga na tatizo la kuharisha.

  • Zingatia usafi binafsi, wa vyakula na vinywaji.
  • Nawa mikono kabla na baada ya kula ama kushika chakula.
  • Chemsha maji ya kunywa.
  • Hakikisha vyakula vinaiva vizuri.
  • Kuwa makini unapoogelea hasa mabwawa ya kuogelea.
  • Tunza vyanzo vya maji.
  • Pata chanjo, kwa sasa ni chnjo ya kipindupindu pekee.
  • Tumia chumvi/sukari tiba maalumu, maarufu kama ORS, ikiwa una maradhi hatarishi.
  • Ishi kwa kuzingatia kanuni za afya ikiwa una maradhi hatarishi kama vile uvimbe katika kongosho na vidonda vya tumbo.

Hitimisho.

Fika kituo cha afya uonapo dalili zozote za kuharisha. Ufikapo kituo cha afya mtaalamu wa maabara anaweza kuhitaji kinyesi au damu, ni kawaida na ni kwa lengo zuri.

Tatito la kuharisha ni hatari kwa uhai, kupotea kwa madini joto ya Potasium na kupungua kwa maji mwilini ndio hasa hupelekea vifo.

Chukua tahadhali, hakikisha unajikinga kwa kufuata kanuni za afya na kujiepusha na vihatarishi vinavyoweza kukusababishia tatizo.

Hakikisha unatoa ushirikiano kwa manufaa ya afya yako.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url