Njia za kisasa za uzazi wa mpango na faida zake

Uzazi wa mpango ni hali ya kuzuia mimba kutunga kwa kuathiri mchakato wa kibaolojia unaopelekea mimba kutunga kwa kutumia njia za kisasa au za asili.

Lengo la uzazi wa mpango ni kuzuia mimba kutunga na si kuzuia mimba kukua. Katika kufanikisha jambo hili zipo njia mbalimbali za kisasa na za asili ambazo unaweza kuzitumia.

Katika makala hii tutaangazia njia za uzazi wa mpango za kisasa na jinsi njia hizi zinatumika pamoja na faida zake.

Njia za kisasa za uzazi wa mpango

#1: Matumizi ya mipira (kondomu).

Njia hii inaweza kutumiwa na watu wa rika na jinsia zote. Zipo kondomu kwa ajili ya wanaume na wanawake.

Mbali na kutumika kama njia ya uzazi wa mpango, matumizi sahihi ya kodomu pia hutoa zaidi ya 95% ya ulinzi dhidi ya magonjwa ya zinaa na magonjwa mengneyo kama vile UTI.

#2: Matumizi ya homoni kama njia ya uzazi wa mpango.

Njia hizi hutumia homoni kuthibiti au kuzuia kutungwa kwa mimba kwa namna zifuatazo ambazo ni:
  • Kuthibiti au kuzuia upevukaji wa yai la mwanamke.
  • Kuongeza ute katika mlango wa kizazi ili kuzuia manii kuingia.
  • Kusababisha kusinyaa kwa mfuko wa uzazi.
Matumizi ya homoni katika kupanga uzazi yanatokana na mchango wa homoni katika mchakato mzima wa kuthibiti hatua na mabadiliko mbalimbali katika mfumo wa uzazi.

Hii inatokana na msukumo wa homoni hizi katika mfumo wa uzazi na mzunguko wa hedhi kwa wanawake.
Baadhi ya homoni zinazotumika katika kupanga uzazi ni pamoja na;
  • Progestrin 
  • Levonogestrel
  • Norethindrone
  • Etonogestrel
  • Nestorone
  • Cyproterone acetate
Homoni hizi huweza kutumiwa katika kupanga uzazi kwa namna na muudo mbalimbali kama vile;
  • Njia ya kitanzi ya uzazi wa mpango.
  • Uzazi wa mpango kwa kutumia vipandikizi.
  • Sindano za uzazi wa mpango.
  • Vidonge vya uzazi wa mpango.
  • Matumizi ya plasta za uzazi wa mpango.
  • Matumizi ya ringi maalumu ukeni.

#3: Njia za uzazi wa mpango za kutumia dutu maalumu na kemikali sumu.

Moja ya njia ya kisasa ya uzazi wa mpango ni ile ambyo huangamizi mbegu za mwanaume kabla hazijafikia yai kwa kutumia kemikali sumu.

Kemikali hii hupachikwa ndani ya mfumo wa uzazi wa mwanamke, au maeneo ya nje ya uke. Baadhi ya njia zinazotumia sumu kuua mbegu za kiume ni pamoja na;

3.1: Matumizi ya vitanzi vyenye madini joto ya shaba.

Shaba ina uwezo wa kuangamiza mbegu za kiume kwa ufanisi wa hadi 99%.

Mbali na kuzuia urutubishwaji wa yai kwa kuangamiza manii, vilevile shaba ina uwezo wa kuzuia yai lililorutubishwa kujishikiza katika tumbo la uzazi kwa ajili ya ukuaji wa mtoto hivyo kuzuia ukuaji wa mimba.

Hii ndio njia ya uzazi wa mpango ambayo huweza kuchukua miaka mingi zaidi kuliko njia yoyote bila kupoteza uwezo wa mwanamke kuzaa.

Mwanamke akiwekewa kitanzi chenye madini joto ya shaba inaweza kuchukua takribani miaka 10 bila kupata ujauzito ikiwa atakiacha kitanzi hicho ndani ya mfumo wake wa uzazi.

3.2: Matumizi ya sumu za kuua manii.

Mwanamke anaweza kutumia vifaa maalumu vya kupachika ukeni ambavyo vimewekewa sumu maalumu ya kuua mbegu za kiume.

Sumu inayotumiwa zaidi ni nonoxynol-9 (N-9). Sumu hii inaweza kuwekwa kwenye vifaa vya aina mbalimbali ambavyo hupachikwa ukeni.

Baadhi ya vifaa hivyo ni sponji maalumu ambayo hupachikwa ukeni dakika 30 kabla ya kujamiana na huondolewa baada ya siku moja kupita baada ya kujamiana.

Vifaa vingine ni pamoja na kikofa cha mlango wa uzazi na diaframu maalumu ambazo zote hupachikwa ukeni dakika kadhaa kabla ya kujamiana na huondolewa ndani ya masaa 8 baada ya kujamiana.

#4: Njia za uzazi wa mpango za dharula.

Pamoja na tahadhari mbalimbali hasa wapenzi wanaotumia njia za asili za uzazi wa mpango, kuna wakati mambo huenda kombo.

Katika hali hii wahusika wanahitaji njia ya dharula ya kuzuia mimba kutunga au kuendelea kukua ikiwa tayari imekwisha anza kukua.

Zipo njia ambazo mwanamke anaweza kutumia kufanikisha hili. Njia hizo ni kama ifuatavyo:

4.1: Kwa kutumia kitanzi cha madini joto ya shaba.

Hii ndio njia pekee ya dharula yenye ufanisi mkubwa katika kuzuia mimba kutunga au kuendelea kukua.

Kitanzi hiki huweza kupachikwa kwa mwanamke ndani ya masaa 120 takribani siku 5 baada ya kujamiana na kikawa na ufanisi wa hadi 95%.

Ufanyaji kazi wa aina hii ya kitanzi cha shaba huendelea muda wote ambao kitabaki katika mji wa uzazi.

4.2: Vidonge vya dharula vya Progestrin.

Ikiwa huna uwezo wa kupata kitanzi cha shaba, njia hii ndio chaguo la pili kuzuia mimba ya dharula.

Vidonge hivi vimetengenezwa kwa homoni ya progestrin aina ya levonogestrel au emerginogestrel.

Vidonge hivi huweza kutumika kama dozi moja au dozi mbili tofauti.

Ikiwa vitatumika kama dozi mbili tofauti basi mwanamke anapaswa kutumia kidonge 1 kila baada ya masaa 12.

Kidonge hiki kinapaswa kutumika ndani ya masaa 72 baada ya kujamiana na ufanisi wa dawa hii kiutendaji hutegemea jinsi utakavyowahi kuitumia.

Kwa wanawake wengi ufanisi wa dawa hii ni 85% ikiwa itatumika ndani ya masaa 24, 66% ya ufanisi ikiwa itatumika ndani ya masaa 48.

Na ufanisi hupungua zaidi na kufikia chini ya 50% ikiwa itatumika baada ya masaa 50 ya kujamiana.

Sehemu kubwa ya wanawake nchini Tanzania hutumia njia hii kutokana na urahisi wa upatikanaji na gharama zake.

Kwa wastani, dawa kidonge hiki hupatikana kwa kati ya Tshs 2000 hadi 7000 katika maduka karibu yote ya dawa.

#5: Njia za uzazi wa mpango za moja kwa moja.

Kwa wapenzi au wanandoa ambao tayari wamepata watoto na kuamua kutopata mtoto tena katika maisha yao, wanaweza kutumia njia za kufunga kizazi.

Njia hizi ni za moja kwa moja, maana yake baada ya kuitumia hautakuwa na uwezo wa kushika mimba au kushikisha mimba.

Kwa sasa zipo njia kuu tatu za kufanikisha njia hii ya kupanga uzazi, ambazo ni:

5.1: Vipandikizi maalumu katika milija ya uzazi.

Njia hii ni ya kisasa na hufanywa kwa mwanamke ambapo vipandikizi maalumu huingizwa katika milija ya falopia kupitia uke bila upasuaji.

Baada ya muda wa takribani miezi 3, vipandikizi hivi husababisha kuziba kwa milija hii ya falopia kwa kutengeneza makovu katika milija hiyo.

Kuziba kwa milija hii ni kwa moja kwa moja, hakuna namna hali inaweza kujirudi na milija kuzibuka.

Uangalizi na ufuatiliaji wa kitaalamu unatakiwa ili kujiridhisha na ufanisi wa njia hii.

5.2: Kufungwa kwa milija ya uzazi kwa njia ya upasuaji.

Katika njia hii mwanamke hufanyiwa upasuaji mdogo kisha milija ya falopia hukatwa na kufungwa kiasi cha kupoteza uwezo wa kupitisha mayai au mbegu za kiume.

5.3: Kufungwa kwa mlija wa manii.

Njia hii hufanywa kwa mwanaume ambapo milija ya kupitisha manii iitwayo vas deferens hukatwa na kufungwa kwa ajili ya kuzuia manii kupita na kuingia katika mlija wa urethra.

Hitimisho.

Kama zilivyoainishwa katika makala hii, kuna njia nyingi za uzazi wa mpango. Kila mtu ana uhuru wa kuchagua njia aipendayo kutokana na sababu zake binafsi.

Mbali na kuwa na uhuru wa kuchagua njia uipendayo, si kila njia ya uzazi wa mpango inaweza kuwa sahihi kwako.

Hakikisha unapata ushauri wa kitaalamu kuhusu njia hizi za uzazi wa mpango kabla ya kuamua njia ipi ni sahihi kwako.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url