Faida za kitunguu saumu mwilini na jinsi ya kutumia

Kitunguu saumu kitaalamu hutambuliwa kama Allium sativum, ni moja kati ya mimea maarufu na ya muda mrefu kutumiwa na binadamu. 

Vitabu mbalimbali vya kihistoria vimeutaja mmea huu kama moja ya mimea ya kwanza kutumiwa na binadamu kama chakula klakini pia kutumiwa kama dawa.

Mmea huu unalimwa duniani kote, na hulimwa kwa kupandikiza punje za kitunguu ambacho tayari kimekomaa. Punje za kitunguu saumu hufukiwa chini na baadae hukua na kuzalisha punje nyingi zaidi.

Tafiti mbalimbali zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika zinathibitisha faida mbalimbali za kitunguu saumu kiafya na uwezo wake wa kukabiliana na matatizo ya kiafya ya binadamu. 

Baadhi ya matatizo ambayo kitunguu saumu kimethibitisha kuyatatua ni pamoja na; 
  • maradhi ya bakteria hasa yale yanayoshambulia mfumo wa upumuaji yaani puani, kooni na kifua, 
  • kitunguu saumu kimethibitisha kuwa na uwezo wa kupunguza rehemu mwilini, 
  • matatizo katika mzunguko wa damu kama vile shinikizo la damu
  • Vilevile husaidia watu wenye tatizo la kisukari aina ya pili (type 2 diabetes).

Faida za Kitunguu saumu zinatokana na nini?

Licha ya kuwa na ukali na radha isiyopendeza sana lakini ndani ya kitunguu saumu kuna dutu za kipekee ambazo hukifanya kuwa chakula adhimu na cha kipekee. 

Zifuatazo ni dutu muhimu zipatikanazo katika kitunguu saumu ambazo zinaupa mmea huu nguvu na uwezo wa kupambana na magonjwa mbalimbali.
  • Alliin, alliinase na allicin: Hizi ni dutu muhimu zaidi katika kitunguu saumu. Uwezo wa mmea huu kupambana na magonjwa kwa sehumu kubwa hutegemea kemikali hizi. Alliinase ni kimeng’enya ambaco huungana na alliin na kutengeneza allicin. Alliicin ndio dutu kuu ambayo huua vimelea vya magonjwa hata vile ambavo vimetengeneza usugu na dawa za kisasa.
  • Scordinins: Utafiti wa hivi karibuni unathibitisha dutu hii husaidia kutibu na kuzuia tatizo la saratani. Na ni moja ya dutu zinazopatikana kwa wingi zaidi katika kitunguu saumu.
  • Selenium: Madini joto haya ni ya lazima katika mwili ingawa yanahitajika katika kiwango cha kawaida. Kazi kubwa ya madini joto haya ni uwezo wake wa kupunguza sumu chaji katika mwili yaani hufanya kazi kama kiantioksideshaji, kuongeza utendaji kazi wa mwili na uzalishaji wa vinasaba.
  • Vitamins A, B, C, na E: Kitunguu saumu kina kiwango kikubwa cha vitamini ikiwamo vitamini A, Vitamin B, C, na E. Vitamini ni dutu muhimu zaidi katika ukuaji na maendeleo ya mwili.

Faida za Kitunguu saumu Mwilini

#1: Husaidia kutibu magonjwa ya bakteria.

Kabla ya kuanza kutengenezwa kwa dawa za kutibu bakteria kitunguu saumu kilitumika kwa kiwango kikubwa hasa wakati wa vita kuu ya kwanza ya dunia ambapo askari waliojeruhiwa walipewa na kufungwa vitambaa sambamba na vitunguu saumu.

Alliicin katika kitunguu saumu ndio inatajwa kuwa na uwezo wa kuua na kuangamiza vimelea vya bakteria hata vile ambavyo vimetengeneza usugu na dawa za kawaida za kisasa. 

Matumizi sahihi ya kitunguu saumu hukukinga pia na magonjwa hayo. Mfano wa magonjwa yanayowezatibiwa na kitunguu saumu ni 
  • Magonjwa ya mfumo wa mkojo(UTI), 
  • kifua kikuu
  • kuharisha
  • matatizo ya minyoo
  • matatizo ya ngozi kama vile majipu 
  • uvimbe
  • kikohozi, 
  • mafua
  • kuwashwa kooni.
Utafiti uliofanywa na Journal of Antimicrobial Chemotherapy, unaonyesha uwezo wa allicin katika kuangamiza bakteria ni mara 100 ya uwezo wa kutibu wa dawa za kawaida za kutibu maradhi ya bakteria.

#2: Hupunguza shinikizo la damu.

Mbali na kutibu lakini pia matumizi ya mara kwa mara ya kitunguu saumu husaidia kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya moyo. 

Kemikali ya Diallyl trisulfide ndani ya kitunguu saumu ndio hasa huusishwa na uwezo wa kitunguu saumu kutibu maradhi ya mzunguko wa damu.

#3: Hutibu maradhi ya kikohozi, mafua na kifua.

Hasa yale yalioambatana na bakteria, tafiti mbalimbali za kisayansi zinaonyesha hakuna bakteria anaweza kupona mbele ya Alliicin, silaha iliyomo ndani ya kitunguu saumu. 

Lakini pia uwepo wa vitamin C ndani ya kitunguu saumu husaidia kuimarisha kinga ya mwili.

#4: Hukukinga na maradhi ya saratani.

Uwepo wa scordinins katika kitunguu saumu kunaupa mmea huu uwezo wa kipekee wa kupambana na maradhi ya saratani vilevile kupunguza uwezekano wa kupata saratani. 

Tafiti mbalimbali zimefanywa na kudhibitisha uwezo wa scordinins katika kupambana na saratani. Kemikali hii ni moja ya silaha adimu zinazopatikana katika kitunguu saumu.

#5:  Husaidia kuangamiza minyoo katika mwili.

Matumizi ya kitunguu saumu husaidia katika kupambana na maradhi yasababishwayo na minyoo hii inatokana na uwepo wa Alliicin.

#6: Husaidia kupunguza na kuondoa tatizo la kisukari.

Kitunguu saumu kinaweza kukusaidia kujikinga, kupunguza au kumaliza tatizo la kisukali hasa kisukari aina ya pili. 

Hii hutokana na uwezo wa kitunguu saumu kuongeza utendaji kazi wa mwili.

Ongezeko la utendaji kazi wa mwili hupelekea mwili kuhitaji kiwango kikubwa cha nishati ambapo ziada ya sukari katika mwili hulazimishwa kutumiwa kama nishati.

#7:Hutumika kutibu maradhi ya Fangasi.

Kitunguu saumu hutumiwa kama tiba mbadala ya fangasi kwa kutafuna au kupaka sehemu iliyoathirika.

Moja ya tiba asili za fangasi zenye ufanisi wa hali ya juu. Si kingine bali ni uwepo wa Alliicin, silaha pekee ambayo huipati kwingine kwa kiwango kikubwa na kwa unafuu zaidi ya kitunguu saumu.

Faida nyinginezo za kitunguu saumu ni pamoja na;

  • kutibu tatizo la  pumu,
  • tezi dume 
  • maumivu ya magoti 
  • kiharusi na shambulizi la moyo 
  • maradhi ya masikio, 
  • chunusi na majipu

Ni sehemu ipi hutumika kama tiba?

Sehemu zote za mmea wa kitunguu saumu zina faida na zinafaa kuliwa, lakini punje za kitunguu saumu ndio hasa huweza kukuletea faida za kitabibu kama zilivyoainishwa hapo juu. 

Unaweza kuandaa kitunguu saumu katika namna mbalimbali kama vile;
  • Unga wa kitunguu saumu
  • Mafuta
  • Vidonge lishe.

Namna gani ya kuandaa kitunguu saumu kama dawa?

Si kila utumiapo kitunguu saumu basi utafaidika na faida zake za kiafya, la hasha kuna namna ambayo unapaswa kukiandaa kitunguu ili upate kilichobora zaidi kwa manufaa ya kiafya.

Katika namna ya asili yake kitunguu saumu hakina Alliicin! Kemikali hii ya Alliicin hupatikana pale tu Alliicinase(kimeng’enya) huungana na Alliin. 

Jambo hili hutokea ikiwa tu  Kitunguu saumu kitapondwa au kutafuna. Jinsi unavyotafuna au kikiponda kwa muda mrefu ndivyo unarahisisha muungano wa Alliicinase na Alliin kuwa mkubwa hivyo utengenezwaji wa Alliicin kuwa mkubwa, vilevile uwezo wa kutibu wa kitunguu saumu unaongezeka.

Ili kutengeneza kiwango kikubwa cha kemikali hii ya Alliicn unashauriwa  kuuacha mchanganyiko huu uliopondwa walau dakika 1 ili kuruhusu kiwango kikubwa cha Alliicin kupatikana.

Jinsi ya kutumia Kitunguu saumu kama tiba.

Tumia punje 3 hadi 5 kila siku au unaweza kutengeneza juisi ya kitunguu saumu kwa kuchanganya punje zisizopungua 20 katika mililita 100(glasi 1 ya maji) kisha tumia kijiko 1 kila baada ya masaa 3.

Matumizi haya ni kwa watumiaji ambao tayari wanasumbuliwa na maradhi tajwa hapo juu. 

Matibabu ya mitishamba yanaweza kuchukua kati ya siku 14 hadi 21 kupata matokeo chanya. Hivyo basi unashauriwa kutumia kitunguu saumu kila siku kwa muda usiopungua siku 14 mfululizo.

Kwa matatizo ya sikio tumia kiwango kidogo cha unga wa kitunguu saumu kupaka au kuweka ndani ya sikio.

Kwa matatizo ya ngozi unaweza tengeneza mchangayiko mzito bila kuchanganya na maji kisha kupaka sehemu yenye tatizo.
 
Muhimu
Matumizi ya kitunguu saumu kama tiba hayashauriwi kufanyiwa Watoto chini ya umri wa miaka 12.

Hitimisho

Kuna faida nyingi za kutumia kitunguu saumu kila siku. Mbali na kutumika kama tiba, matumizi ya kila siku ya kitunguu saumu ina kusaidia na kukukinga na maradhi kadhaa ya mwili hasa maradhi ya mfumo wa mzunguko wa damu na moyo.

Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url