Umuhimu wa kuanza mapema kliniki ya wajawazito

Baada ya mwanamke kupata ujauzito, kuna maswali mengi huwa yanaibuka kuliko majibu hasa ikiwa ni ujauzito wa kwanza.

Mwanamke huwa na furaha na shauku ya kutaka kujua mambo mengi kuhusu ujauzito. Ndugu, jamaa na marafiki huwa ni miongoni mwa watu wa kwanza kufikiwa kwa ajili ya ushauri.

Unaweza kupata ushauri wa kila aina kutoka kwa watu hawa, kuna watakaokupa ushauri kutokana na uzoefu, wengine watatoa ushauri kulingana na tetesi na ikiwa miongoni mwa ndugu, jamaa na marafiki zako ni wataalamu wa afya basi unaweza kupata ushauri sahihi zaidi na wa kitaalamu.

Ushauri unaopata unaweza kuwa ni mzuri, lakini ushauri sahihi utaupata kutoka kwa wataalamu wa afya, si tu ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya ni sahihi lakini pia ni wa uhakika kwa sababu wataalamu hawa wanaweza kutumia vipimo ili kujiridhisha na ushauri wanaotoa.

Hii ndio sababu kubwa ni kwanini unashauriwa kupata ushauri juu ya utunzaji wa ujauzito kutoka kwa wataalamu wa afya.

Inashauriwa kuhudhulia kliniki ya kwanza ndani ya wiki 12 za mwanzo za ujauzito. Na walau uhudhurie kliniki zisizopungua 4 katika kipindi chote cha ujauzito.

Si salama kupata ushauri katika kipindi hiki kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Umuhimu wa kuhudhuria kliniki ya wajawazito mapema

Kuna faida nyingi za kuhudhulia kliniki mapema baada ya kupata ujauzito, hasa wiki 12 za mwanzo. 

Baadhi ya faida ambzo utazipata ni pamoja na;

  • Ushauri sahihi juu ya lishe bora kwa mjamzito
  • Ushauri sahihi na njia za kujikinga na magonjwa kipindi cha ujauzito
  • Kupata vipimo vya UKIMWI bure
  • Ushauri sahihi juu ya usafi na jinsi ya kujitunza wakati wa ujauzito
  • Utapata ushauri sahihi juu ya namna nzuri za kufanya mapenzi salama kwako na kwa mtoto
  • Ushauri juu ya vitu gani utumie na vitu gani usitumie
  • Utapata chandalua chenye dawa ili kujikinga na malaria bure
  • Utapewa tiba za kujikinga na matatizo mbalimbali yanayoweza kuathiri afya ya mtoto, Mfano minyoo na kifafa cha mimba
  • Ushauri juu ya virutubisho sahihi kwa ajili ya ukuaji wa mimba
  • Utapata vipimo muhimu kama vile kuangaliwa kiwango cha damu, magonjwa ya zinaa, homa ya ini, utapiamlo, malaria, kifua kikuu, magonjwa ya moyo na kufahamu kundi la damu
  • Utapewa chanjo muhimu ikiwa bado hujapata ili kumlinda mtoto, Mfano chanjo ya ugonjwa wa Rubella

Mambo ya kuzingatia kwa mjamzito wakati wa kwanza kliniki

Kabla ya kuhudhuria kliniki kwa mara ya kwanza, mama mjamzito anapaswa kuwa na taarifa sahihi za mambo yafuatayo;

  1. Taarifa muhimu za ujauzito zilizopita ikiwa si ujauzito wa kwanza
  2. Urefu wa mzunguko wako wa hedhi
  3. Mara ya mwisho kupata hedhi
  4. Ikiwa unatumia dawa za kupanga uzazi
  5. Kama kuna dawa zozote unatumia
  6. Ikiwa una tatizo lolote la mzio (aleji)
  7. Ikiwa umewahi kufanyiwa upasuaji wa aina yeyote
  8. Mazingira yako kwa ujumla ikiwa ni pamoja na maeneo unayoishi na shughuli unazofanya
  9. Mtindo wa maisha, ikiwa ni pamoja na chakula unachopenda, matumizi ya pombe na sigara
  10. Historia ya familia, ikiwa kuna magonjwa ya kurithi katika familia au ukoo
  11. Ikiwa una magonjwa sugu kama vile kisukari, shinikizo la damu, UKIMWI na msongo wa mawazo

Hitimisho

Kuhudhuria kliniki kwa wajawazito ni nguzo muhimu ya kuboresha afya ya mama na mtoto.

Unashauriwa kuhudhuria kliniki walau mara 4 katika kipindi chote cha ujauzito, idadi ya mahudhurio inatofautiana kati ya wanawake.

Zipo sababu kadhaa zinaweza kuathiri ni kwa namna gani unapaswa kuhudhuria kliniki, kwa baadhi ya wanawake anaweza kupangiwa kuhudhuria kliniki mara nyingi iwezekanavyo ikiwa wataalamu wa afya wataona inafaa.

Hudhuria kliniki mapema iwezekanavyo, kuchelewa kufanya hivyo ni hatari kwako na kwa mtoto aliyeko tumboni, kwa sababu baadhi ya matatizo ya uzazi yanapaswa kutatuliwa mapema iwezekanavyo.

Ikiwa utachelewa kuanza kuhudhuria kliniki, baadhi ya matatizo yanaweza kuleta madhara makubwa ya kiafya kwako na kwa mtoto ikiwemo kifo.

Next Post Previous Post
No Comment
Andika Swali au Maoni
comment url