Dalili za upungufu wa mbegu za kiume, sababu, madhara yake na tiba

Kuwa na familia ni ndoto ya kila mwanaume, yawezekana hiki ndio kipimo muhimu na kikubwa cha uanaume.

Pengine umejisikia vibaya baaada ya kusoma sentensi hii hapo juu kwa vile labda haujafanikiwa kupata mtoto au unahangaika kupata mtoto lakini hakuna mafanikio. 

Ikiwa una shida ya kupata mtoto na unahangaika kila kukicha yawezekana kabisa una tatizo la upungufu wa mbegu za kiume.

Upungufu wa mbegu za kiume(manii) hutafsiriwa kama hali ambapo kiwango cha shahawa anachotoa mwanaume wakati anafika kileleni (wakati wa kujamiana) kinakuwa na idadi ndogo ya mbegu za kiume. 

Kitaalamu huitwa tatizo hili huitwa Oligospermia. 

Na kwa mujibu wa miongozo ya shirika la afya la umoja wa mataifa (WHO) kiwango kidogo cha mbegu ni pale mwanaume hukojoa shahawa zenye idadi chini ya mbegu milioni 15 kwa milimita moja ya ujazo yashahawa.

Kwa wastani kiwango cha mbegu za kiume kwa milimita 1 ya ujazo wa shahawa ni kati ya mbegu milioni 40 hadi 300

Kiwango hutofautiana kulingana na sababu nyingi ikiwamo mazingira, lishe, mitindo ya maisha na muundo wa chembe za urithi(vinasaba).

Tatizo la kuwa na kiwango kidogo cha mbegu za kiume husababisha matatizo mbalimbali ya kiafya na kijamii, kubwa zaidi ni mwanaume kuwa katika uwezekano mdogo wa kupata mtoto(kutungisha mimba).

Mbali na kushindwa kutungisha mimba, mwanaume anaweza kupata matatizo mengine kama vile kupoteza hamu ya kufanya mapenzi, upungufu wa nguvu za kiume, msongo wa mawazo na kushindwa kujiamini.

Kiwango kidogo cha mbegu za kiume haimaanishi huwezi kupata mtoto, bado una nafasi ya kupata mtoto na kuitwa baba endapo utanzingatia ushauri, miongozo na mienemdo fulani ya maisha.

Sayansi ya mbegu za kiume.

Mbegu za kiume hupitia mlolongo tata mpaka kukamilika na kuwa tayari kutolewa nje. Hatua za utengenezwaji mpaka utolewaji wa mbegu za kiume unafanyika katika korodani.

Mbegu za kiume(manii) hutengenezwa kwenye korodani na seli za sertoli, kwa msaada wa tezi za haiposalamasi na pituitari(tezi hizi zote hupatikana kwenye ubongo).

Tezi hizi huzalisha vichocheo(homoni) ambazo hupelekea seli za sertoli katika korodani kutengeneza mbegu za kiume. 

Baada ya mbegu kutengenezwa husogezwa kwenye kifuko cha dharula kiitwacho epidydimis ambako hukomaa na tayari kutolewa. 

Wakati wa kutoka hupitia mirija ya manii kisha kuingia mlija wa mkojo ambako huchanganyikana na shahawa ili kuongeza ulinzi, kurekebisha hali ya chaji ndani ya manii(PH) na kusaidia manii kusafiri kwa urahisi.

Dalili za upungufu wa mbegu za kiume

  • Upungufu wa nguvu za kiume: Ikiwemo kutopata hamu ya kufanya mapenzi, ugumu wa kusimamisha uume na kukojoa kwa shida.
  • Uvimbe au maumivu maeneo ya korodani: Dalili hii hutokea ikiwa tatizo linasababishwa na maambukizi ya magonjwa au saratani.
  • Kushindwa kutungisha mimba.
  • Kupungua kwa nywele na vinyweleo mwilini hasa usoni, kifuani, makalioni na sehemu nyinginezo.
  • Sauti kuwa nzito zaidi: Sauti nzito ni ishara kwamba utengenezwaji wa homoni za testosterone ni wa kiwango kikubwa mwilini, kiwango kikubwa cha homoni za testosterone hupunguza utengenezwaji wa manii.

Sababu za mwanaume kupata tatizo la upungufu wa mbegu za kiume

01: Matatizo katika mfumo wa utengenezaji wa manii

Tatizo linaweza kuwa ni sehemu moja au zaidi ya moja ambapo linaweza kuhusisha tezi, milija au seli za sertoli. 

Baadhi ya matatizo yanayoukumba mfumo wa utengenezwaji wa manii ni pamoja na;
  • uvimbe katika milija ya manii, hii husababisha kiwango kidogo cha manii kufika nje huku kiasi kingine kikizuiliwa au kushindwa kufika kwa wakati
  • maradhi katika mfumo mzima wa utengenezwaji wa manii au maeneo ya jirani na mfumo huu au organi zinazohusika katika utengenezaji wa manii
  • uvimbe katika korodani
  • uvimbe katika epidydimis
  • saratani
  • ugonjwa wa tezi dume
  • Maradhi ya mfumo wa mkojo kama (UTI)
  • MAYAZI(magonjwa ya zinaa) kama vile gono,UKIMWI n.k.

02: Manii kushindwa kutoka nje ya uume

Kuna wakati maradhi au maumbile yanaweza sababisha kiwango kikubwa cha manii kushindwa kufika katika uume na kuingia sehemu nyingine tofauti na uume.  

Moja ya eneo ambalo manii yanaweza kufika ni kibofu. Hali hii husababishwa na maradhi sugu kama vile;
  • kisukali, 
  • majeraha ya mfumo wa fahamu
  • ikiwa mwanaume amewahi fanyiwa upasuaji wa kibofu, tezi au milija ya manii.

03: Tatizo la seli za ulinzi za mwili kuangamiza manii

Kuna wakati mwanaume anaweza kuwa na tatizo hili ambalo kisayansi hutambuliwa kama Autoimmune disesese, ambapo seli za ulinzi hutafsiri manii kama seli hatari za mwili kimakosa na kuzishambulia.

04: Matatizo ya ukuaji wa korodani

Kuna baadhi ya wanaume korodani zao zimeshindwa kukua na kuchomoza katika vifuko vya nje hivyo zinabaki ndani ya tumbo.

Kutokana na joto kali ndani ya tumbo kiwango kikubwa cha manii kinachotengenezwa huishia kufa.

05: Matatizo ya vichocheo vya homoni mbalimbali za uzazi

Kutokuwapo kwa mlinganyo wa vichocheo(homoni) huathiri utengenezwaji wa manii.

06: Kujikunja kwa Mirija ya manii na mkojo

Majeraha au mikunjo katika mirija ya manii na milija ya mkojo huathiri usafirishwaji wa manii ambapo kiwango kidogo tu hufika katika uume kwa ajili ya kutolewa.

07: Matatizo katika chembe za urithi

Moja ya tatizo kubwa la urithi ni Klinefelters syndrome amabapo mwanaume huzaliwa na uanamke kwa kiasi kikubwa.

Mwanaume anakuwa na mbegu X ya ziada, yaani badala ya XY yeye huzaliwa na XXY, ambapo XX hupunguza uwezo wa kiume na kuongeza uanamke ndani ya mwanaume. Matatizo mengine ni kama kallmanns syndrome na kartageners syndrome.

08: Matumizi ya dawa mbalimbali

Matumizi ya aina fulani za dawa kama vile dawa za saratani(ikiwemo tiba ya mionzi), dawa za fangasi, dawa za vidonda vya tumbo, dawa za mzio na matumizi ya unga wa protein kwa ajili ya kutunisha misuli.

09: Joto kali na nguo za kubana korodani

Manii ni protini kwa asili, protini ni kemikali ambayo huaribiwa na joto kwa urahisi sana.

Kuziweka korodani katika joto la sentigredi 50 na zaidi ni hatari kwa afya ya uzazi kwa kuwa joto hili huweza kuua manii kwa urahisi.

10: Kemikali sumu

Kujiweka katika mazingira ya kemikali sumu kama vile dawa za kupuliza za kuua wadudu, rangi za kupaka, madini shaba nyekundu, madini ya zebaki na mafuta ya ndege.

Sababu nyinginezo za upungufu wa mbegu za kiume 

  • pombe na sigara
  • sonona 
  • kitambi
  • ajali kubwa
  • msongo wa mawazo.

Upungufu wa mbegu za kiume na uwezo wa kutungisha mimba.

Ni muhimu kufahamu ya kuwa wingi wa mbegu za kiume pekee si uthibitisho wa uhakika ya kwamba mwanaume anaweza kutungisha mimba.

Unaweza kuwa na kiwango kikubwa cha manii lakini ukashindwa kutungisha mimba, vilevile unaweza kuwa na kiwango kidogo cha manii na ukaweza kutungisha mimba”

Yafuatayo ni mambo ambayo huzingatiwa ili kujua iwapo mwanaume anaweza kutungisha mimba

01: Wepesi na uzito wa shahawa

Shahawa nzito ni ishara ya kuwa zina kiwango kikubwa cha manii yenye afya, hali hii huzisaidia mbegu kusafiri kwa urahisi zaidi kuliko katika shahawa nyepesi ambapo ni kiashirio kuwa kiwango cha manii ni kidogo.

02: Kiwango cha mbegu kusafiri

Uwezo wa mbegu kusafiri ni kiashirio mojawapo cha kugundua ya kwamba mwanaume ana uwezo wa kutungisha mimba au la.

kwa wastani inatakiwa walau kuanzia asilimia 40 ya mbegu ziwe na uwezo wa kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine. 

Ikiwa chini ya 40% maana yake kiwango kikubwa cha mbegu hakina uwezo wa kusafiri na hufia njiani kulingana na mazingira hatari ya mfumo wa uzazi wa mwanamke.

03: Hali ya chaji ya manii(PH)

Kwa kawaida manii huwa na kiwango cha chaji katika mzani wa PH kati ya 7.2-7.8, ikiwa ni zaidi ya hapo huashiria kuna maradhi katika mfumo wa uzazi na chini ya hapo ni ishara ya kuwa manii yamechanganyikana na dutu zisizofaa.

04: Kiwango cha manii kwa milimita ya shahawa

Kwa wastani kiwango cha manii kwa kila milimita ya ujazo ya shahawa ni kati ya milioni mbili na nusu hadi tatu. 

Chini ya hapo ni ishara kwamba kiwango cha manii katika shahawa ni kidogo na uwezo wa kutungisha mimba unakuwa ni mdogo.

Hitimisho

Kiwango kidogo cha mbegu za kiume si kipimo pekee kwamba huwezi kutungisha mimba. 

Uzito wa shahawa, PH ya shawa na uwezo wa mbegu kusafiri, kwa pamoja ndio vigezo vikubwa vya kufahamu ikiwa mwanaume anaweza kutungisha mimba au hawezi.

Ikiwa unatoa shahawa ambazo zimekizi viwango tajwa hapo juu basi hata kwa mwanaume ambae hutoa kiwango cha shahawa chenye manii kati ya milioni 20 hadi 40 bado anaweza kutungisha mimba bila shida.

Vilevile ikiwa mwanaume hutoa mbegu nyingi lakini hazikizi vigezo tajwa hapo juu anaweza pia kushindwa kutungisha mimba.

Ikiwa wewe ni mwanaume na unapata changamoto ya kushindwa kutungisha mimba basi tembelea kituo kikubwa cha afya uweze kupima na kufahamu afya ya mfumo wa uzazi ikiwa ni pamoja na kufahamu ubora wa mbegu zako.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url