Dalili za nimonia (homa ya mapafu) , tiba na jinsi ya kuzuia

Kuonekana kwa dalili za nimonia kunatofautiana kati ya mtu na mtu na hutegemea zaidi aina ya nimonia, umri wa mgonjwa na afya ya mgonjwa.

Vilevile dalili za nimonia hutegemea ni kwa kiasi gani tatizo limemuathiri mtu, aina ya vimelea na uwepo wa maradhi mengineyo katika mfumo wa upumuaji.

Si rahisi kuitambua nimonia ya kawaida kwa vile dalili zake hufanana na dalili za homa za kawaida za mafua na kikohozi

Dalili za nimonia.

Zifuatazo ni dalili za  nimonia ya kawaida.

  • Homa inayoambatana na kutokwa jasho na kutetemeka.
  • Kikohozi ambacho kinaweza kuambatana na makohozi au kikavu.
  • Maumivu ya kifua hasa wakati wa kukohoa.
  • Kupumua kwa shida.
  • Uchovu.
  • Maumivu ya kichwa.
  • Maumivu ya misuli na maungio.
  • Kichefuchefu na kutapika.
  • Kuchanganyikiwa na kupoteza fahamu.

Dalili za nimonia kali/sugu.

Dalili zote za nimonia za kawaida jumlisha dalili zifuatazo.

  • Vidole kubadilika na kuwa rangi ya bluu.
  • Sauti mithiri ya mruzi wakati wa kupumua.
  • Magonjwa ya sikio, vipele mithiri ya malengelenge.
  • Chakula kuingia koo la chakula kiurahisi, kupaliwa mara kwa mara.
  • Maambukizi ya ogani mbalimbali za mwili.
  • Kifua kuuma na kubana.
  • Mapigo ya moyo kwenda kasi.
  • Kikohozi kizito chenye makohozi yenye rangi. Makohozi yanaweza kuwa yenye rangi na ladha ya kutu, ya kijani, mekundu, na yenye harufu kali.

Jinsi ya kupima na kutambua tatizo la nimonia.

Kuna namna nyingi za kupima na kutambua uwepo wa ugonjwa wa nimonia. Uchunguzi wa macho na baadhi ya dalili zinaweza kutumika kuthibitisha ikiwa una ugonjwa wa nimoni.

Njia kuu zinazotumika kutambua uwepo wa ugonjwa wa nimonia ni pamoja na

  • Kutumia uchunguzi wa mionzi, Mfano X-ray na CT-Scan.
  • Kupima damu na kuangalia uwepo wa vimelea, dutu zinazochagiza kutengenezwa kwa uvimbe na kiwango cha seli za ulinzi katika damu.
  • Kupima makohozi ili kubaini uwepo wa vimelea.
  • Uchunguzi wa mapigo ya moyo na sauti maeneo ya kifua.

Jinsi ya kutibu tatizo na dalili za nimonia.

Nimonia inaweza kutibiwa kwa njia za kisasa na za kienyeji.

Njia za kisasa za kutibu nimonia..

Ugonjwa wa nimonia unatibiwa kwa namna tofauti kulingana na hatua na ukubwa wa tatizo, vilevile aina ya kimelea aliyesababisha tatizo.

Jinsi ya kutibu nimonia ya kawaida.

Mara nyingi Nimonia ya kawaida hutibiwa kwa kutumia kundi moja la dawa. Mgonjwa anaweza kutumia kundi moja ya kundi la dawa zifuatazo.

Dawa za antibiotiki la macrolides kama vile azithromycin na clarithromyci.

Dawa za antibiotiki la fluoroquinolones kama vile levofloxacinmoxifloxacin, au gemifloxacin.

Vilevile mgonjwa anaweza kutumia kundi la dawa za antibiotiki la tetracyclines kama vile Doxycycline.

Jinsi ya kutibu nimonia sugu/kali.

Wagonjwa wengi wenye aina hii ya nimonia huishia kulazwa kulingana na madhara na hali anayokuwanayo mgonjwa.

Dawa zinazotumiwa ni;

Dawa mseto kutoka makundi ya dawa za antibiotiki ya (fluoroquinolone + beta-lactam) au (macrolide + beta-lactam).

Baadhi ya dawa kutoka kundi la antibiotiki la beta-lactam ni pamoja na Amoxicillin, Ampicillin, Piperacillin, Cefixime, Ceftriaxone, Cefepime,Meropenem.

Matumizi ya antibiotiki zenye nguvu zaidi kama Vancomycin na linezolid. Hasa kwa wagonjwa ambao vimelea wao wametengeneza usugu wa antibiotiki za kawaida.

Njia za kienyeji za kutibu nimonia.

Mgonjwa anayetumia tiba za kisasa anashauriwa kutumia pia njia zifuatazo ili kuharakisha uponaji wa tatizo.

  • Kunywa maji ya kutosha.
  • Matumizi ya juisi ya uwatu.
  • Tumia maji ya vuguvugu na chumvi kidogo.
  • Tangawizi na bizali.
  • Mafuta ya mkaratusi.

Jinsi ya kujikinga na tatizo la nimonia.

  • Zingatia usafi wa mwili na mazingira yako.
  • Punguza au acha ulevi.
  • Epuka uvutaji wa sigara na bangi.
  • Zingatia lishe bora hasa matunda ili kuimarisha kinga ya mwili.
  • Pata chanjo ya nimonia.

Athari za kutotibu nimonia.

Kushindwa kutibu tatizo la nimonia kunaweza kukusababishia matatizo mengi ya afya ambayo ni hatari kwa uhai wako.

Baadhi ya athari za kutotibu nimonia ni pamoja na;

  • Mapafu kutengeneza vidonda na makovu hivyo kushindwa kufanya kazi.
  • Vidonda ndugu katika mfumo wa upumuaji hasa mapafu.
  • Kutengenezwa kwa usaha katika mapafu.
  • Maambukizi huweza kusambaa katika ogani nyingine za mwili.
  • Maradhi ya bakteria katika ubongo.

Hitimisho.

Katika makala hii tumeangazia kwa kina dalili na jinsi ya kutibu aina mbalimbali za nimonia.

Makala hii itumike kama jukwaa la kujielimisha na si muongozo rasmi wa jinsi ya kutibu ugonjwa wa nimonia.

Hupaswi kutumia dawa ya aina yeyote kati ya dawa zilizoainishwa katika makala hii bila ushauri wa mtaalamu wa dawa (mfamasia) na daktari.

Ikiwa unasumbuliwa na dalili zozote kati ya dalili zilizotajwa katika makala hii tafadhali fika kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

Usichukulie poa nimonia ni ya pili kwa kusababisha vifo nchini.

 


Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url