Magonjwa hatari yanayosababisha mwanamke kushindwa kupata mimba

Wanawake wengi wanahangaika kupata watoto bila mafanikio. 

Tatizo hili la kutoshika mimba linazidi kushamili na linawaathiri wanawake kwa namna tofauti kama ifuatavyo;
  • Kuna wanawake ambao hawawezi kabisa kushika mimba
  • wapo ambao wanashika mimba lakini mimba zinashindwa kukua
  • wengine wanashika mimba lakini zinaharibika katika hatua za awali.
Zipo sababu nyingi zinazopelekea tatizo hili la wanawake kushindwa kupata mimba, lakini magonjwa katika mfumo wa uzazi wa mwanamke ndio sababu kuu ya wanawake kushindwa kushika mimba.

Magonjwa katika mfumo wa uzazi wa mwanamke yanaweza kuathiri uwezo wa mwanamke kushika mimba au kuathiri hatua mbalimbali za ukuaji wa mimba kwa namna zifuatazo;
  • Kutengenezwa kwa mayai yasiyokuwa na uwezo wa kuchavushwa au kurutubishwa
  • Hitilafu au kuharibika kwa milija ya falopia, katika milija hii ndipo urutubishwaji wa yai hutokea
  • Athari katika mfuko wa uzazi ambazo huzuia yai lilitengenezwa kujishikiza katika kuta za mfuko wa uzazi na kutengeneza placenta
  • Matatizo katika mlango wa kizazi ambayo yanaweza kusababisha msukumo mkubwa ndani ya mfuko wa uzazi, msukumo ambao unaweza kusababisha yai lililorutubishwa kutolewa nje kabla ya kutengeneza placenta

Kwa sehemu kubwa magonjwa haya yanaweza kutibiwa na kupona. 

Baadhi ya magonjwa haya hayana tiba, hivyo zinahitajika njia na mbinu mbadala za kisasa ili kumsaidia mwanamke kupata ujauzito na kujifungua salama.

Katika makala hii tutakuelezea magonjwa yote hatari ambayo yanaweza kushambulia mfumo wa uzazi wa mwanamke na kusababisha matatizo ya uzazi.

Magonjwa yanayosababisha mwanamke kushindwa kupata mimba

01: Tishu zinazounda tumbo la uzazi kukulia nje ya tumbo la uzazi (Endometriosis)

Endometriosis ni ugonjwa unaotokea pale ambapo tishu zinazounda ukuta wa mfuko wa uzazi zinasafiri na kujishikiza maeneo menginge ya jirani na mfumo wa uzazi.

Baadhi ya maeneo yanayoathiriwa na tatizo hili ni pamoja na kibofu, mirija ya falopia, katika ovari, katika misuli ya kuta za mfuko wa uzazi na katika uke.

Zikiwa katika maeneo haya tishu hizi huendelea kukua, ukuaji huu unapelekea kutengenezwa kwa uvimbe na vidonda ambavyo husababisha damu nyingi kutoka.

Ikiwa tishu hizi zitajishikiza katika mirija ya falopia, husababisha kuziba kwa mirija hii, hivyo kuzuia yai kupita kutoka katika ovari kuelekea katika mfuko wa uzazi.

Kuzuiwa kwa yai kunasababisha mimba kutunga nje ya kizazi, moja ya tatizo hatari ambalo linaweza kusababisha hata kifo kwa mama ikiwa halitagundulika mapema.

Kwa sehemu kubwa tatizo hili la Endometriosis husababishwa na tishu za mfuko wa uzazi kusambaa kupitia tukio la mzunguko wa hedhi.

Ambapo damu ya hedhi huwa na mchanganyiko wa tishu hizi kutoka katika mfuko wa uzazi, iwapo damu hii itafika maeneo mbalimbali ya karibu na mfumo wa uzazi, tishu ndani ya damu hii zinaweza kujishikiza na kuendelea kukua.

Tatizo la Endometriosis linaweza kutibiwa kwa kutumia dawa za kuthibiti homoni za uzazi.

02: Ugonjwa wa PID (Maambukizi ya bakteria katika via vya uzazi)

Pelvic inflammatory disease (PID) ni maradhi ya uvimbe katika via vya uzazi.

PID inaweza kuathiri eneo lolote la mfumo wa uzazi, kuanzia mlango wa uzazi, mfuko wa uzazi, mirija ya falopia hadi kiwanda cha mayai (ovari).

Mirija ya falopia ni miongoni mwa maeneo yanayoshambuliwa sana na PID, mashambulizi yanayopelekea uvimbe na kuziba kwa mirija hii.

Kuziba kwa mirija ya falopia ni sababu kuu ya tatizo la mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi.

Tatizo PID husababishwa na magonjwa ya zinaa hasa ugonjwa wa gono na chlamydia.

PID ni ugonjwa hatari hasa ile inayosababishwa na ugonjwa wa chlamydia, kwa sababu katika hatua za mwanzo ugonjwa huu wa chlamydia hauonyeshi dalili zozote.

Mara nyingi dalili za PID inayosababishwa na chlamydia huanza kuonyesha dalili wakati tayari mwanamke ameshakuwa mgumba.

Matumizi ya vitanzi kama njia ya uzazi wa mpango inaongeza uwezekano wa kupata PID.

Tatizo la PID linaweza kutibiwa lakini madhara ambayo tatizo hili litasababisha ni ngumu kuyatibu.

03: Uvimbe usio wa saratani katika tumbo la uzazi, uke na mlango wa uzazi (Fibroids na Polyps)

Fibroids na Polyps ni uvimbe usio wa saratani uliojaa nyama na misuli. Uvimbe huu unadhaniwa kusababishwa na homoni za oestrojeni kwa kiasi kikubwa.

Uvimbe huu unaweza kutokea sehemu yeyote ya mfumo wa uzazi lakini uke, mlango wa uzazi na tumbo la uzazi ndio maeneo ambayo huathiriwa zaidi.

Tatizo hili husababisha mimba kuharibika, kutokana na kusababisha yai lililorutubishwa kushindwa kujishikiza katika ukuta wa tumbo la uzazi.

Madhara ya uvimbe huu yanategenea na ukubwa wa uvimbe, ikiwa uvimbe ni mkubwa mwanamke anaweza kupata maumivu makali na kutokwa damu nyingi ya hedhi, maumivu wakati wa kujamiana na kutokwa damu mara kwa mara tofauti na ile ya hedhi.

Tatizo hili la uvimbe linaweza kutibiwa kwa kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe huu.

04: Uvimbe wenye usaha katika ovari (Ovarian cysts)

Uvimbe huu unaweza kutokea katika sehemu mbalimbali za ovari, unaweza kutokea katika vifuko vyenye mayai au vifuko ambavyo tayari vimeshatoa mayai.

Uvimbe huu huambatana na majimaji na usaha, unaweza kuwa mmoja au zaidi ya mmoja. Ikiwa utatokea zaidi ya mmoja husababisha ugonjwa wa polycystic ovarian syndrome (PCOS).

Sababu kubwa inayopelekea tatizo hili la uvimbe katika ovari ni kiwango kikubwa cha homoni za testosterone na LH (luteinizing) kinachozalishwa kutoka katika tezi ya pituitari.

Tatizo hili husababisha mayai kushindwa kukomaa na kupevuka. Kwa wanawake wenye tatizo hili dalili mojawapo kubwa ni kukosa hedhi kwa muda mrefu.

Kitambi, chunusi, tabia za kiume kwa wanawake (Mfano nywele kifuani na mgongoni) na kisukari ni miongoni mwa viashiria vya tatizo hili.

Tatizo hili linaweza kutibiwa kwa kutumia dawa za kurekebisha homoni, vilevile dawa za kuongeza uwezekano wa kushika mimba, mfano clomifene.

05: Maradhi ya fangasi sugu ukeni (Vulvovaginitis)

Vulvovaginitis ni uvimbe katika maeneo ya uke unaosababishwa na maambukizi ya fangasi sugu ukeni, unasababishwa na fangasi wa aina kuu mbili Candida albicans na Trichomonas vaginalis.

Fangasi sugu ukeni inaweza kusambaa na kuambukiza hadi maeneo ya ndani ya mfumo wa uzazi.

Kuambukizwa kwa maeneo ya ndani ya mfumo wa uzazi hupelekea mwanamke kuwa katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa mengine kama PID.

Vilevile maradhi ya fangasi ukeni hubadilisha hali ya chaji katika uke, kubadilika kwa hali ya chaji kunaweza kusababisha mbegu za kiume kufa kabla ya kufika maeneo ya ndani ya mfumo wa uzazi.

Tatizo hili linaweza kutibiwa na kupona kabisa kwa kutumia dawa za fangasi.

06: Maambukizi ya bakteria katika eneo la nje la uke (Bacterial vaginosis)

Bakteria na fangasi katika uke ni moja ya vimelea vya faida kwa sababu hufanya kazi mbalimbali ukeni, ikiwemo kuleta mlinganyo wa chaji katika uke, vilevile husaidia kuimarisha ulinzi wa uke dhidi ya vimelea vya magonjwa.

Miongoni mwa bakteria wa faida ukeni ni Gardnerella vaginalis na Mycoplasma hominis. Bakteria hawa wanapaswa kuwa katika mlinganyo.

Ikiwa mlinganyo utavurugika basi uke unaweza kutawaliwa na bakteria hatari kwa urahisi, bakteria ambao huweza kusababisha ugonjwa wa PID.

07: Uvimbe wa eneo la Bartholin katika uke (Bartholinitis)

Bartholinitis ni uvimbe wa tezi zinazozalisha majimaji na utelezi wa uke wakati wa kujamiana. Tezi hii inapatikana chini ya mashavu ya uke.

Tezi hizi zinaweza kuvimba ikiwa zitatawaliwa na bakteria, magonjwa ya zinaa na usafi duni. Ikiwa tezi hizi zitavimba zitapelekea mirija yake inayopitisha utelezi kuziba.

Kuziba kwa milija ya tezi ya Bartholin kunasababishwa kutengenezwa kwa uvimbe wenye usaha ambao huambatana na maumivu makali.

Maambukizi haya huweza kusambaa maeneo mengine ya mfumo wa uzazi na kusababisha tatizo la PID.

Tatizo hili la Bartholinitis linaweza kutibiwa na dawa za antibiotiki na kupona kabisa.

08: Magonjwa ya saratani

Sehemu yoyote ya mfumo wa uzazi wa mwanamke inaweza kuathiriwa na tatizo la saratani. Saratani husababisha uvimbe ambao unakuwa bila udhibiti.

Ukuaji huu unaweza kuanzia sehemu moja na baadae ukasambaa maeneo mengine ya mwili.

Baadhi ya saratani katika mfumo wa uzazi wa mwanamke ambazo huathiri wanawake wengi ni pamoja na saratani ya mlango wa kisazi, saratani ya ovari, saratani ya mfuko wa kizazi na saratani ya ndani ya uke.

Nchini Tanzania, takwimu zinaonyesha saratani ya mlango wa kizazi ni moja ya aina ya saratani ambayo huwasababishia wanawake wengi ugumba.

Saratani ya mlango wa kizazi inatibika ikiwa utawahi kuitambua.

08: Matatizo katika mzunguko wa hedhi

Mzunguko wa hedhi ni tukio la kibaolojia na la lazima kwa mwanamke. Kwa kawaida tukio hili hutokea mara moja kwa kila mwezi, yaani kila baada ya siku 28.

Tukio hili ndio ambalo huratibu utengenezwaji na upevukaji wa yai. Ikiwa kuna hitilafu zozote katika mzunguko wa hedhi, basi hitilafu hizi zinaweza kuathiri uwezo wa mwanamke kupata mimba.

Lakini pia hitilafu katika mzunguko wa hedhi inatoa ishara ya uwepo wa tatizo lingine ambalo linaweza kuwa chanzo cha mwanamke kushindwa kupata mimba.

Kwa mwanamke ni lazima kuzingatia mzunguko wako wa hedhi, ikiwa ni pamoja na kuratibu urefu wa mzunguko, mabadiliko ya kimwili na kiasi cha damu kinachotoka.

Baadhi ya matatizo ya hedhi ambayo yanaweza kuathiri uwezo wa mwanamke kupata mimba ni pamoja na;
  • Kupata damu nyingi ya hedhi. Mwanamke anapaswa kutilia shaka ikiwa anatoka damu nyingi wakati wa hedhi, zaidi ya mililita 100 za damu ni ishara ya uwepo wa tatizo.
  • Hedhi isiyo na mbangilio. Kutokupata hedhi katika mlolongo unaoeleweka ni ishara ya kuwepo kwa tatizo katika mfumo wa uzazi, mara nyingi husababishwa na mvurugiko wa homoni.
  • Kukosa hedhi. Kutopata hedhi kwa zaidi ya miezi 3 na kuendelea ni ishara ya uwepo wa tatizo katika mfumo wa uzazi.
  • Maumivu makali wakati wa hedhi. Ikiwa unapata maumivu makala ya tumbo na nyonga wakati wa hedhi kiasi cha kuathiri shughuli za kawaida za kila siku, ni ishara ya tatizo katika mfumo wa uzazi, mara nyingi tatizo hili husababishwa na ugonjwa wa PID.

Hitimisho

Haya ni magonjwa mbalimbali ambayo huathiri mfumo wa uzazi wa mwanamke. Kwa sehemu kubwa magonjwa haya yasipodhibitiwa husababisha tatizo la ugumba au utasa kwa mwanamke.

Mbali na magonjwa haya, mwanamke anaweza kupata tatizo la kushika mimba kutokana na matatizo ya kuzaliwa.

Mfano mwanamke kuzaliwa bila mfuko wa uzazi, au hitilafu za kimuundo za mfuko wa uzazi ambazo huathiri ukuaji wa mimba.

Kwa wanawake, magonjwa mengi yanayosababisha ugumba au utasa ni ngumu kuyatambua hasa katika hatua zake za awali, ni vizuri kuweka tamaduni za kufanya vipimo walau mara 1 kwa mwaka ili kubaini mapema ikiwa kuna tatizo.
Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url