Faida za bamia mwili na jinsi ya kutumia

Wimbi la matumizi ya mitishamba linazidi kushamiri duniani kote kila kukicha. Moja ya sababu ni tatizo la usugu wa bakteria dhidi ya dawa za kisasa. Katika makala hii tutaangazia faida za bamia katika kutibu magonjwa mbalimbali.

Bamia ni chakula kundi la mbogamboga ambalo lina virutubisho vingi vya mwili, vilevile ina uwezo wa kutibu maradhi kadhaa ya mwili.

Kitaalamu bamia hujulikana kwa jina la Abelmoschus esculentus. Inaaminika mmea huu asili yake ni Ethiopia lakini kwa sasa unastawi karibu maeneo yote ya ukanda wa kitropiki (maeneo ya mvua nyingi na joto).

Sehemu mbalimbali za mmea huu zina kiwango kikubwa cha kemikali tiba ambazo zina uwezo wa kutibu magonjwa kadhaa yakiwemo kisukari, magonjwa ya ini na magonjwa ya bakteria.

Vilevile bamia ina aina ya sukari ambayo hutumiwa viwandani kuongeza radha kwenye baadhi ya bidhaa na vyakula hususa ni rambaramba na mikate.

Ndani ya bamia kuna nini?

Faida za bamia kiafya hutegemea zaidi na hatua ya ukuaji ambao mmea huu umefikia. 

Kemikali tiba na lishe ndani ya bamia hutofautiana kadri ya umri na hatua za ukuaji wa mmea huu.

Kemikali lishe ndani ya bamia.

Bamia ni moja ya mimea michache ambayo ina kemikali lishe za mafuta ya omega-3 na omega-6. 

Aina hii ya mafuta tunaipata kwa wingi katika vyakula vya baharini na ni moja ya kemikali lishe muhimu zaidi kwa watoto.

Mbali na mafuta, bamia ina kemikali lishe kadhaa kama vile Protini, ufumwele, sukari, wanga na nishati, β-carotene, riboflavin, na vitamin B changamano.

Vilevile bamia ni chanzo kizuri cha madini joto ya Potassium, Calcium, Phosphorus na Magnesium. Pia kuna madini joto ya Shaba, Selenium, Zinc, Sodium na madini joto ya chuma.

Faida za bamia mwilini

#1: Bamia hutumika kutibu tatizo la kisukari.

Mmea huu umethibitika kisayansi kuwa na uwezo mkubwa wa kutibu tatizo la kisukari aina ya 2.

Matumizi ya mlenda wa bamia changa ya kila siku yameonyesha matokeo mazuri kwa wagonjwa wa kisukari aina ya 2.

Hakuna maelezo ya moja kwa moja ya kitaalamu ni jinsi gani bamia hufanikisha hili bali kemikali tiba za quercetin, quercetin-3′-O-glucoside, isoquercitrin, na hyperoside ndio zinatajwa vinara wa kufanikisha hili

Kemikali tiba za Oligomeric proanthocyanidins ndani ya bamia zinasaidia kuzuia utendaji kazi wa kichocheo cha α-glucosidase na α-amylase.

Vichocheo hivi husababisha kutengenezwa kwa sukari aina ya glucose kwa wingi mwilini. Hivyo kuzuia kwa vichocheo hivi huleta nafuu kubwa kwa wagonjwa kwa kisukari.

#2: Kupunguza sumu za mwili.

Mbegu za bamia changa zina kiwango kikubwa cha kemikali za polyphenols na Flavonoids.

Kemikali za polyphenols husaidia kuondoa sumu mbalimbali za mwili kwa kudhibiti ongezeko la taka zinazotokana na kuunguzwa kwa mafuta mwilini.

Vilevile husaidia kuongeza kiwango cha vichocheo vya superoxide dismutase na glutathione peroxidase ambavyo husaidia kupunguzwa kwa kemikali sumu za mwili.

Wakati kemikali za Flavonoids hupunguza sumu za mwili kwa kuungana na chaji huru kadhaa za mwili ambazo ni hatari kwa uhai wa seli.

Baadhi ya Flavonoids zinazopatikana kwa wingi ndani ya bamia changa ni quercetin-3-O-gentiobioside, quercetin-3-O-glucoside (isoquercitrin), rutin, a quercetin derivative, protocatechuic acid, na flavanoids kundi la catechin.

#3: Kutibu na kutoa ulinzi dhidi ya saratani.

Saratani ni ugonjwa wa pili unaosababisha vifo vyote duniani. Mpaka sasa kuna dawa za chache za kutibu saratani ambazo pia zimeanza kukumbana na usugu wa mwitikio katika ufanyaji kazi wake.

Tiba nyingi za saratani zinaambatana na madhara makubwa ya kiafya jambo hili linafanya mitishamba kuwa chaguo sahihi na salama zaidi katika kupambana na kuzuia tatizo.

Kiwango kikubwa cha flavanoids na na protini za lectins na pectins ndani ya bamia kinafanya chakula hiki kutumika kama sehemu ya tiba na kinga dhidi ya maradhi ya saratani mbalimbali za mwili.

Maua, majani, mbegu na maganda ya bamia changa yote yanatajwa kuwa na kiwango kikubwa cha flavanoids.

#4; Kuimarisha kinga ya mwili.

Kinga ya mwili ndio nguzo kuu ya ulinzi wa mwili dhidi ya hatari na maradhi mbalimbali ya mwili. Kuimarisha kinga ya mwili ni njia pekee ya kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mwili.

Bamia ina kiwango kikubwa cha kemikali za protini aina ya lectins na vitamini C.

Kemikali hizi zimethibitika kuwa na uwezo wa kuimarisha kinga za mwili kwa namna mbalimbali ikiwemo, kudhibiti uvimbe katika mwili na kuchagiza mwitikio na ufanyaji kazi wa dutu za ulinzi mwilini.

#5: Huimarisha afya na ujazo wa mifupa.

Kemikali za Calcium, Vitamin K na C husaidia kutengenezwa na kuimarika kwa mifupa.

Bamia ni chakula muhimu kwa watu wenye ujazo mkubwa wa mifupa hasa wanawake ambao wana uzito mdogo na wanasumbuliwa na changamoto ya kutopata hedhi.

#6: Kuimarisha afya ya macho.

Vitamin A na viondoa sumu vya mwili (viantioksideshaji) vya lutein, xanthein, and carotenes husaidia kuimarisha afya ya macho.

#7: Kutibu vidonda vya tumbo.

Kemikali za Rhamnogalacturonan ndani ya bamia husaidia kuzuia kujishikiza kwa bakteria wa H. pylori ambao husababisha vidonda vya tumbo.

#8: Kuondoa uchovu.

Kemikali za Polyphenols na flavonoids ambazo hupatikana katika mbegu za bamia changa husaidia kuondoa uchovu wa mwili.

Matumizi ya mlenda ni moja ya tiba bora za asili za kuondoa uchovu.

#9: Chanzo bora cha lishe kwa wajawazito.

Wanawake wenye mimba bamia ni moja ya vyakula vya lazima kwa vile ina kiwango kikubwa cha virutubisho muhimu kwa mjamzito vya Vitamin A, vitamins (B1, B2, B6) na vitamin C. 

Vilevile kuna kiwango kidogo cha zinc, calcium, folic acid, na vyakula vya nyuzinyuzi.

#10: Faida nyinginezo za bamia ni pamoja na;

  • Kupunguza kiwango cha rehemu mwilini
  • Kuimarisha mfumo wa fahamu
  • Kusaidia kupata haja laini
  • Kutibu magonjwa ya moyo
  • Kusafisha ini

Ni sehemu ipi ya mmea wa bamia hutumika kama tiba.

Majani, mbegu, maganda na maua vyote hutumika kama tiba. Sehemu hizi za mmea huu zinaweza kupatikana katika namna ya;
  • Unga.
  • Mbogamboga.
  • Mafuta ya mbegu za bamia.

Jinsi ya kuandaa bamia kama tiba.

Ili kunufaika na faida za bamia, maandalizi yanapaswa kuwa kama ifuatavyo:

Kwa kuchemsha.

Pika bamia changa zisizokomaa sana kwa kuchemsha katika maji safi na salama kwa muda usiozidi dakika 2 hadi 5.

Kisha tumia kwa kunywa mchanganyiko wake kadri uwezavyo. Unaweza kuchanganya na kitunguu, nyanya au magadi ili kuongeza radha.

Tumia kwa kutafuana zikiwa mbichi.

Unaweza kutumia bamia kwa kutafuna zikiwa mbichi ikiwa unaweza kufanya hivyo au kuziponda kabla ya kula.

Tumia unga wa bamia.

Ikiwa huna uwezo wa kupata bamia mbichi, unaweza kununua unga wa bamia ambao umesagwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya matumizi.

Tumia unga wa bamia kwa kutengeneza juisi au kama kiongeza radha katika chakula kingine.

Kwa watu wenye maradhi ya kisukali aina ya 2 matumizi ya bamia 3 hadi 5 au kijiko 1 hadi 2 kwa siku husaidia kupunguza nafuu ya tatizo hili.

Kumbuka kwa wagonjwa wa kisukari aina ya 2 matumizi ya bamia pekee si suhulisho la tatizo.

Ikiwa unatamani kuachana na dawa za kisasa na kujikita kwenye mitishamba na lishe basi hakikisha unawasiliana na mtaalamu wa afya kabla ya kuacha kutumia dawa za kisasa za kisukari.

Hitimisho.

Hizi ni baadhi ya faida za bamia katika kutibu na kupambana na magonjwa mbalimbali ya mwili kulingana na tafiti za hivi karibuni juu ya mmea huu.

Kisukari aina ya 2 ndio ugonjwa unaotajwa kuthibitiwa kwa kiwango kikubwa na matumizi ya bamia.

Mmea huu unaweza kuwa na faida zaidi ya hizi zilidhoorodheshwa hapa. Ili kunufaika na faida za mmea huu weka mazoea ya kutumia bamia kama sehemu ya chakula cha kawaida cha kila siku.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url