Mambo ya kuzingatia ili kurefusha na kutunza nywele zako kwa ufanisi.

Ukuaji wa nywele za kiafrika una changamoto nyingi, changamoto ambazo huathiri kwa kiwango kikubwa ubora wa nywele.

Moja ya sababu kubwa inayosababisha changamoto hizi ni kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya nywele.

Watu wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu sayansi ya nywele na utunzaji sahihi. Jambo hili hupelekea maamuzi yasiyo sahihi katika kuchagua njia sahihi ya utunzaji wa nywele.

Siri ya Ukuaji wa nywele.

Baada ya kuzaliwa nywele zote za mwili wako isipokuwa kope, nyusi na nywele za kichwani huanza kukua kwa kasi moja.

Ukuaji wa nywele hubadilika zaidi mtu anapofikia balehe. Baada ya balehe baadhi ya nywele huanza kuota kwa kasi na kuwa ndefu kuliko nywele nyingine.

Nywele ambazo uotaji wake huathiriwa na balehe ni pamoja na ndevu, nywele za kwapani, na nywele katika nyeti.

Nywele nyinginezo hasa kope, nyusi na nywele za kichwani uotaji wake unategemea zaidi chembe za urithi (vinasaba), lishe na matunzo.

Mbali na vinasaba pia kuna dutu na vipokezi kadhaa mwilini ambazo kwa pamoja zinafanikisha ukuaji sahihi wa nywele.

Tatizo katika vinasaba, dutu na vipokezi linaweza kusababisha mapungufu kadhaa ya ukuaji wa nywele kama vile upara, nywele nyekundu, na mvi.

Kwa kuzingatia mambo yote muhimu uotaji wa nywele hupitia hatua kuu nne. Hatua hizo ni kama ifuatavyo;
  • Anagen
  • Catagen.
  • Telogen.
  • Exogen.

Anagen ( Hatua ya kwanza ya ukuaji wa nywele ).

Hii ni hatua ya kwanza ya ukuaji nywele kati ya hatua nne. Katika hatua hii nywele hutengenezwa na seli hai zilizopo katika shina sambamba na rangi ya nywele. Kadri nywele inavyotengenezwa ndivyo inavyozidi kuchomoza.

Hii ndio hatua ndefu zaidi kati ya hatua za ukuaji wa nywele. Kwa nywele za kichwani hatua hii huchukua kati ni kati ya mwaka 1 hadi 10.

Na kwa nywele za mikono, miguu, kope, nyusi, kwapani na nyeti ni kati ya miezi 1 hadi 8.

Katika kipindi chote cha hatua nywele huota kwa kasi ya milimita 0.2 hadi milimita 0.4 kwa siku.

Sawa na sentimita 0.6 hadi sentimita 1.2 kwa mwezi ambapo kwa mwaka ni kati ya sentimita 7.2 hadi sentimita sentimita 14.4.

Katika hatua hii kati ya 80% hadi 90% ya nywele zako za kichwani huwa katika hatua hii muda wowote, hata wakati unasoma makala hii.
Je kuna watu ambao nywele zao hukua zaidi ya wengine?

Nywele za kiafrika ndio nywele zinazokuwa kwa kasi zaidi kuliko jamii nyingine ya nywele.
Tofauti ya ukuaji wa nywele baina ya jamii moja unategemea na mambo kadhaa ikiwemo 
  • Urithi wa vinasaba vinavyoshughulikia ukuaji wa nywele.Lishe bora.
  • Kiwango cha homoni.
  • Dutu nyinginezo za uratibu wa ukuaji wa nywele.
  • Utunzaji bora wa nywele na,
  • Magonjwa yanayoshambulia nywele na shina la nywele.
  • Urefu wa hatua hii ya kwanza ya ukuaji wa nywele.
Kasi ya ukuaji wa nywele yaweza kuwa sawa lakini tofauti ya urefu wa hatua hii ya anagen inaweza kuwa ndio sababu ya utofauti wa urefu wa nywele baina ya watu.

Mfano mtu ambaye hatua hii huchukua miaka 4, ikiwa nywele zake hukua kwa kasi ya sentimita 10 kwa mwaka, maana yake ndani ya miaka 4 nywele zake hufikia sentimita 40.

Baada ya miaka 4 nywele hizi hazikui tena, yaani huendelea na hatua nyingine na kuharibika.

Kwa hivyo mtu huyu kiwango cha juu cha nywele zake kukua huchukua miaka 4 na hazizidi urefu wa sentimita 40.

Lakini pia kwa mtu ambaye hatua hii huchukua miaka 6, ikiwa nywele zake hukua kwa kasi ya sentimita 10 kwa mwaka,maana yake ndani ya miaka 6 nywele zake hufikia sentimita 60.

Baada ya miaka 6 nywele hizi hazikui tena, yaani huendelea na hatua nyingine na baadae kuharibika.

Kwa hivyo mtu huyu kiwango cha juu cha nywele zake kukua huchukua miaka 6 na hazizidi urefu wa sentimita 60.

Catagen (Hatua ya pili ya ukuaji nywele).

Hii ni hatua ya pili ya ukuaji wa nywele ambapo utengenezwaji wa nywele kutoka seli zilizopo katika shina la nywele husinyaa na aadae kusimama.

Vilevile utengenezwaji wa chembe za rangi ya nywele (melanini) pia husimama. Hali hii husababisha nywele kupoteza mshikamano na shina la nywele na kuanza kusogea juu.

Hatua hii huchukua takribani muda wa siku 10 hadi 25 ambapo asilimia 3% ya nywele za kichwani huwa katika hatua hii muda wowote hata pindi usomapo makala hii.

Telogen (Hatua ya tatu ya ukuaji wa nywele).

Katika hatua hii hakuna ukuaji wowote wa nywele unaendelea. Hatua hii hutajwa ni hatua ya mpito ambapo nywele hujiachia kutoka katika shina kabla ya kunyofoka.

Pia katika hatua hii hakuna nywele inayodondoka. Hatua hii huchukua kati ya muda wa mwezi 1 hadi miezi 3. Na wakati wowote 10% ya nywele zako huwa katika hatua hii.

Exogen (Hatua ya nne ya ukuaji wa nywele).

Hatua hii ni muendelezo wa hatua ya tatu ambapo nywele hudondoka au kunyofoka. Takribani nywele 70 hadi 100 huwa katika hatua hii kila siku.

Hatua hii huchukua kati ya miezi 2 hadi 5 kukamilika kwa nywele moja kuikamilisha.

Kwa maana nyingine ni kwamba kila siku unapoteza takribani nywele 50 hadi 100 ambazo zinakuwa katika hatua hii.

Kutana nywele, kuosha au kusuka ni moja ya mambo yanazorahisisha udondokaji wa nywele hizi.

Mambo yanayoathiri ukuaji wa nywele.

Yapo mambo kadhaa ambayo huathiri ukuaji wa nywele. Baadhi ya mambo hayo ni;

Lishe bora.

Nywele kwa asili zimeundwa na dutu za protini kwa kiasi kikubwa. Kutokana na sababu hii kitu muhimu zaidi katika ukuaji wa nywele ni lishe hususa protini, madini joto ya chuma na vitamini (C na D).

Baadhi ya vyakula muhimu kwa ukuaji wa nywele ni maharage, nyama, samaki, mboga za majani.

Msongo wa mawazo.

Msongo wa mawazo ni adui wa afya yako. Si tu katika ukuaji wa nywele bali afya ya mwili kwa ujumla. Tatizo hili huathiri mfumo mzima wa homoni ambao ni dutu muhimu za ukuzaji wa nywele.

Utunzaji wa nywele.

Nywele zinapaswa kutunzwa kwa namna bora ili kukua katika afya na ubora. Utunzaji wa nywele unapaswa kuzingatia matumizi sahihi ya kemikali kulingana na aina ya nywele.

Nywele zenye mafuta, kavu au zenye tabia mchanganyiko zinapaswa kutunzwa kwa namna tofauti.

Chagua kemikali sahihi kulingana na aina za nywele zako. Ili kufanikisha hili zingatia kuchunguza kemikali ndani ya kipodozi, sabuni au shampuu unayotumia.

Vilevile epuka kutumia joto kukaushia nywele.

Sababu nyinginezo ni pamoja;
  • Kiwango cha homoni za uzazi.
  • Vipokezi vya vitamini D katika shina la nywele.
  • Magonjwa katika shina la nywele.
  • Vipokezi vya homoni ya thailoidi shina la nywele.
  • Vipokezi vya homoni za uzazi.

Hitimisho.

Ukuzaji wa nywele una changamoto nyingi. Ikiwa unadhani nywele zako zinakuwa taratibu kuliko kawaida au kukatika kuliko kwaida.

Unashauriwa kuwasiliana na mtaalamu wa afya ili kufahamu ikiwa kuna tatizo la kiafya au ni utunzaji mbovu wa nywele zako.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url