Njia kuu 4 za asili za uzazi wa mpango na jinsi ya kuzitumia

Ili kujikinga na wimbi la mimba zisizotarajiwa ambalo huwaathiri wanawake katika nyanja mbalimbali, elimu juu ya uzazi wa mpango ni muhimu.

Matumizi sahihi ya njia za uzazi wa pango humkinga mwanamke dhidi ya mimba zisizotarajiwa lakini pia baadhi ya njia hizi hutoa ulinzi dhidi ya maradhi mbalimbali ya mwili.

Kimsingi njia za uzazi wa mpango zimegawanywa katika aina kuu mbili, ambazo ni:
  • Njia za uzazi wa mpango za kienyeji/Asili,
  • Na njia za uzazi wa mpango za kisasa.
Katika makala hii tutaangazia njia mbalimbali za asili uzazi wa mpango kwa wanawake na wanaume na jinsi njia hizo hutumiwa.

Njia za Asili za uzazi wa mpango.

Hizi ni njia za asili ambazo zinaweza kufanywa na mtu yeyote. Njia hizi ni rahisi kutumia na hazina gharama.

Baadhi ya njia hizi zinahitaji utayari wa wapenzi wote kwa vile zinahitaji zaidi umakini na ushirikiano wa wahusika.

Baadhi ya njia hizi ni pamoja na;

#1: Kutoa uume wakati wa kufika kileleni (Kumwaga nje ya uke).

Hii ndio njia kongwe zaidi ya uzazi wa mpango kuwahi kutumiwa na binadamu. Njia hii inahitaji mwanaume kumwagia nje mbegu zake mara tu afikapo kileleni.

Ni njia inayohitaji umakini na ushirikiano wa hali ya juu kati ya wapenzi wakati wa kujamiana. Mwanaume anahitajika kuwa na uwezo mkubwa wa kujithibiti kiakili, kifikra na kimwili ili njia hii ifanikishe.

Hata hivyo kutokana na ugumu wa njia hii watu wengi wanaochagua njia hii hushindwa kufanikisha lengo.

#2: Kunyonyesha.

Mwanamke anayenyonyesha anazalisha homoni ya prolactini. Homoni hii huzuia upevukaji wa yai, hivyo mwanamke hukosa uwezo wa kushika mimba vilevile kushindwa kupata hedhi katika kipindi cha kunyonyesha.

Homoni hii ya prolactini huweza kuzalishwa kwa muda hadi wa miezi 6 ikiwa mama anayenyonyesha atanyonyesha walau masaa 8 kwa siku, yaani masaa 4 mchana na masaa 4 usiku.

Kutokana na changamoto za wamama kipindi cha kunyonyesha, ni asilimia chache ya wamama ambao hunyonyesha watoto wao katika kiwango hiki.

Changamoto mbalimbali kama vile muda mwingi mtoto anakuwa amelala, maumivu ya chuchu, vidonda katika chuchu na mengine mengi.

Yote haya huathiri kiwango cha unyonyeshaji na kufanya dhana ya kumnyonyesha mtoto masaa 4 na 4 usiku kuwa ni ya kinadharia zaidi kuliko vitendo.

Kutokana na hali hii basi, zaidi ya 60% ya wanawake wanaonyonyesha, homoni ya prolactini huacha kuzalishwa kwa wingi baada ya miezi 4 au 5 ya kunyonyesha.

Kwa hivyo basi kwa mama anayenyonyesha kinga dhidi ya kupata mimba husababishwa na homoni ya prolactini ambayo hudumu takribani miezi 3 baada ya kuanza kunyonyesha.

Baada ya miezi 3, uwezekano wa kushika ujauzito kwa mama anayenyonyesha unakuwa ni mkubwa na kama homoni ya prolactini imeachwa kuzalishwa basi anaweza kuanza kupata hedhi pia.

#3: Uzazi wa mpango kwa njia ya kalenda.

Njia hii hutumiwa kwa kutabiri upevukaji wa yai la mwanamke. Utabiri huu unaenda sambamba na uelewa wa kutosha juu ya mzunguko wa hedhi.

Kwa mwanamke siku za kupata mimba ni kipindi ambacho yai lake limepevuka. Siku hizi za yai kupevuka zinaweza kutabiriwa kwa kutumia kalenda ya mzunguko wa hedhi.

Mwanamke anapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mzunguko wake wa hedhi kiasi cha kutambua siku za yai kupevuka na kupata mimba.

Baada ya kuzifahamu siku za yai kupevuka, mwanamke anaweza kuepuka mimba kwa kujiepusha na kujamiana katika kipindi hiki.

Hata hivyo njia hii haina ufanisi mkubwa miongoni mwa wanawake kutokana na elimu duni juu ya afya ya uzazi na mzunguko wa hedhi.

Ikiwa itatumika kwa ufasaha, hii ndio njia pekee ambayo ni bora na rahisi, vilevile ndio njia ambayo haivurugi misingi ya kimila na kiimani.

#4: Jiepushe na kujamiana pamoja na ngono.

Bila shaka hii ndio njia pekee salama na inayokubalika na jamii na desturi zote za ulimwengu.

Si tu inakukinga dhidi ya mimba, vilevile ni njia bora ya kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ya zinaa.

Njia hii ni bora zaidi hasa kwa wanafunzi na mabinti wadogo ambao bado wako katika uangalizi wa wazazi/walezi.

Changamoto ya njia za asili za uzazi wa mpango.

Zipo changamoto kadhaaza kutumia njia za asili za uzazi wa mpango, baadhi ya changamoto hizo ni kama zifuatazo;
  • Baadhi ya njia zinakinzana na mila, desturi, tamaduni na imani. Mfano Njia ya kumwagia nje.
  • Elimu duni juu ya afya ya uzazi hasa elimu ya mzunguko wa hedhi.
  • Ushirikiano hafifu baina ya wapenzi au wanandoa.
  • Maradhi mbalimbali ya mwili yanaweza kuathiri afya ya uzazi na mzunguko wa hedhi.

Hitimisho

Uzazi wa mpango ni muhimu kwa ustawi wa jamii bora na yenye afya. Una uwanja mpana wa kuchagua njia gani utumie ya kupanga uzazi, njia za kisasa za kupanga uzazi au njia za asili za mpango wa uzazi.

Licha ya changamoto zake, lakini njia za asili za uzazi wa mpango ndio njia salama zaidi katika kupanga uzazi ukilinganisha na njia za kisasa.

Iwapo utaamua kutumia njia za asili katika kupanga uzazi hakikisha unapata elimu ya kutosha juu ya njia ulioichagua kutoka kwa mtaalamu wa afya na masuala ya uzazi.

Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url