Jinsi aina za nywele zinvyoathiri mitindo ya nywele.

Mitindo ya nywele ni moja ya sanaa inayopendwa zaidi na wanawake kwa vile ni miongoni mwa mambo ambayo huwaongezea mvuto na muonekano.

Moja ya changamoto kubwa katika urembo wa nywele ni mipaka ya unyambulikaji na uimara wa nywele.

Kwa sehemu kubwa mitindo mbalimbali ya nywele huathiriwa zaidi na unyumbulikaji, rangi na uimara wa nywele, jambo linalopelekea wanawake wengi kuwa na mipaka ya machaguo ya kuzitinda na kuziremba nywele zao.

Habari njema ni kwamba jamii ya watu wenye asili ya kiafri wamejaliwa kuwa na aina za nywele ambazo ni imara zisizo na mipaka ya unyumbulikaji.
Uimara na unyumbulikaji wa nywele za watu kutoka jamii ya kiafrika kunawafanya watu hawa kuwa ndio jamii pekee ulimwenguni ambayo haina mipaka katika kuamua mitindo mbalimbali ya nywele yenye kupendeza na kuvutia iliyojaa ubunifu wa hali ya juu.

Jambo hili huifanya sanaa hii ya mitindo ya nywele kwa jamii ya kiafrika kuwa moja ya nguzo kuu za urembo na mvuto.

Tofauti za Uimara, mga’o na unyumbulikaji wa nywele.

Uimara, mg'ao na unyumbulikaji wa nywele hutegemea zaidi na dutu zilizounda nywele husika.

Kwa upande wa mg’ao wa nywele, mga'o wa nywele hutofautiana kati ya jamii moja na nyingine kulingana na kiwango cha dutu za mafuta na maji katika nywele.

Nywele za watu wa jamii za kiafrika na Asia zinatajwa kuwa ndio nywele zinazoongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha mafuta na maji.

Nywele jamii ya Asia zina kiwango kikubwa cha mafuta na maji wakati nywele za kiafrika zina kiwango kikubwa cha mafuta lakini kiwango kidogo cha maji.

Hali ya kuwa na kiwango kikubwa cha mafuta na maji kunazifanya nywele za watu wa jamii ya Asia kuwa ndio nywele zenye kung’ara na kuteleza bila kukatika kuliko nywele za jamii yoyote.

Kwa upande mwingine hali ya nywele za kiafrika kuwa na mafuta mengi kuliko maji kunazifanya kuwa ni nywele zinazoongoza kwa ukakamavu.

Lakini pia kunazifanya kuwa ni aina pekee ya nywele ambazo ni rahisi kunyumbulika na kukatika ikiwa zitakutana na nguvu ya kiasi kama vile wakati wa kusuka na kutana nywele.

Wakati nywele kutoka jamii za Asia na Afrika zikitajwa kuwa ndio nywele zenye mafuta na maji mengi, nywele za watu kutoka jamii ya Ulaya wao wako katikati.

Yaani nywele zao zina mafuta na maji ya wastani , hali hii inafanya nywele hizi kuwa na muonekano wa mg’ao zaidi ya zile za kiafrika lakini mg’ao hafifu ukilinganisha na zile za watu wa jamii ya Asia.

Athari za mafuta na maji katika mitindo ya nywele.

Kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha maji, nywele za kiafrika ndio nywele ambazo zinaweza kunyumbulika katika namna tofauti na kubaki katika mnyumbuliko husika kwa muda mrefu kuliko aina nyingine ya nywele.

Uwezo wa kunyumbulika katika mitindo tofauti bila kukatika ni kutokana na kuwa na kiwango kikubwa na cha kutosha cha mafuta katika nywele za kiafrika.

Matumizi ya mafuta katika kusaidia mnyumbuliko huu ni muhimu hasa kwa wale ambao nywele zao zina kiwango kidogo cha mafuta.

Mafuta yanayopendekezwa ni yale yaliyo na virutubisho sahihi kwa ajili ya kutunza na kurefusha nywele ambavyo ni vitamini D na E, pamoja na madini joto ya chuma.

Mafuta bora ya nywele yanayopendekezwa ni pamoja na mafuta ya;   
  • Mnyonyo,
  • Mzeituni, 
  • Parachichi na 
  • Karanga 
Kwa upande wa pili, nywele za jamii ya watu wa Asia na ulaya si nywele rafiki kwa mitindo mbalimbali ya nywele kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha maji na mafuta, pia kiwango kidogo cha madini ya salfa.

Hivyo kuzifanya kuwa nywele zinazoteleza zaidi na kutofaa kwa mitindo mbalimbali kama zilivyo nywele za kiafrika.

Tofauti za rangi za nywele kama moja ya mitindo ya nywele.

Rangi ya nywele hutegemea zaidi na uwepo wa dutu za rangi ambazo kitaalamu hutambulika kama Melanini.

Kemikali hii hutengenezwa katika sehemu ya chini ya nywele. Seli za melanosaiti ndio hasa mashine kuu ya utengenezaji wa dutu hizi.

Melanini kwa asili ina rangi nyeusi. Lakini kemikali hizi za melanini katika nywele hutengenezwa katika aina kuu aina mbili, ambazo ni;
  • Eumelanini.
  • Pheomelanini.
Rangi ya nywele zako inategemea zaidi na kiwango na aina ya melanini zilizopo katika nywele zako.

Zifuatazo ni aina kuu za kemikali ya melanini ambayo inaweza kupatikana katika nywele;

Eumelanini.

Hii ni moja ya aina kuu mbili za melanini ambazo hupatikana katika nywele. Aina hii ya melanini inaweza kutokea katika rangi ya kahawia au nyeusi.

Weusi wa nywele hutegemea zaidi kiwango cha kemikali hizi, watu wenye nywele za kahawia hutajwa kuwa na kiwango kidogo cha eumelanini na watu wenye nywele nyeusi hutajwa kuwa na kiwango kikubwa cha eumelanini.

Nywele za jamii ya kiafrika ndio nywele zilizoundwa na kemikali hizi kwa wingi kuliko jamii nyingine ya nywele.

Jambo hili linafanya nywele za kiafrika kuwa ndio nywele zenye rangi nyeusi zaidi ya nywele za jamii yoyote duniani.

Jamii nyingine ambazo nywele zao zimeundwa na kemikali hii ni jamii za watu wa Asia, Amerika ya kati na Ulaya magharibi.

Pheomelanini.

Hii ni aina ya pili ya melanini inayopatikana katika nywele. Aina hii ya melanini inaweza kutokea katika rangi ya njano, nyeupe au nyekundu.

Nywele za jamii nyingi za watu wa Ulaya (wazungu) zinatajwa kuwa ndio nywele zenye kiwango kikubwa cha Pheomelanini.

Kutokana na sababu hii ni katika jamii hizi pekee tunaweza kushuhudia watu wakiwa na nywele zenye rangi nyeupe, njano au nyekundu.

Tofauti na kemikali za eumelanini, pheomelanini inatajwa kuwa ni aina ya melanini ambayo ni dhaifu katika kupambana na hatari zinazoweza kuikabili nywele.

Melanini ndio hutoa kinga katika nywele dhidi ya mionzi hatari ya jua na kemikali mbalimbali mfano vipodozi.

Hivyo basi, udhaifu wa melanini aina ya pheomelanini kunawafanya watu wa jamii za ulaya kuwa na nywele dhaifu na rahisi kuathiriwa na mionzi na kemikali kuliko aina nyingine ya nywele.

Kwa upande wa pili nywele za kiafrika ndio nywele imara zenye uwezo wa kuhimili hatari za mionzi na kemikali kwa kiwango kikubwa bila kuharibika, zikifuatiwa na nywele jamii ya Asia na baadhi ya maeneo ya Amerika.

Muhimu juu ya mitindo ya nywele.

Mitindo ya nywele huathiriwa zaidi na uimara na kiwango cha mafuta katika nywele.

Licha ya faida ya kuwa na nywele bora, imara na zenye kunyumbulika bado muonekano wa nywele za kiafrika imekuwa ni changamoto kubwa hasa kwa wanawake.

Hii inatokana na kuwa na elimu duni juu ya utunzaji wa nywele na matumizi ya kemikali ambazo ni kali na si rafiki kwa nywele za kiafrika.

Ili kuongeza mvuto na kupendezesha muonekano wa nywele zako jambo la msingi ni kutambua aina ya nywele zako. Je, ni za mafuta mengi, ni kavu au ni mchanganyiko.

Baadha ya kufahamu hilo ni vyema kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa mambo ya urembo au wataalamu wa afya kwa msaada na ushauri sahihi juu ya ni kitu gani nywele yako inahitaji.

Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url