Vidonda vya tumbo husababishwa na nini?

Ikiwa unapata maumivu makali ya tumbo mara kwa mara, kuhisi kutapika, kupungua uzito, kupoteza hamu ya chakula au kiungulia cha mara kwa mara, basi yawezekana una tatizo la vidonda vya tumbo.

Vidonda vya tumbo ni tatizo linalotokea katika mfumo wa chakula ambapo vipele, uvimbe wenye michubuko au michubuko isiyoambatana na vipele wala uvimbe hujitokeza katika kuta za mfumo wa chakula.

Vidonda vya tumbo huweza kujitokeza katika sehemu yoyote ya mfumo wa chakula yaani katika koo la chakula(hasa sehemu ya chini ya koo), tumboni na katika utumbo(sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo).

Nukuu Muhimu!

Vidonda vya tumbo humpata mtu yeyote bila kujali umri, rangi, jinsia au asili yake 
Zaidi ya watu milioni mia saba duniani kote husumbuliwa na tatizo la vidonda vya tumbo. 
Kwa sehemu kubwa Vidonda vya tumbo husababishwa na ratiba ya chakula isiyoeleweka, bakteria au matumizi ya dawa za kutuliza maumivu. 
Vidonda vya tumbo huweza kutibiwa na kupona kabisa. 
X-ray, damu na kinyesi, chochote au vyote vinaweza kutumika kugundua ukubwa wa tatizo la vidonda vya tumbo.

Mfumo wa chakula na tatizo la vidonda vya tumbo.

Mfumo wa chakula umeumbwa katika namna tata na ya kipekee ili kuhakikisha kazi ya kumeng’enya na kufyonzwa kwa chakula katika seli za mwili inafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu. 

Ili kufanikisha hili mfumo huu umeumbwa na tezi na ogani mbalimbali ambazo huzalisha kemikali(vimeng’enyo) zinazosaidia kazi ya mmeng’enyo wa chakula kufanyika kwa ufanisi. 

Sehemu kubwa ya vimeng’enyo hivi hufanya kazi vizuri katika hali ya tindikali. Katika kuhakikisha kunakuwa na hali ya tindikali katika baadhi ya maeneo ya mfumo wa chakula, mwili huzalisha tindikali ijulikanayo kama Hydrochloric acid .

Tindikali hii huzalishwa katika nyongo na kumiminwa katika mfumo wa chakula pale inapohitajika, katika vipimo vya hali ya tindikali au magadi tindikali hii hutajwa kuwa na nguvu ya PH 3.5.

PH 3.5 ni kiwango kikubwa cha nguvu ya tindikali, ikiwa tindikali yenye nguvu hii itaufikia mwili bila kuwepo ulinzi basi inaweza kusababisha madhara makubwa katika mwili.

Tindikali hii ndio sababu kuu ya tatizo la vidonda vya tumbo ikiwa haitadhibitiwa kikamilifu. 

Ili kuzuia hatari ya kemikali hii mfumo wa chakula una tezi maalumu ambazo huzalisha ute kwa ajili ya ulinzi wa kuta za mfumo wa chakula dhidi ya mashambulizi ya moja kwa moja ya vidudu na tindikali.

Endapo ute huu utateteleka basi ulinzi wa kuta za mfumo wa chakula pia utakuwa duni kupelekea tindikali hizi kuzifikia kuta za mfumo wa chakula na kuziharibu kwa kuziiunguza na kusababisha vidonda ama michubuko.

Vidonda vya tumbo husababishwa na nini?

Zipo sababu kuu tatu zinazoelezea ni kwa namna gani mtu anaweza kupata tatizo la vidonda vya tumbo.

Vidonda vya tumbo huweza kusababishwa na mambo yafuatayo:
  • Maambukizi ya bakteria aina ya H.Pylori
  • Matumizi ya mara kwa mara ya dawa za kutuliza maumivu hasa kundi la dawa zijulikanazo kama NSAIDs, mfano Paracetamol na Diclofenac
  • Kutokuwa na ratiba sahihi ya chakula.

01: Maambukizi ya Bakteria na vidonda vya tumbo

Ni katika miaka ya 2000 ndipo wanasayansi waligundua kwamba bakteria anaetambulika kwa jina la Helicobacter Pylori anaweza kusababisha tatizo la vidonda vya tumbo.

Bakteria huyu ambaye kwa asili huishi katika mwili wa binadamu na vilevile hupatikana kwa wanyama wengine kama vile Ng'ombe. 

Bakteria huyu anaweza kusambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia majimaji ya mwili, vilevile huweza kusambaa kupitia chakula hasa kutoka katika wanyama kwenda kwa binadamu.

Maziwa yasiyochemshwa vizuri hutajwa kama sababu nambari moja ya usambaaji wa bacteria huyu kutoka katika wanyama kwenda kwa binadamu.

Akiwa katika tumbo au sehemu yoyote ya mfumo wa chakula, bakteria huyu huzalisha kemikali aina ya Urease.

Kemikali hii ina hali ya magadi, utengenezwaji wake unapunguza hali ya tindikali katika mfumo wa chakula hususa ni tumboni.

Hali hii ya kupungua kwa tindikali katika mfumo wa chakula kunapelekea mwili kuzalisha tindikali ya HCL kwa wingi ili kuleta mlinganyo wa hali ya magadi na tindikali tumboni. 

Jambo hili hupelekea kiwango kikubwa cha tindikali kuzalishwa kuliko kile ambacho ute unaweza kuhimili, matokeo yake tindikali hii hufikia kuta za tumbo na kuziaharibu.

Lakini pia uwepo wa bakteria hawa huufanya mwili kuitikia kwa kutengeneza uvimbe kama sehemu ya mapambano ya mwili na vimelea. 

Uvimbe huu hujitokeza kwa juu na kuwa rahisi Zaidi kufikiwa na tindikali hii na kuharibiwa.

02: Matumizi ya dawa za maumivu na vidonda vya tumbo.

Matumizi ya dawa ya kundi la dawa za kutuliza maumivu na homa lijulikanalo kama Non-steroidal anti-inflammatory drugs (NSAIDS) hutajwa kuwa moja ya chanzo kikubwa cha tatizo la vidonda vya tumbo.

Dawa hizi hupunguza uwezo wa seli za mwili kuzalisha ute ambao ndio ulinzi mkuu wa tumbo dhidi ya tindikali ya HCL. 

Hali hii hufanya tumbo kuwa katika hatari ya kushambuliwa na tindikali kwa vile kinga yake(ute) hupungua na kuzalishwa kwa kiwango kidogo. 

Pia dawa hizi hupunguza kiwango cha damu kinachofika katika tumbo, hii huzifanya seli za tumbo kukosa virutubisho vya kutosha kwa hivyo utendaji kazi wake pia hudhoofu.

03: Kutokuwa na mpangilio bora wa chakula

Mwili wa binadamu una tabia ya kukariri utendaji kazi wake, kitaalamu mwili huchukua siku saba kuzoea jambo na siku 21 kulifanya jambo kuwa kama tabia. 

Vivyo hivyo ratiba ya chakula inayofanana kwa siku saba mfululizo huufanya mwili kuzoea na kukariri muda na aina ya chakula, lakini kama ratiba hiyo itaenda kwa siku 21 basi mwili hufanya ratiba hiyo kama tabia.

Hali hii husababisha mwili kuzalisha kemikali zote muhimu kila ifikapo muda ambao umezoea kula chakula kwa ajili ya kupokea na kumeng’enya chakula.

Moja ya kemikali zinazozalishwa kwa wingi ni tindikali hii ya HCl, ikiwa kemikali hii itazalishwa kwa wingi wakati tumboni hakuna chakula basi itapelekea tumbo kuharibiwa au kumeng’enywa.

04: Matumizi ya maziwa na Vidonda vya tumbo.

Ng’ombe ni moja ya wanyama ambao hutumiwa sana na bakteria huyu wa H.pylori kama makazi yake.

Bakteria huyu hutolewa mwilini kwa ng’ombe kupitia maziwa. Kwa hivyo matumizi ya maziwa yaliyochemshwa chini ya kiwango inaweza sababisha maradhi ya vidonda vya tumbo.

Hitimisho

Vidonda vya tumbo ni tatizo linanowasumbua watu wengi. Tatizo hili linaweza kushambulia sehemu yeyote  ya mfumo wa chakula lakini tumbo ndio sehemu ambayo huathiriwa zaidi.

Mbali na sababu zilizotajwa hapo juu vilevile uvutaji, ulevi wa kupita kawaida, sonona, msongo wa mawazo, matatizo ya urithi katika vinasaba na  mengine mengi, vyote hivi huweza kusababisha tatizo hili.

Tiba ya vidonda vya tumbo inategemea zaidi sababu iliyopelekea tatizo kujitokeza. Ni vizuri kufahamu tatizo lako la vidonda vya tumbo linesababishwa na nini kabla ya kuchukua hatua ya matibabu.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url