Dawa za kisasa za kutibu fangasi sugu za ukeni

Tafiti za kisayansi zinaonyesha kwamba zaidi ya 75% ya wanawake hupatwa na tatizo la fangasi za ukeni walau mara moja katika maisha yao. Kuna sababu mbalimbali zinazopelekea tatizo la fangasi za ukeni kuwa la kawaida sana kwa wanawake.

Matumizi holela ya dawa za kuua bakteria na matumizi ya dawa za uzazi wa mpango na ni baadhi ya sababu zinazopelekea fangasi za ukeni kuwa ni miongoni mwa matatizo ya kawaida yanayoathiri mfumo wa uzazi wa mwananmke.

Kwa kawaida fangasi za ukeni huambatana na dalili mbalimbali kama vile kuwashwa maeneo ya nje na ndani ya uke, kutokwa na uchafu ukeni ulinaombatana na harufu kali na wakati mwingine maumivu makali ya uke.

Katika makala hii tutaangazia dawa za kisasa za kutibu tatizo la fangasi za ukeni, ili kufahamu njia za asili za kutibu fangasi soma makala hii dawa asili za kutibu fangasi ukeni.

Jinsi ya kutibu fangasi za ukeni

Moja ya changamoto kubwa ya kutibu fangasi za ukeni ni umuhimu wa fangasi hawa ambao husababisha tatizo hili.

Candida albicans, fangasi anayesababisha tatizo hili ni fangasi wa faida kwenye mwili wa binadamu hususa ni maeneo ya uke.

Wakiwa katika uke fangasi hawa husaidia kuupatia uke mlinganyo wa chaji (PH), lakini pia fangasi hawa husaidia kudhibiti kiasi cha mamilioni ya bakteria hatari wanaovamia uke kila siku.

Lakini wanapokuwa wengi zaidi ya kawaida basi husababisha athari hasi kwa afya ya uke.

Hata hivyo chini ya ushauri na uangalizi wa kitaalamu ni rahisi kwa mwanamke kudhitibi fangasi hawa katika kiwango ambacho ni rafiki katika uke.

Usitumie dawa aina tofauti za fangasi au kwa muda mrefu bila ushauri kutoka kwa mtaalamu wa afya kwa sababu kufanya hivyo kunapelekea idadi kubwa ya fangasi kufa, jambo hili linaweza kuibua matatizo mengine katika uke, Mfano maradhi ya PID na uvimbe.

Dawa za fangasi za ukeni na jinsi ya kutumia

Zipo njia na dawa mbalimbali ambazo unaweza kutumia kutibu fangasi za ukeni. Njia hizi zinaweza kuwa za kisasa au za kienyeji.

Bila kujali njia utakayochagua, dawa za kutibu fangasi za ukeni hutumiwa kwa namna kuu 3, kwanza ni kwa njia ya kupaka ukeni, njia ya kunywa na kwa njia ya kupachika ukeni.

Dawa za kisasa za kutibu fangasi ukeni

Unaweza kutumia dawa za kisasa kutibu fangasi ambazo hupatikana katika muundo wa kupaka, kumeza au kupachika ukeni.

Dawa za kisasa za kupaka na kupachika za kutibu fangasi za ukeni

Muundo huu wa dawa hutumika kutibu fangasi za kawaida za ukeni, kundi la dawa katika muundo huu ambalo limeonyesha uwezo mkubwa wa kuwaangamiza fangasi wa Candida albicans ni kundi la Azole.

Dawa maarufu kutoka katika kundi hili ni pamoja na
  • Butoconazole cream au vidonge vya kupachika yenye dozi ya 2% au 5 g.
  • Clotrimazole cream au vidonge vya kupachika yenye dozi ya 1%, 5 g, 100-mg au 500-mg
  • Miconazole cream au vidonge vya kupachika yenye dozi ya 2%, 5 g, 100-mg au 200-mg
  • Nystatin vidonge vya kupachika 100,000-U
  • Tioconazole ointment, yenye dozi ya 6.5% au 5 g
  • Terconazole cream au vidonge vya kupachika yenye dozi ya 0.4%, 5 au 0.8%
Dozi ya dawa hizi hutofautiana kulingana na ukubwa wa tatizo, kwa kawaida dozi inaweza kuwa ya siku 1, 3 au siku 7 hadi 14.

Kupata ushauri wa dozi sahihi, tafadhali wasiliana na mfamasia au daktari.

Dawa za kisasa za vidonge vya kumeza

Kwa kawaida utapewa dawa katika muundo wa vidonge ikiwa una fangasi sugu za ukeni. 

Dawa za vidonge zinazotumiwa zaidi kutibu fangasi sugu za ukeni ni Fluconazole 150-mg ambayo unaweza kupewa katika dozi tofauti kulingana na ukubwa wa tatizo lako.

Fangasi sugu za ukeni na dawa yake

Ikiwa tatizo lako la fangasi linakutokea zaidi ya mara 4 kwa mwaka na unapata shida kupona hata unapotumia dawa za kwaida za kupaka au kupachika, basi fangasi za aina hii hutajwa kama fangasi sugu.

Fangasi sugu si rahisi kuzitibu kwa sababu aina hii ya fangasi haisababishwi na Candida albicans. Candida glabrata ndio jamii ya fangasi ambayo hutajwa kusababisha fangasi sugu kwa kiasi kikubwa.

Dawa za kawaida za kutibu fangasi hazina ufanisi wa hali ya juu kwa jamii hii ya fangasi. Ili kutibu fangasi hawa Unahitaji kutumia dawa zaidi ya moja.

Inashauriwa kutumia dawa za kupaka au vidonge vya kupachika pamoja na vidonge vya kumeza kwa wakati mmoja.

Madhara ya kutumia dawa za kisasa za fangasi kiholela

Watu wengi husumbuliwa na tatizo la fangasi, huku wengi wao wakijaribu kutumia dawa bila ushauri wa kitaalamu.

Jambo hili ni hatari, kwa sababu matumizi holela ya dawa hizi husababisha usugu wa dawa na kutengenezwa tatizo la fangasi sugu.

Mbali na kutengenezwa usugu wa dawa, matumizi holela ya dawa za fangasi za ukeni hasa za kupaka na kupachika husababisha Michubuko, Miwasho na kupungua kwa maeneo ya uke.

Hitimisho

Fangasi za ukeni ni tatizo ambalo linawaathiri wanawake wengi. Kabla ya kuamua kutumia dawa hakikisha unafahamu sababu ambayo imepelekea tatizo lako.

Kufahamu sababu ni muhimu katika kuchagua njia na dawa sahihi ya kutibu tatizo lako.

Kumbuka matumizi ya dawa za kutibu fangasi hayawezi kuwa na mafanikio ikiwa sababu iliyopelekea kupata tatizo bado haujaitafutia ufumbuzi.

Mbali na sababu iliyopelekea tatizo, mambo mengine ambayo ni muhimu kuzingatia wakati wa kutibu fangasi ni usafi binafsi, kula vizuri, safisha mwili wako hasa unapotokwa na jasho, ruhusu uke kufikiwa na hewa safi ya oksijeni na epuka nguo za kubana.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url