Je, Unafahamu nywele yako imeundwa na nini?

Miili yetu imefunikwa na aina mbalimbali za nywele. Kati ya aina hizi, nywele za kichwani ni moja ya aina muhimu ya nywele katika miili yetu kwa kuwa mbali na kuwa na faida ya kulinda kichwa lakin pia hutumiwa zaidi kama sehemu ya urembo na kuongeza mvuto.

Ukiachana na nywele kutumika kama sehemu ya urembo na kuongeza  mvuto, nywele katika mwili wa mwanadamu zina faida kibao ambazo pengine hujawahi kuzifikiria.

Baadhi ya faida za nywele mwilini ni pamoja na;

  • Kutukinga dhidi ya mionzi hatari ya jua.
  • Kutukinga dhidi ya vumbi na wadudu, mfano kope.
  • Kusaidia mwili kuhisi miguso na hatari katika ngozi.
  • Kuzuia maji kupotea mwilini.
  • Nywele husaidia kufunika sehemu mbalimbali za mwili hivyo kutusitili maeneo muhimu kama vile nyeti zetu.

Katika makala hii tutaagazia sayansi ya nywele katika nyanja ya urembo na mwonekano hususa ni nywele za kichwani, kidevuni (ndevu), na machoni (kope na nyusi).

Asili na aina za nywele.

Je, unafahamu ya kuwa sehemu zote za mwili wako zimefunikwa na mashina ya nywele isipokuwa viganja, nyayo na midomo pekee.

Mashina haya ya nywele huanza kuota wiki ya 22 ya ukuaji wako ukiwa tumboni, yaani mwezi wa 5.

Mpaka kufikia muda wa kuzaliwa takribani jumla ya mashina ya nywele millioni 5 yanakuwa tayari yametengenezwa mwili mzima.

Kutoka katika idadi hii kichwa hupata mgawo wa mashina ya nywele kati ya 100,000 hadi 150,000. Idadi hii haiongezeki badala yake hupungua kadri umri unavyo ongezeka.

Kwa kawaida baada ya kuzaliwa nywele zote za mwili wako huwa na kimo sawa. Nywele huanza kutofautiana kimo kutokana na sababu mbalimbali za kimazingira, lishe au kibaolojia.

Moja ya sababu kuu na ya kawaida ni balehe. Baada ya kufikia umri wa balehe mwili huzalisha homoni za androjeni (homoni za uzazi) ambazo ndio chanzo kikuu kinachopelekea baadhi ya maeneo kuota nywele ndefu kuliko maeneo mengine.

Mbali na homoni hizi, pia dutu kama vipokezi vya mwili vya vitamini D, vipokezi vya mwili vya homoni ya thailoidi na dutu nyinginezo.

Kwa pamoja husababisha hali hii ya baadhi ya maeneo kuota nywele ndefu zaidi ya maeneo mengine.

Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na  

  • kidevuni, 
  • sehemu za siri(uume au ukeni), 
  • matakoni, 
  • makwapani, 
  • kifuani, 
  • tumboni, 
  • miguuni, 
  • masikioni na kichwani.

Kuna baadhi ya watu huzaliwa bila nywele au huzaliwa na mapungufu ambayo huathiri ukuaji wa kawaida wa nywele.

Katika hali hii chanzo kikubwa cha tatizo hili hutajwa kuwa ni mapungufu katika chembe za urithi.

Mbali na chembe za urithi, pia kuna dutu kadhaa ambazo kwa pamoja zinafanikisha ukuaji sahihi wa nywele.

Tatizo lolote katika chembe ya urithi au dutu nyinginezo linaweza kusababisha mapungufu kadhaa kama vile

  • Upara.
  • Nywele nyekundu/nyeupe.
  • Mvi nk.

Muundo wa nywele na aina za nywele.

Kitaalamu nywele imegawanyika katika sehemu kuu mbili;

  • Sehemu ya ndani ya nywele.
  • Pili ni Sehemu ya nje ya nywele.

Sehemu ya ndani ya nywele.

Hii ni sehemu ya nywele isiyoonekana ambayo ipo ndani ya ngozi (shina la nywele), kitaalamu sehemu hii huitwa papilla.

Sehemu hii ya nywele imeundwa na seli hai tofauti ambazo hufanya kazi mbalimbali katika sehemu hii ya nywele ikiwemo kutengeneza nywele na rangi ya nywele.

Baadhi ya seli katika sehemu hii ya ndani ya nywele ni seli zinazounda mfumo wa fahamu (seli za neva), seli za melanosaiti na seli za damu.

Vilevile seli zinazounda mishipa ya damu na seli zinazounda tezi ya kutengeneza ute wa sebamu.

Baadhi ya kazi za ziada zinazofanywa na seli hizi ni pamoja na;

  • Seli za damu husaidia ufikishwaji wa hewa na viutubisho kwa ajili ya ukuaji wa nywele.
  • Kusaidia kutengeneza ute wa sebamu kama ulinzi wa ngozi na nywele.
  • Kusaidia upokeaji na usafirishaji wa taarifa za miguso na hatari za kimazingira kupitia ngozi au nywele.
  • Husaidia hatua nzima ya utoaji takamwili kupitia ngozi.
  • Baadhi ya seli husaidia kutengenezwa dutu rangi za melanini.

Ni katika sehemu hii ambapo seli hai hutengenezwa na kupitia mchakato tata ambao hubadili seli hai kuwa mfu na seli hiyo katika hali ya ufu hujitokeza nje kama nywele.

Sehemu ya nje ya nywele.

Hii ni sehemu ya nywele iliyojitokeza kwa nje na tunaweza kuiona kwa macho na kuishika. Sehemu hii imeundwa na seli zilizokufa.

Hii ni sehemu muhimu zaidi ya nywele kwa vile inatofautiana kwa kiasi kikubwa kati ya mtu na mtu kutokana na tofauti za muundo na aina ya viambata ndani ya sehemu hii ya nywele.

Urefu wa nywele, rangi ya nywele, uimara wa nywele na muonekano vyote hivi huathiriwa na hutegemea zaidi muundo na nini kimeunda sehemu hii ya nywele.

Muundo wa sehemu ya nje ya nywele.

Sehemu hii imeundwa na matabaka matatu au mawili ya katika muundo wa duara. Matabaka hayo ni kama ifuatavyo;

  • Cuticle (Tabaka la nje).
  • Cortex (Tabaka la kati).
  • Medulla (Tabaka la ndani).

Muhimu zaidi ni tabaka la kati ambalo limeundwa na protini muhimu ya keratini na dutu za rangi za melanini.

Mbali na dutu za keratini na melanini, sehemu ya nje ya nywele pia imeundwa na mafuta pamoja na madini joto kadhaa.

Kutokana na kuundwa na seli zilizokufa. Nywele ni sehemu pekee ya mwili ambayo madini joto hatari kama zebaki na shaba nyekundu, pamoja na kemikali kadhaa hatari (sumu) katika mwili hulundikana na kukaa katika nywele kwa muda mrefu.

Kwa maana nyingine ni kwamba ni nywele pekee katika mwili wa binadamu ndio ambayo inaweza kukaa muda mrefu (maelfu ya miaka) bila kupoteza uhalisia wake au kuoza.

Asili hii ya nywele inafanya sehemu hii ya mwili kuwa chaguo namba moja la uchunguzi wa kisayansi dhidi ya uhalifu, hasa uhalifu wa kutumia sumu.

Dutu za keratini na uimara wa aina za nywele.

Keratini ni aina ya protini ambayo hutengenezwa na mwili na kuhifadhiwa katika maeneo mbalimbali ya mwili ikiwemo kucha, nywele na macho.

Protini hii imeundwa na elementi za hydrojeni, nitrogen, oksijeni na salfa. Kiwango cha elementi za salfa ndio hasa huamua ni kwa kiwango gani nywele zako ziwe imara.

Ikiwa nywele itaundwa na kiwango kikubwa cha protini hii ya keratini iliyo na kiasi kikubwa cha elementi za salfa basi nywele hizo hutafsiriwa kama nywele imara.

Kwa wastani nywele moja iliyo imara inaweza kuhimili uzito wa takribani 100gm.

Kwa maana nyingine ni kwamba ukikusanya nywele 10 za kichwani, kwa pamoja zinaweza kuhimili uzito wa kilogramu moja bila kuharibika.

Moja ya jambo linaloathiri kiwango cha protini ya keratini na uimara wa nywele ni unene wa matabaka ya sehemu ya nje ya nywele hususa ni tabaka la kati.

Unene wa tabaka hili la kati la sehemu ya nje ya nywele hutofautiana mtu na mtu. Yapo mambo mengi yanayoweza kuathiri unene wa tabaka hili, lakini kubwa ni utofauti katika chembe za urithi yaani vinasaba (RNA & DNA).

Ikiwa tabaka hili litakuwa nene ndivyo kiwango cha keratini huwa kikubwa, hivyo nywele nene hutajwa kuwa ndio nywele imara zaidi kuliko nyembamba.

Kutokana na kwamba kwa sehemu kubwa unene wa nywele unarekebishwa na vinasaba, ufuatao ni mchanganuo wa uimara wa nywele kulingana na asili na aina za vinasaba katika jamii mbalimbali.

Ni watu gani wenye nywele imara zaidi?

Utafiti wa kitaalamu unaonyesha nywele za watu wenye asili ya Afrika, bara la Asia na wahindi wekundu ndio jamii ya watu wenye nywele imara zaidi kuliko jamii yeyote.

Hii inatokana na kwamba nywele kutoka jamii hizi ndio nywele zilizo na unene mkubwa kuliko jamii yeyote.

Hivyo nywele hizi huhifadhi kiwango kikubwa cha keratini kuliko nywele za jamii yeyote.

Wakati nywele za kiafrika zikitajwa kuwa ndio zenye mshonano mkubwa wa elementi ya salfa, jambo linalozifanya kuwa kinara kati ya nywele imara.

Wakati nywele kutoka jamii za kiafrika kitajwa kama nywele imara zaidi, zikifuatiwa na wahindi, waarabu kisha wachina, hali ni tofauti kwa nywele za jamii ya watu wa ulaya.

Nywele za watu wa jamii ya ulaya (wazungu) zinatajwa kuwa ndio nywele dhaifu zaidi kati ya nywele za jamii mbalimbali. Hii inatokana na muundo wa nywele zao.

Kibaolojia nywele za jamii hii huwa na upana/unene mdogo jambo ambalo hupelekea nywele hizi kukusanya kiwango kidogo zaidi cha keratini.

Bila shaka utakuwa umejibiwa maswali yako mengi na makala hii kuhusu sayansi ya nywele na mambo yanayoathiri muundo na uimara wa nywele baina ya jamii. Tumia somo hili katika kuchagua kemikali sahihi kwa ajili ya utunzaji wa nywele zako.

Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url