Sababu kuu 17 za tatizo la nguvu za kiume

Hali ya uume kusimama ni kitendo tata ambacho kinahusisha hatua na matukio mengi. Kitendo hiki huanza kwa uwepo wa kiamshi cha ashki na kuhusisha mfumo wa neva, misuli na mabadiliko katika mishipa ya damu katika uume.

Jambo lolote ambalo linaweza kuingilia na kuvuruga hatua yoyote ya kuwezesha uume kusimama huweza kuwa sababu muhimu ya tatizo hili la upungufu wa nguvu za kiume.

Kwa kuzingatia hili, zipo sababu nyingi ambazo huweza kusababisha tatizo hili. 

Sababu hizi zimegawanywa katika makundi makuu mawili ambayo ni sababu za 
  • kisaikolojia na 
  • kibaolojia.

Sababu za kisaikolojia za upungufu wa nguvu za kiume.

Tatizo la upungufu wa nguvu za kiume huweza kutokea kutokana na sababu za kisaikolojia. Mambo mbalimbali hutokea katika Maisha kiasi cha kuacha majeraha katika fikra zetu.

Baadhi ya mambo yanaweza kuharibu akili kiasi cha kusababisha mwanaume kushindwa kushiriki tendo la ndoa na mwenzi wake. 

Baadhi ya mambo hayo ni Pamoja na;

01: Unyanyaswaji wa kingono kwa wanaume.

Baadhi ya wanaume hukutana na changamoto kwa wenza wao kiasi cha kupoteza hamu na ashki kwa wanawake. 

Mfano mwanamke kumsababishia ajali ya uume mwanaume (kuvunjika au kupasuka kwa uume) ambako husababishwa na mwanamke ama makusudi au bahati mbaya.

02: Matatizo ya kimaisha.

Changamoto mbalimbali anazopitia mwanaume zinaweza kumsababishia kupoteza hamu ya kujamiana na kushindwa kusimamisha uume. 

Mfano sonona (msongo wa mawazo), hali mbaya ya kiuchumi, matatizo ya kazi na ajira na mengineyo.

03: Elimu ya mahusiano.

Elimu mbalimbali za mahusiano ambazo mwanaume anazipata zinaweza kuwa chanzo cha yeye kupoteza hamu ya kujamiana na kushindwa kujiamini. 

Mfano kutazama video za ngono, tatizo linakuja pale unapotaka kufanya yale uliyoyashuhudia katika video hizo ambazo asilimia kubwa hazina uhalisia.

04: Sababu za kiimani na kitamaduni.

Kwa baadhi ya Imani na tamaduni zinaweza kuwa chanzo cha mwanaume kupoteza hamu ya kujamiana na kushindwa kupata ashki kabisa.

Mfano aina Fulani za maumbile kwa baadhi ya wanawake wa jamii fulani zinaweza zisimvutie mwanaume, mikao fulani wakati wa kujamiana inaweza kuwa ni makatazo ya kimila au kiimani kwa mwanamke lakini mwanaume akahitaji.

05: Kukosa uaminifu (kuchepuka).

Kwa mwanaume anayependa kuchepuka inaweza kuwa sababu ya yeye kupata tatizo hili hasa anapokutana na mwanamke ambaye hamvutii maumbile yake ya ndani.

Vilevile mwanume anaweza kukutana na mwanamke mwenye mvuto wa hali ya juu kiasi kwamba anapokuwa na mwenza wake au mke wake anapoteza hisia kabisa.

06: Upendo uliokithiri.

Upendo uliokithiri wa mwanaume kwa mwenza au mke wake inaweza sababisha tatizo la kukosa nguvu za kiume hasa inapotoka mwanaume anampoteza mwanamke wake ama kwa kuachana au kifo.

Hii inatokana na mwanaume kuamini ya kwamba hakuna mwanamke anayeweza kumpa alichokuwa anakipata.

07: Wasiwasi na nia kuu.

Kuwa na wasiwasi ama kuweka nia kwa mwanamke kunasababisha mwanaume kushindwa kusimamisha uume. 

Sababu kuu ni kwamba katika hali hii mwili unakuwa katika uthibiti wa mfumo wa neva wa sympathetic ambao husababisha kukaza kwa misuli na kuzuia damu kufika katika uume.

08: Aibu na mawasiliano mabovu kati ya wapenzi.

Baadhi ya wapenzi huoneana aibu na kushindwa kuwasiliana kimahaba kiasi cha kuamshiana ashki. Vilevile kushindwa kuambiana ni kwa namna gani kila mmoja anafurahia tendo kwa ujumla.

Sababu za kibaolojia za upungufu wa Nguvu za kiume

Yapo mambo mbalimbali ya kibaolojia ambayo husababisha tatizo la upungufu wa nguvu za kiume. Mambo hayo ni kama yafuatayo;

01: Maradhi ya mfumo wa mzunguko wa damu.

Hii ni sababu kuu ya kibaolojia inayosababisha tatizo la upungufu wa nguvu za kiume. 

Moja ya tatizo kuu la mfumo huu ambalo huathiri zaidi nguvu za kiume ni atherosclerosis, kuziba kwa mishipa ya damu kutokana na uwepo wa mafuta (rehemu) katika damu.

Tatizo hili la atherosclerosis husababisha mafuta kuziba mishipa ya damu katika uume na kuzuia damu kufika katika uume.

Tatizo hili la atherosclerosis huchagizwa zaidi na;
  • matatizo ya kisukari, 
  • kiwango kikubwa cha mafuta na 
  • shinikizo la damu.

02: Maradhi ya kisukari na nguvu za kiume.

Wanaume wenye kisukari huwa katika hatari mara 3 zaidi ya kupata tatizo la upungufu wa kinga mwilini ukilinganisha na wanaume ambao hawana kisukari.

Sababu kubwa ni kuharibiwa kwa neva kunakosababishwa na kisukari. Vilevile kuharibiwa kwa kuta za seli ambazo huzarisha kemikali ya Nitric oxide.

04: Kiwango kikubwa cha rehemu (mafuta) mwilini.

Kiwango kikubwa cha mafuta mwilini hasa yale ya Wanyama yenye rehemu ni moja ya sababu kuu za tatizo hili.

Rehemu nyingi kupita kawaida kunasababisha kutengenezwa kwa kemikali ya low-density lipoprotein (LDL ). Kemikali hii huweza kuziba mishipa ya damu.

05: Umri mkubwa.

Umri kubwa unachangia tatizo hili kwa vile kadri mwanaume anavyozeeka ndivyo anashambuliwa na maradhi ya mzunguko wa damu na kisukari kwa urahisi zaidi.

Vilevile kuzeeka kunaambatana na kupoteza au kupungua kwa misuli. Misuli inapopungua au kupotea mbadala wake ni mifupa laini ambayo haina msaada katika uume kusimama.

Mengineyo ni pamoja na kupungua kwa homoni ya testosterone ambayo husaidia ashki na kupungua kwa neva katika uume.

06: Matatizo katika mfumo wa tezi (homoni).

Matatizo katika mfumo wa tezi, hasa tezi za uzazi yanaweza kuwa chanzo cha tatizo. 

Magonjwa kama uvimbe wa korodani, kubonyea kwa korodani, mionzi katika mfumo wa uzazi na magonjwa ya kuzaliwa kama Klinefelter’s syndrome.

Pia tatizo la kutengenezwa kwa homoni ya prolactin kupita kawaida, tatizo ambalo husababishwa na uvimbe katika tezi ya pituitari. Tatizo hili huambatana na mwanaume kuota matiti.

07: Ajali katika via vya uzai.

Ajali mbalimbali katika maeneo ya mfumo wa uzazi zinaweza kusababisha tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.

Baadhi ya ajali hizo ni Pamoja na kupasuka kwa uume, kuharibika kwa pelvic plexus, kuharibiwa na mionzi na kufikiwa, kemikali sumu kama madini ya zebaki Pamoja na upasuaji katika maeneo ya mfumo wa uzazi.

08: Matumizi ya dawa.

Baadhi ya dawa huathiri mchakato mzima wa uume kusimama. Dawa hizo hizo huweza kusababisha matatizo ya muda mfupi au muda mrefu kutegemea na aina ya dawa.

Baadhi ya dawa zinazoweza kusababisha upungufu wa nguvu za kiume ni pamoja na dawa za kutibu shinikizo la damu mfano furosemide, methyldopa na clonidine, dawa za kutibu magonjwa ya akili kama vile Phenothiazines na dawa za kutibu saratani.

Dawa nyingine ni pamoja na Digoxin, Cimetidine, Metoclopramide, Phenytoin, Carbamazepine. Vilevile dawa za kutibu UKIMWI, pombe, bangi na dawa za kulevya kama cocaine.

09: Maradhi katika via vya uzazi.

Magonjwa mbalimbali yanaweza kusababisha upungufu wa nguvu za kiume kwa wanaume. Baadhi ya magonjwa hayo ni gono, UKIMWI, UTI na maradhi mengine ya mfumo wa mkojo.

Hitimisho

Upungufu wa nguvu za kiume ni tatizo linaloathiri wanaume wengi kutokana na sababu mbalimbali kama ilivyoainishwa katika makala hii.

Jambo muhimu zaidi katika kutibu na kupambana na tatizo la nguvu za kiume ni kufahamu chanzo na sababu.

Zipo dawa za aina tofauti za kutibu nguvu za kiume, kuna vidonge, sindano, upasuaji na tiba asili kulingana na sababu ya tatizo lako na kiwango ambacho tatizo limefikia.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url