Sababu za kichefuchefu na kutapika kwa mjamzito na tiba yake

Kichefuchefu na kutapika ni miongoni mwa hali za kawaida sana kwa mjamzito hasa miezi miezi 3 ya mwanzo ya ujauzito. 

Hali hii inatokana na mabadiliko makubwa ya mwili ambayo hutokea kwa mwanamke baada ya ujauzito.

Katika makala hii tutaangazia chanzo, dalili, tiba na athari za hali hii kwa mjamzito na mtoto aliye tumboni kabla na baada ya kuzaliwa.

Kichefuchefu na kutapika kwa wajawazito

Takribani asilimia 70 hadi 80 ya wanawake wote wanaopata ujauzito hupatwa na hali hii ya kichefuchefu na kutapika.

Hali hii pia hujulikana kwa jina la “ugonjwa wa asubuhi wa wajawazito” kwa sababu hali hii mara nyingi hutokea nyakati za asubuhi, ingawa inaweza kutokea muda wowote.

Hali hii hutokea zaidi kati ya mwezi wa kwanza hadi wa nne wa ujauzito.

Mara nyingi hali hii hupungua ama kuisha baada ya mwezi wa 5 wa ujauzito, ingawa kwa baadhi ya wanawake hali hii huweza kuendelea hadi kipindi cha kujifungua.

Kutapika na kichefuchefu kupita kawaida

Pamoja na kwamba hali hii ni ya kawaida na kwa sehemu kubwa ni ya lazima kwa mjamzito, kuna wakati hali hii hupita kawaida na kusababisha tatizo lijulikanalo kama Hyperemesis gravidarum.

Hyperemesis gravidarum ni hali ya kichefuchefu na kutapika kupita kawaida ambapo mjamzito hutapika zaidi ya mara 3 kwa siku kwa nyakati tofauti.

Tatizo hili huathiri kati ya 0.2-2% ya wajawazito. Ikiwa tatizo hili halitatibiwa au kuthibitiwa kwa wakatilinaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtoto na mama.

Kwa wajawazito, kichefuchefu na kutapika kupita kiasi husababisha mjamzito kushindwa kula na hata akiweza kula ni rahisi chakula kupotea kwa sababu anakitapika.

Kuathirika kwa ulaji kwa mjamzito kutokana na tatizo hili hupelekea mjamzito kukumbwa na matatizo ya upungufu wa lishe ambayo huathiri ukuaji wa mtoto.

Moja ya tatizo kubwa kwa watoto ambalo huweza kusababishwa na kichefuchefu na kutapika kupita kiasi ni mtindio wa ubongo, ambalo ni matokeo ya upungufu wa vitamini B1.

Upungufu wa vitamini B1 kwa mjamzito husababishwa na mjamzito kushindwa kula chakula cha kutosha kutokana na tatizo hili.

Matatizo mengine yanayoweza kusababishwa na kutapika na kichefuchefu kupita kawaida kwa mjamzito ni:
  • Mara nyingi tatizo hili huambatana na ujauzito wenye watoto zaidi ya 1.
  • Maradhi ya saratani kwa mama hasa saratani katika mfumo wa uzazi.
  • Kushindwa kujifungua.
  • Kushindwa kutengenezwa kwa plasenta.
  • Kuzaa mtoto njiti.
  • Matatizo mbalimbali ya ukuaji ya mtoto, mfano Down syndrome.
  • Kuzaa mtoto mwenye matatizo ya mlundikano wa maji sehemu mbalimbali za mwili, mfano watoto wenye vichwa vikubwa.

Athari za kchefuchefu na kutapika kwa mjamzito

Katika hali ya kawaida kichefuchefu na kutapika kwa mjamzito vina faida kadhaa za kiafya kwa mama na mtoto ikiwemo:
  • Kupunguza uwezekano wa mimba kuharibika.
  • Husaidia mtoto kuzaliwa na uzito unaotakiwa.
  • Kupunguza uwezekano wa kuzaa mtoto njiti.
  • Ni ishara ya mojawapo ya ujauzito wenye mapacha au watoto zaidi zaidi.
Hata hivyo hali ya kichefuchefu na kutapika kwa mjamzito inaweza kuambatana na athari hasi katika nyanja mbalimbali za kibaolojia, kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

Baadhi ya athari hasi ambazo zinaweza kuandamana na hali hii kwa mjamzito ni pamoja na:
  • Huweza kusababisha shinikizo la damu.
  • Hali hii huweza kuchagiza kifafa cha mimba.
  • Huweza kumsababishia mjamzito sonona.
  • Mjamzito kukosa raha.
  • Kupungua kwa utendaji kazi za nyumbani na ofisini.
  • Hali hii huweza kuathiri malezi ya watoto wengine.
  • Matatizo ya kisaiolojia

Vihatarishi vya tatizo hili kwa wajawazito.

Yapo mambo kadhaa ambayo huchagiza mjamzito kuathiriwa na hali hii ya kichefuchefu na kutapika, baadhi ya mambo hayo ni;
  • Kula vyakula vyenye mafuta mengi.
  • Uzito mdogo wa mama.
  • Historia ya familia.
Tafiti nyingi zinaonye jinsia kama kisababishi cha tatizo, ambapo inatajwa kuwa mimba ya mtoto wa kike huambatana na tatizo hili kwa kiasi kikubwa kuliko mimba ya mtoto wa kiume.

Sababu za kichefuchefu na kutapika kwa mjamzito

Licha ya kuwa hakuna uthibitisho wa moja kwa moja juu ya chanzo cha hali hii wakati wa ujauzito, kuna sababu kadhaa zinadhaniwa kuchochea hali hii kwa wajawazito.

Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na:

01: Mabadiliko ya homoni mwilini

Homoni ya human chorionic gonadatropin (hCG) ndio hudhaniwa kuwa sababu mojawapo kuu ya hali hii.

Homoni hii hutengenezwa mara baada ya siku 7 hadi 14 za ujauzito. Kiwango cha homoni hii huwa kikubwa miezi 4 ya awali ya ujauzito na baadae huanza kupungua.

Kwa vile katika kipindi hiki cha mwezi 1 hadi wa 5 wa ujauzito tatizo la kichefuchefu na kutapika huwa katika kiwango cha juu.

Inadhaniwa kuwa homoni hii ina mchango mkubwa katika kusababisha hali hii ya kichefuchefu na kutapika.

Vilevile homoni za estrogen na progesterone zinatajwa kuchangia hali hii kwa sababu katika kipindi cha ujauzito homoni hizi hutawala mwilini.

Kutokana na kwamba wanawake wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango hushambuliwa sana na hali basi uwepo wa homoni hizi mwilini kwa mjamzito huchangia tatizo hili.

Kwa sababu dawa hizi za uzazi wa mpango kwa sehemu kubwa zimetengenezwa kwa homoni hizi.

Pia homoni za progesterone na estrogen husababisha tatizo hili kutokana na uwezo wake wa kupunguza mnyumbuliko wa misuli laini mbalimbali ya mwilinini ikiwemo misuli katika mfumo wa chakula.

Jambo hili hupelekea kuchelewesha mmeng’enyo. Kuchelewa kwa mmeng’enyo wa chakula ni moja ya sababu zinazoweza kusababisha mtu kutapika.

Mbali na homoni, vilevile dutu za prostaglandini E2 pia zinatajwa kusababisha hali hii ya kichefuchefu na kutapika kwa sababu husababisha misuli katika mfumo wa chakula kupunguza mjongeo.

02: Bacteria wa Helicobacter pylori

Wajawazito ambao wana maambukizi ya bakteria wa H. pylori wameonyesha kuathiriwa zaidi na hali hii kuliko wale wasio na maambukizi.

H. pylori ni bacteria huyu husababisha ugonjwa wa vidonda vya tumbo. Kwa hivyo wajawazito wenye tatizo la vidonda vya tumbo kwa sehemu kubwa huathiriwa zaidi na hali hii ya kichefuchefu na kutapika.

Ni rahisi kwa mjamzito kupata maamukizi ya bakteria huyu wa H. pylori kutokana na mabadiliko makubwa hali ya chaji ambayo husababishwa na mabadiliko ya homoni.

Mabadiliko ya hali ya chaji tumboni yanatoa mazingira rafiki kwa bakteria huyu kukua na kuzaliana kwa wingi.

03: Kupungua kwa mjongeo wa misuli ya mfumo wa chakula

Kupungua kwa mjongeo wa misuli inayozunguka mfumo wa chakula kunasababisha mmeng’enyo wa chakula kuchelewa na chakula kutumia muda mwingi katika mfumo huu.

Uwepo wa chakula katika mfumo wa chakula kwa muda mrefu bila kumeng’enywa huchangia kwa kiasi kikubwa tatizo la kutapika na kichefuchefu.

Kwa mjamzito mambo kadhaa husababisha kupungua kwa mjongeo huu, baadhi ya mambo hayo ni:
  • Kiungulia.
  • Kucheua mara kwa mara.
  • Kiwango kikubwa cha homoni za progesterone.
  • Matumizi ya vyakula vya mafuta kwa kiasi kikubwa.

04: Sababu za kijamii na kisaikolojia

Sababu mbalimbali za kisaikolojia zinaweza kuchangia hali hii ya kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuna mambo kadhaa ya kijamii na kisaikolojia ambayo yanaweza kumsababishia mjamzito tatizo hili la kichefuchefu na kutapika.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na:
  • Mimba zisizotarajiwa.
  • Kukataliwa na jamii.
  • Msongo wa mawazo.
  • Umasikini.
  • Kukomaa kiakili na kujitambua wakati wa ujauzito.
  • Migogoro ya kijamii.

Dalili na viashiria vya tatizo hili kwa wajawazito

Licha ya kuitwa ugonjwa wa asubuhi kwa wajawazito, utafiti unaonyesha ni 2% tu ya wajawazito ndio ambao hali hii huwatokea asubuhi pekee.

Kundi kubwa la wajawazito limeonyesha kushambuliwa na hali hii wakati wowote bila kujali majira ya muda.

Hali hii huanza kujitokeza kuanzia wiki ya 4 ya ujauzito na kushika kasi kati ya wiki ya 10 hadi 16.

Kabla ya tatizo hili kuna mambo kadhaa na viashiria ambavyo hujitokeza au kuwepo kabla na vinaweza kutumiwa kama ishara ya kwamba tatizo hili la kichefuchefu na kutapika litakusumbua.

Baadhi ya dalili na viashiria hivyo ni:
  • Maradhi ya vidonda vya tumbo.
  • Kiungulia na kichefuchefu.
  • Homa ya ini.
  • Makovu au vidonda katika utumbo mdogo wa chakula.
  • Uvimbe katika kibofu cha mkojo.
  • Mawe katika figo.
  • Maumivu ya kichwa na kipandauso.
Ikiwa una tatizo lolote miongoni mwa baadhi ya matatizo yaliyoorodheshwa hapo juu basi kuna uwezekano mkubwa ukaathiriwa na tatizo hili la kichefuchefu na kutapika.

Tiba ya kichefuchefu na kutapika kwa mjamzito

Tatizo la kichefuchefu kwa mjamzito ni la kawaida sana na kwa sehemu kubwa halihitaji dharula ya kitabibu.

Ikiwa mjamzito anaweza kuvumilia hali hii basi anashauriwa kutotumia dawa za aina yeyote isipokuwa kuboresha lishe.

Wakati mwingine tatizo hili huweza kuwa kubwa kiasi cha kudhoofisha shughuli za kiutendaji kila siku za mjamzito.

Vilevile linaweza kuwa kubwa kiasi cha kuathiri au kuhatarisha afya ya mama na mtoto. Katika hali hii mjamzito anashauriwa kutumia njia zifuatazo katika kukabiliana na tatizo hi:

Njia za asili za kutibu kichefuchefu na kutapika kwa wajawazito

Lengo la dawa na njia hizi za asili ni kupunguza na kuzuia tatizo. Baadhi ya njia za kienyeji za kutibu tatizo hili ni pamoja na:

01: Zingatia lishe bora

Hii inapaswa kuwa chaguo nambari moja miongoni mwa njia za kupambana na hali hii. Mjamzito anashauriwa kutokula chakula kingi kwa wakati mmoja.

Mjamzito anashauriwa kutumia chakula kiasi kidogo mara nyingi zaidi kwa siku kuliko chakula kingi kwa mara moja.

Vilevile, mjamzito anatakiwa kuepuka vyakula vyenye wanga na mafuta kwa kiasi kikubwa na kutumia zaidi vyakula vyenye protini kwa wingi.

Mjamzito anashauriwa kutumia vyakula vifuatavyo kwa wingi zaidi:
  • Maji yaliyochanganywa na chumvi kidogo walau mara moja kwa siku.
  • Soya.
  • Ndizi.
  • Nyama ya kuku
Vyakula hivi vina kiwango kikubwa cha Vitamini B6 ambayo husaidia mwili katika mambo mbalimbali ikiwamo kuimarisha utendaji kazi wa mmeng’enyo wa chakula.

02: Pata msaada wa kisaikolojia

Ikiwa mjamzito anasumbuliwa na matatizo mbalimbali ya kijamii ambayo yanaathiri saikolojia kama vile migogoro, kukataliwa na kutengwa, basi ni vyema kupata ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa masuala ya akili na saikolojia.

03: Matumizi ya tangawizi

Pengine hii ndio tiba pekee yenye ufanisi wa hali ya juu isiyo na madhara makubwa kwa mjamzito na mtoto.

Matumizi ya tangawizi kwa mjamzito yana msaada mkubwa katika kupunguza tatizo la kichefuchefu na kutapika.

Uwezo wa tangawizi kuongeza mjongeo wa misuli inayounda mfumo wa chakula ndio kunafanya tangawizi kuwa chaguo la kwanza miongoni mwa dawa salama za kutibu tatizo hili kwa mjamzito.

04: Matumizi ya njia na dawa za kisasa za kutibu tatizo hili

Kuna dawa za aina nyingi za kisasa za kutibu tatizo hili kwa wajawazito. 

Nyingi ya dawa hizi huambatana na madhara kadhaa ya kiafya kwa mama na mtoto hasa zikitumiwa bila uangalizi wa mtaalamu wa dawa (mfamasia).

Baadhi ya dawa hizi ni kama zifuatavyo.
  • Pyridoxine-doxylamine.
  • Phenothiazines.
  • Chlorpromazine.
  • Aluminum na calcium.
  • Metoclopramide.
  • Methylprednisolone
  • Meclizine.
  • Ondansetron.
  • Droperidol.
Hizi ni baadhi ya dawa ambazo hutumika kukabiliana na tatizo hili kwa wajawazito. Dawa hizi hufanya kazi kwa namna tofauti kwa hivyo matumizi yake yanategemea zaidi hitaji la mgonjwa.

Baadhi ya dawa hizi pia hazitibu tatizo moja kwa moja bali hutibu matatizo ambayo hudhaniwa kuwa ni chanzo cha tatizo hili la kichefuchefu na kutapika.

Onyo! 
Usitumie dawa hizi bila ushauri wa kitaalamu kwa sababu zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya mama na mtoto.
Kwa wagonjwa ambao tiba za lishe na dawa hazitasaidia basi hupatiwa tiba ya chakula kwa njia ya sindano na mipira maalumu.

Na ikiwa tatizo litakuwa kubwa kupita kawaida, pendekezo la kutoa mimba huwa ni moja ya mtazamo tiba unaoshauriwa ili kunusuru afya ya mama, vilevile afya ya mtoto kabla na baada ya kuzaliwa.

Hitimisho

Tatizo la kutapika na kichefuchefu ni miongoni mwa matatizo ya kawaida ambayo huibuka kipindi cha ujauzito na huaathiri wanawake wengi.

Lishe bora kipindi cha ujauzito na kupunguza msongo wa mawazo ni miongoni mwa tiba zinazopendekezwa kama chaguo la kwanza.

Epuka matumizi ya dawa za kisasa katika kipindi chote cha ujauzito. Tumia dawa hizi pale tu inapobidi kwa vile dawa nyindi si salama kipindi cha ujauzito.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url